Dar es Salaam. Ushindani wa hoja, vijembe na misimamo ya kisiasa, ni miongoni mwa mambo yaliyoshuhudiwa katika mdahalo uliohusisha viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokraisa na Maendeleo (Chadema), ACT Wazalendo pamoja na mwanasheria.
Mdahalo huo uliolenga kujadili tathmini ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024, umefanyika ikiwa zimepita siku tano tangu kufanyika kwa uchaguzi huo, Novemba 27, 2024.
Ushindi wa asilimia 99.01 wa CCM katika uchaguzi huo wa vijiji, vitongoji na mitaa ndiyo iliyokuwa hoja kuu ya chama tawala, huku vyama vya upinzani vikijenga hoja kuonyesha uharamu wa mchakato na uchaguzi wenyewe kwa ujumla.
Kwa upande wa taaluma ya sheria, mwanasheria alisimama kuweka muktadha wa kisheria juu ya kila hoja iliyotolewa kwenye mdahalo huo.
Katika mdahalo huo, CCM iliwakilishwa na mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo, Chadema iliwasilishwa na Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Boniface Jacob huku ACT Wazalendo ikiwakilishwa na makamu mwenyekiti wake Bara, Issihaka Mchinjita.
Wakili Peter Madeleka ndiye aliyekuwa akitoa tafsiri za kisheria na kikatiba kulingana na kila kinachozungumzwa.
Hayo yameshuhudiwa usiku wa jana Jumamosi, Novemba 30, 2024 katika mdahalo ulioendeshwa na kipindi cha Medani za Siasa kinachorushwa na kituo cha runinga ya Star TV.
Uhalali, uharamu wa uchaguzi
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu Boni Yai, ameukosoa mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, akisema umeunyima upinzani haki ya kuingia katika ushindani.
Kwa sababu ya mazingira hayo, amesema haoni kama upinzani umeshindwa na CCM imeshinda kwa kuwa hakukuwa na ushindani.
“Sisi hatuwezi kusema CCM wameshinda na Chadema wameshindwa, hapakuwa na ushindani kwa sababu mazingira ya ushindani hayakuwepo,” amesema.
Kwa mujibu wa Jacob, ukiengua wagombea wengi zaidi ya uliowaacha unafifisha ushindani, badala yake chama tawala kilijitangazia ushindi.
“Kwa mantiki hiyo, uchaguzi huu mimi nasema ni batili, unakosa uhalali wa kisiasa, ndiyo maana unaona wameshinda (CCM) lakini hawana furaha,” amesema na kuongeza kuwa uchaguzi huo hauna uhalali wa kisheria na kimaadili.
Mtazamo wa Jacob hakutofautiana na Mchinjita aliyesema hakukuwa na uchaguzi, isipokuwa dola iliwakabili wananchi na kupoka mamlaka yao ya kuamua nani awe kiongozi wao.
Katika mchakato huo, amesema tangu wakati wa utungaji wa kanuni, kulishuhudiwa uamuzi wa Bunge wa kutaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) isimamie uchaguzi, ukikiukwa.
“Pia ulikwenda kinyume na makubaliano ya kikosi kazi ambacho kiliazimia maboresho ya sheria za uchaguzi mahususi kabisa kwa ule wa serikali za mitaa,” amefafanua.
Amesema kulitolewa sharti kwa Bunge kutunga sheria ya kuipa INEC mamlaka ya kuusimamia uchaguzi huo na hilo halikutekelezwa.
Hata uamuzi wa mahakama kuruhusu Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) iendelee kusimamia uchaguzi huo, amesema unakwenda kinyume na majadiliano na makubaliano mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mchinjita, mambo yaliendelea hata wakati wa uandikishaji, akidai Tamisemi iliwaandikisha hadi wasio hai na baadhi wasiokidhi umri.
Katika uchukuaji wa fomu, amesema kulishuhudiwa uenguliwaji wa wagombea, kwa ACT Wazalendo zaidi ya 5,000 walikumbwa na hilo.
Wakati vyama vya upinzani vikitoa malalamiko hayo, Profesa Mkumbo ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji amesema kuna ishara kwamba vyama hivyo havikuwa vimejiandaa kwa uchaguzi.
Hilo linatokana na ufafanuzi wake kuwa asilimia 75 ya vitongoji kabla ya kuenguana, CCM ilikuwa mgombea pekee.
