Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wamesema sio pombe na virusi vya homa ya ini ndiyo vinavyoweza kuathiri ogani hiyo, bali hata matumizi ya vinywaji vyenye sukari huiweka hatarini.
Hiyo ni kutokana na kile walichoeleza kuwa, sukari inapozidi mwilini hutengeneza mafuta ambayo mbali na kuathiri sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo moyo pia ini huwa katika hatari zaidi.
Wametoa kauli hiyo ikiwa ni siku saba tangu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kutangaza kuanza upandikizaji wa ini ifikapo mwaka 2025 wakati ambao tayari wagonjwa 607 wanahitaji upandikizaji wa ini nchini.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Desemba mosi 2024, daktari bingwa wa mfumo wa chakula na ini kutoka Muhimbili, Dk John Rwegasha amesema mbali na pombe na virusi vinavyosababisha homa ya ini, pia vitu vya sukari vyote kwa jumla vinavyochangia kuongeza uzito huweza kumuweka mtu hatarini kupata ugonjwa wa ini.
Miongoni mwa vyakula hivyo ni vile vilivyo katika makundi ya wanga, vyakula vya mafuta huku watumiaji wakiwa hawafanyi mazoezi.
“Sukari iliyozidi mwilini mara nyingi hubadilishwa na kuwa mafuta, mafuta haya huingia katika sehemu mbalimbali za mwili na huathiri mfumo mzima wa metabolisim,” amesema Dk Rwegasha.
Amesema mafuta hayo yanapofika kwenye ini ambalo kwa kawaida huwa na rangi ya kahawia hulifanya lishindwe kufanya kazi kama inayotakiwa.
Na katika mafuta hayo, amesema baadhi huanza kuunguza ini kama ilivyo athari zinazosababishwa na pombe na virusi vya homa ya ini.
“Hili linalifanya ini kusinyaa. Hivyo ni vyema kukumbuka kuwa unapotumia vitu vinavyoongeza uzito kanuni yake ni moja tu kutofurahia kuongezeka. Kila kitu kikizidi kiwango ni hatari. Tunashauriwa kutofanya kwa kiasi kikubwa, kama pombe ukiweza acha au punguza,” amesema Dk Rwegasha.
Ametolea pia mfano wa soda akisema haijazuiwa mtu asinywe, lakini kuna kiwango ambacho kimewekwa kwa ajili ya matumizi tofauti na mtu kunywa soda tatu hadi nne bila kufanya mazoezi.
“Hali hii inafanya mtu anaanza kuongezeka uzito na mwisho wa siku unazalisha mafuta ambayo yanakimbilia kwenye ini na kuleta athari,” amesema Dk Rwegasha.
Maneno yake yanaungwa mkono na Dk Boaz Mkumbo kutoka Sayansi ya Mapishi ambaye amesema matumizi ya vimiminika vya sukari kama kunywa soda, juisi za viwandani na za kukamua nyumbani hata ambazo haziongezwi sukari huweza kuathiri ini la mtu.
Hiyo ni kutokana na kusababisha mrundikano wa mafuta kwenye ini na kulifanya lishindwe kudhibiti kiwango cha rehemu kinachohitajika mwilini.
“Hii ikiwa na maana kuwa mtu anayesumbuliwa cholesterol isiyoshuka anatakiwa kudhibiti kitu kinacholeta mrundikano wa mafuta kwenye ini ikiwamo soda, juisi za viwandani na nyumbani zinazokamuliwa. Wengine wanajitetea kuwa nakamua tu embe, ndizi, tikiti siweki sukari,”
“Sukari ni sukari na mwili hautakiwi kurundika sukari kwa mkupuo kwa sababu hiyo itaufanya mwili kuchukua sukari ya ziada na kuhifadhi kuwa mafuta,” amesema.
Hata hivyo, mbali na matumizi ya vitu vya sukari magonjwa ya ini yana vyanzo mbalimbali ambavyo asilimia kubwa yanatokana na mitindo ya maisha katika matumizi ya vyakula, vinywaji au bidhaa zenye kemikali (sumu).
Matumizi makubwa ya vilevi na sigara, dawa zenye kemikali, virusi aina ya hepatitis A, hepatitis B, na hepatitis C, unene na uzito uliopitiliza, kurithi, kutokula au kunywa vitoa sumu mwilini kama maji pamoja na tatoo au kutoboa mwili.
Ikiwa ini litaharibika, utahitaji upandikizaji na ikiwa utapata mchangiaji ndugu gharama za upandikizaji hutegemea na hospitali na huanzia Dola 25,000 za Marekani(Sh69.9 milioni) na iwapo utanunua katika soko la viungo thamani yake inafikia Dola za Marekani 557,000 (Sh1.4 bilioni).
Aina nyingi za magonjwa ya ini hazionyeshi dalili au dalili katika hatua za mwanzo.
Dalili huonekana wakati ini tayari limeharibiwa au lina makovu. Mgonjwa hujisikia uchovu wa kudumu, kupungua kwa hamu ya kula, kubadilika kwa rangi ya mkojo, rahisi kuvunjika hasa mifupa, kuvimba kwa mguu na kifundo cha mguu.
Nyingine ni kutapika, ngozi inayowaka au kung’aa sana, kuvimba na maumivu ndani ya tumbo, kinyesi kuwa na rangi ya lami au kama udongo, rangi ya njano ya macho na ngozi.
Ili kuepuka hali hii, Dk Rwegasha amesema mtu anatakiwa kujenga tabia ya kufanya mazoezi ili kuyeyusha sukari inayoingia mwilini inayoweza kuzalisha mafuta yenye athari.