KIUNGO Mkongomani Fabrice Ngoma, ambaye mwanzoni alionekana kutokuwa katika sehemu ya mipango ya Kocha wa Simba, Fadlu Davids, ameibuka kuwa lulu katika safu ya kiungo ya timu hiyo.
Msimu huu wa Ligi Kuu Bara ulioanza kwa changamoto kadhaa kwa kiungo huyo, lakini sasa Ngoma ameonyesha uwezo mkubwa akichangia moja kwa moja kurejesha uwiano katika eneo la kiungo cha kati. Hatua hiyo imeiwezesha Simba kuvuna pointi 15 kwenye michezo mitano iliyopita ya ligi.
Ngoma ambaye mwanzoni alionekana kuwa kwenye orodha ya wachezaji waliokuwa wanapigiwa chapuo la kuachwa katika dirisha dogo la usajili, amejibu shaka hizo kwa vitendo.
Katika michezo mitano mfululizo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons, Namungo, Mashujaa, KMC, na Pamba Jiji, Simba haijaruhusu bao hata moja wakati Ngoma akiwa sehemu ya kikosi cha kwanza.
Uwepo wake umerudisha uthabiti katika eneo ambalo awali lilionekana kusuasua kutokana na majeraha ya Mzamiru Yassin na Yusufu Kagoma pamoja na changamoto za kiufundi za Débora Fernandes na Augustine Okejepha.
Simba ilianza msimu kwa kasi, lakini ilipoteza uwiano katika michezo ya mwanzo, hasa kwenye eneo la kiungo mkabaji. Upungufu wa uzuiaji mbele ya mabeki ulijidhihirisha zaidi katika mechi dhidi ya Coastal Union iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2 na Yanga ambayo Simba ilifungwa 0-1 ikiruhusu mabao muhimu.
Fadlu katika kutafuta suluhu ya haraka, aliamua kumpa nafasi zaidi Ngoma. Hatua hiyo imeonyesha mafanikio makubwa, huku Ngoma akifanikiwa kulinda vizuri safu ya mabeki ya Simba.
Katika dakika 384 alizocheza kwenye michezo mitano ya ligi, Ngoma ameonyesha uwezo wa juu wa kuzuia mashambulizi ya wapinzani.
Simba imebaki na rekodi ya kutoruhusu bao, hali inayoashiria mchango wake mkubwa katika kuimarisha eneo hilo muhimu.
Kwa sasa Ngoma amekuwa chaguo la kwanza kwenye mfumo wa 4-2-3-1 wa Fadlu, huku kibarua kikiwa kwa Mavambo na Okejepha ambao wanapigania nafasi ya kuanza naye kulingana na mahitaji ya mchezo.
Mbali na Ligi Kuu Bara, Ngoma ameonyesha umuhimu wake pia katika mashindano ya kimataifa.
Katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya F.C. Bravos do Maquis, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 kupitia penalti iliyofungwa na Jean Charles Ahoua. Ngoma alicheza kwa nidhamu kubwa, akionyesha uwezo wa kusoma mchezo na kudhibiti kasi ya wapinzani, jambo lililompa nafasi ya kuwa mchezaji tegemeo kwa kocha Fadlu.
Kiwango bora cha Ngoma kimeweka bayana tofauti kati ya uwezo wa kiungo huyu Mkongomani na wenzake wa nafasi hiyo.
Mavambo ametumika kwa dakika 194 tu katika michezo mitano iliyopita ya ligi, huku Okejepha akicheza dakika 302 wakati Ngoma akizikata dakika 317. Hii inaonyesha jinsi Ngoma alivyoaminiwa zaidi, hasa katika mechi muhimu zinazohitaji uthabiti wa kiufundi.
Kocha Fadlu ameeleza kuwa mabadiliko ya mara kwa mara kwenye kikosi chake ni sehemu ya mipango ya kiufundi ya timu.
“Ninafurahia kile ambacho wachezaji wangu wamekuwa wakitoa. Tuna nafasi ya kukua zaidi kama timu, na mabadiliko tunayofanya yanatokana na mahitaji ya kila mchezo,” alisema Fadlu, akionyesha kuridhishwa na mchango wa wachezaji wake.
Ngoma pia amepongezwa na kocha wa Bravos, Mário Soares ambaye alisema: “Ni mchezaji mzuri mwenye uwezo mkubwa wa kuchezesha timu na kulind. Pia anaonekana kuwa na uzoefu mkubwa.”
Kwa upande wake, Florent Ibengé, kocha mwenye uzoefu mkubwa Afrika alisema: “Ngoma tayari amethibitisha ubora kwa kucheza kwenye kiwango cha juu katika Ligi ya Tanzania. Sidhani kama kuna haja ya kumuelezea zaidi. Ni kati ya wachezaji ambao navutiwa nao sana. Anajua kumiliki eneo lake.”
Ngoma kwa sasa ni mfano wa wachezaji ambao huchukua changamoto kama fursa ya kuthibitisha thamani yao. Badala ya kukata tamaa alipokuwa akionekana kutopewa nafasi. Hatua hii si tu imempa nafasi kubwa ya kucheza, bali pia imeimarisha imani ya benchi la ufundi na mashabiki wa klabu hiyo.