Vivyo hivyo, amesema asilimia 65 ya vijiji chama hicho tawala kilikuwa na mgombea pekee na hata katika mitaa asilimia 35 CCM ilikuwa pekee.
“Hata kabla ya kuenguana, tayari CCM ilikuwa mbele kwenye vitongoji, vijiji na mitaa,” ameeleza.
Pamoja na hayo, amesema katika mchezo wowote huwa na kanuni, huku akisisitiza tatizo kubwa ni maandalizi.
Ameijenga hoja yake hiyo akitolea mfano chama chake cha CCM, kilichoanza maandalizi kwa kuandikisha wanachama wake.
Pia amesema chama hicho kilihakikisha wanachama wao wote wanakwenda kujiandikisha na wagombea walifundishwa masuala ya kisheria.
“Hoja hapa ni kwamba hawakujiandaa, pili hawakuenguliwa na CCM walienguliwa na vyombo husika. Pia, wafuatilie kwanini walienguliwa, ili upige kura lazima uwe mkazi wa eneo husika, lakini unakuta mtu katoka Temeke anagombea Manzese,” amesema.
Profesa Mkumbo aliyezungumza kwa niaba ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amesema kuna kanuni za uchaguzi lazima zisimamiwe.
Ukiachana na mtazamo ya kisiasa, kuna makosa ya kisheria katika uchaguzi huo, ikiwemo kutoupa mchakato huo misingi ya kikatiba kama inavyoelezwa na Madeleka.
Amerejea Ibara ya 74 ya Katiba ya Tanzania, inayotaja chaguzi za wabunge, madiwani na Rais na namna utakavyosimamiwa.
Kukosekana kwa misingi ya kikatiba kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, amesema ndiko kunakosababisha kutungwa sheria zisizolenga kuhakikisha unaendeshwa kidemokrasia.
“Demokrasia imetajwa na ibara ya 3 ya Katiba kama mambo yatakayoendeshwa na nchi kupitia vyama vya siasa, unapokosa msingi wa kikatiba unatoa mwanya kwa Bunge kutunga sheria wanazozijua wao,” amesema.
Hata hivyo, amesema uwepo wa sheria ni jambo moja, lakini uhalali wake unapimwa iwapo kuwepo kwake kunasababisha watu kupata haki.
Amesema nchi inaweza kujisifu kuendesha mchakato kwa mujibu wa sheria, lakini jambo la ajabu ni kwamba sheria yenyewe haikuwa inatenda haki.
Katika maelezo yake, amejibu hoja ya Profesa Mkumbo kuhusu upinzani kukosa maandalizi, akisema uhalali wa uchaguzi hautokani na kujiandaa kwa vyama, bali uhalali wa michakato.
Amedai kuna baadhi ya maeneo kuna askari walikamatwa wakiwa na kura, wapo wagombea waliopigwa, mambo ambayo hayana uhusiano na vyama kujiandaa.
Akitoa msimamo wa ACT Wazalendo, Mchinjita amesema ni kutaka uchaguzi urudiwe na tayari wamechukua hatua kadhaa, ikiwemo kuwataka Watanzania wasitoe ushirikiano kwa viongozi hao.
“Pili tumeshawaandikia barua vyama wenzetu wa upinzani ili tukutane na tutafute mustakabali mpya wa uchaguzi katika nchi yetu kwa sababu tumekuwa tukicheza shere kuanzia mwaka 2019,” amesema.
Kuhusu viti walivyoshinda, Mchinjita amesema ACT Wazalendo watakwenda mahakamani kwenye maeneo yote ambayo wagombea wao walienguliwa.
Hata hivyo, amesema ushindi wa CCM katika uchaguzi huo si jambo la kujivunia kwa kuwa imetumia nguvu ya dola.
“Ni upungufu wa akili kuamini katika mazingira haya ambayo demokrasia imekuwa nchini kwetu, eti CCM imeshinda kwa asilimia 99,” amesema.
Kwa upande wa Jacob, amesema CCM yenyewe inaondoa uhalali wa wananchi kuuamini na kuwa na hamu ya uchaguzi.
Madhara yake, amesema ni mabaya kwa sababu wananchi watakata tamaa na kuona kuwa uchaguzi hauwapi nafasi ya kupata kiongozi wanayemtaka.
“CCM ina wenyeviti wengi hata kidato cha nne hawajafika, lakini CCM ya Profesa Kitila inaondoa hadi wasomi eti hawajui kusoma na kuandika, kuna wakili ameondolewa eti hajui kusoma na kuandika, kuna mwalimu mkuu mstaafu ameondolewa eti hajui kusoma na kuandika kweli?” amehoji.
