SERILIKA KUZINDUA MPANGO KAZI WA KULINDA WENYE UALBINO-WAZIRI RIDHIWANI KIKWETE

 

 

Na, Mwandishi Wetu – Dar Es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Rihiwani Kikwete amesema Serikali imekamilisha uandaaji wa mpango kazi wa Taifa wa haki na Ustawi kwa watu wenye Ualbino na Mkakati wa Kitaifa wa Teknolojia Saidizi kwa watu Wenye Ulemavu ambao unatarajiwa kuzinduliwa Disemba 3, 2024.

Mhe. Ridhiwani amesema hayo kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa jana tarehe 30 Novemba, 2024 wakati wa matembezi ya hisani ya kukuza uelewa kuhusu Watu wenye Ualbino na harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya kundi hilo ambapo amesema miongozo hiyo itasaidia kulinda Watu Wenye Ualbino.

Aidha Mhe. Kikwete amesema  serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya kwa watu wenye ulemavu wakiwemo wenye Ualbino kwa kujenga vituo vya kutolea huduma za afya vilivyo na miundombinu rafiki  ambapo hadi kufikia machi 2024 tayari vituo 12,266 vimejengwa.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania Godson Mollel ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwalinda na kukamilisha mpango kazi wa Taifa wa haki na Ustawi kwa watu wenye Ualbino.

Matembezi hayo ya hisani ya Sunset Walk yamelenga kukuza uelewa kuhusu Watu wenye Ualbino ambayo yamefanyika Jijini Dar es salaam kuanzia Hospitali ya Ocean Road hadi Daraja la Tanzanite.

Related Posts