Taoussi aziwekea mtego Simba, Yanga

UNAWEZA kuona kama ni mapema hivi, lakini sio kwa kocha wa Azam FC Rachid Taoussi ambaye rekodi za kikosi chake zinazimpa jeuri na kusema mpango wake mpya ni dhidi ya Simba na Yanga.

Azam kufikia sasa msimu imecheza mechi 12 za ligi, imeshinda nane, sare tatu na kupoteza moja dhidi ya Simba. Kati ya mechi ilizoshinda, iliizamisha Yanga 1-0 na kulipa kisasi cha kufungwa 4-1 na timu hiyo ya Jangwani katika mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii.

Rachid ameanza kwa kufundisha kikosi hicho kwa mafanikio makubwa, tangu atue Azam amecheza mechi 11 akipokea kijiti kutoka kwa kocha Youssouph Dabo.

Akizungumza na Mwanaspoti, alisema kwake jambo la muhimu zaidi kwa sasa ni kutengeneza saikolojia ya wachezaji wake kujiona wana uwezo mkubwa.

Alisema ameikuta Azam ina mastaa wazuri wenye vipaji lakini bado zipo timu ambazo zinaweza kuwatikisa kiwepesi, hali ambayo hapendelei kuiona katika kikosi chake.

“Mpango nilionao ni mmoja tu wa kuhakikisha kikosi changu kinapita katikati ya Simba na Yanga, kwani hizo ndio timu pekee zinazoonekana tishio kwenye ligi lakini sio kwetu.

“Ni wazi kuwa Azam ni timu kubwa na ina wachezaji wenye viwango kama ilivyo kwa timu hizi mbili hivyo hatuna sababu ya kutufanya tusiwashinde.”

Azam ndio iliyofungua mlango wa gundu kwa Yanga, baada ya kuwafunga bao 1-0 na baadaye timu hiyo ya wananchi kupoteza mechi nyingine mbili.

Related Posts