Dodoma. Watu wawili wamefariki dunia akiwamo muuguzi wa Kituo cha Afya cha Haneti, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Rhoda Mitinda wakati akimsindikiza mjamzito kwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza na Mwananchi, leo Jumapili Desemba mosi 2024, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo alfajiri ya Novemba 30 mwaka huu.
Amesema ajali hiyo ilihusisha gari la kubebea wagonjwa la Kituo cha Afya cha Haneti, wilayani Chamwino aina ya Toyota Land Crusser lililokuwa likiendeshwa na dereva Mazoea Nampanga (64) aliyegonga lori kwa nyuma lililokuwa limeegeshwa pembeni mwa barabara.
Amewataja waliofariki dunia papo papo kuwa ni Muuguzi wa Kituo cha Afya Haneti, Rhoda Mitanda (30) na ndugu aliyekuwa akimsindikiza mgonjwa Issabela Malimo (64) huku majeruhi kwenye ajali hiyo wakiwa ni dereva wa gari ya wagonjwa Nampanga na mjamzito Patricia Paulo.
“Ni kweli kuna ajali iliyotokea maeneo ya Mayamaya alfajiri ni ambulance (gari ya kubebea wagonjwa) ilikuwa imebeba mjamzito ikimuwahisha kwenye matibabu katika Hospitali ya Dodoma. Ilipofika maeneo hayo gari ikawa imeacha njia na kugonga gari lililokuwa pembeni ambalo ni lori,” amesema.
Kamanda huyo amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi, hivyo dereva kushindwa kulimudu gari hilo na kugonga gari lililokuwa limeegeshwa pembeni mwa barabara.
“Tunamshikilia dereva wa ambulance kwa maana alikuwa anatakiwa kuchukua tahadhari kwa kuendesha gari kwa uangalifu, kwa sababu wakati anamuwahisha mgonjwa alipaswa kuchukua tahadhari. Tunamshikilia kwa mahojiano zaidi,” amesema.
Amesema dereva yuko chini ya uangalizi wa polisi wakati akipatiwa matibabu.
“Tunataka tuondoe hiyo fikra kuwa mwanzo wa mwaka, mwisho wa mwaka kunatokea ajali Jeshi la Polisi la Mkoa wa Dodoma tumeshajipanga, mtu yeyote atakayekiuka sheria za barabarani lazima tuchukue hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine,” amesema.
Amesema wamejipanga kwa kufanya ukaguzi na kuweka askari katika vituo mbalimbali, kuhakikisha watu wanazingatia sheria za barabarani na amewataka kuelimisha wananchi.
Amewataka watumiaji wa barabara kuzingatia sheria na kuchukua tahadhari ya juu hasa wakati huu mvua zinaponyesha mkoani Dodoma.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Alexander Petro amesema ajali hiyo ilitokea alfajiri wakati gari la wagonjwa likitokea Haneti kuelekea jijini Dodoma likiwa na mgonjwa.