Kwa mujibu wa Jacob, haoni matumaini ya kufanyika kwa uchaguzi huru na haki mwakani kutokana na kilichotokea kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
Katika maelezo yake, Profesa Mkumbo amesema kwa mtazamo wake uchaguzi huwa na hatua mbili ambazo ni mchakato na matokeo.
Katika ufafanuzi wake, amesema mchakato umehusisha tangazo, hamasa ya kujiandikisha, kampeni, kupiga kura na baadaye matokeo na kwamba vyama vyote vya siasa vilishiriki.
“Malalamiko yanaweza kuwepo, lakini muhimu ni kwamba utaratibu wa kisheria unaohusu uchaguzi husika uwe umezingatiwa,” amesema.
Hata baada ya kutangazwa matokeo, amesema upo utaratibu wa kisheria kwa walalamikaji kwenda kutafuta hatua ya kutafuta haki kwingineko.
Akitoa msimamo wake, Madeleka amesema ni vigumu kuwa na uchaguzi huru ikiwa mifumo ya kiutawala itabaki kama ilivyokuwa enzi za siasa za chama kimoja.
Amesema kuna haja ya kurudi kwenye ripoti ya Tume ya Jaji Nyalali iliyopendekeza namna mifumo ya kisheria inapaswa kubadilika kuendana na siasa za vyama vingi.
Ameeleza hofu yake kuona Tanzania inaingia katika uchaguzi mkuu mwakani akirejea yaliyotokea katika chaguzi zilizopita.
“Kama kuna sababu yoyote inayosababisha tushindwe kukaa pamoja kupata muafaka wa kitaifa kubadilisha chaguzi zetu. (CCM) wakae madarakani watawale hadi watakapochoka,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu wagombea waliouawa, Profesa Mkumbo ameeleza msimamo wa CCM ni kusikitishwa na kulaani mauaji yanapotokea.
Sambamba na hilo, ameeleza uchaguzi unapaswa kuwa tukio jema la kuwapatia viongozi.
“Nitumie nafasi hii kulaani matukio yaliyotokea na nitake vyombo husika vifanye uchunguzi na kwa kweli hatua za kisheria zichukuliwe kwa wanaohusika,” amesema.
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, mauaji si jambo jema kwa nchi na CCM inalaani na kutaka hatua za kisheria zichukuliwe ili wahusika watiwe hatiani.
Katika maelezo yake, Madeleka amesema kutokana na changamoto za uchaguzi, wanasheria walitimiza wajibu wao wa kwenda mahakamani kupinga sheria zilizotungwa bila dhamira ya kuendesha uchaguzi kwa haki.
Pamoja na jukumu hilo, ameeleza mifumo mibovu ya haki jinai imesababisha kutoa hukumu iliyohalalisha sheria hizo.
Katika mdahalo huo, Jacob alirusha kijembe kwa Profesa Mkumbo, akisema hata uamuzi wa CCM kumtuma msomi huyo ni kiburi cha madaraka.
Hoja yake hiyo inatokana na alichoeleza kuwa CCM ina uongozi wake, kwanini imtume waziri ambaye ni mtumishi wa wananchi kushiriki mdahalo huo.
“Hata (Mohamed) Mchengerwa (Waziri Tamisemi) muda gani aliacha kuwa waziri na muda gani aliacha kuwa CCM,” amesema.
Kadhalika, amehoji CCM imepataje asilimia hizo za kuwa mgombea pekee katika baadhi ya mitaa, vijiji na vitongoji.
Hata hivyo, amelijibu mwenyewe swali hilo akisema, wamepata kwa watendaji kufunga ofisi siku za kutoa fomu, siku za kurudisha ofisi zilifungwa na kugoma kutoa fomu kwa wapinzani.
Licha ya mazingira hayo, amesema bado matokeo yalitangazwa kwa mtutu wa bunduki.
Hata hivyo, Profesa Mkumbo amekana kuwa mtumishi wa umma akisema ana nafasi ndani ya CCM na uanasiasa wake unampa haki ya kuwa sehemu ya mjadala.
Amesema uchaguzi huo umeendeshwa kwa mujibu wa sheria na kwa mtazamo wake hakuna uchaguzi usio na kasoro.
Imani yake ni kile alichofafanua, uchaguzi wowote unatoa nafasi ya kujiandaa na uchaguzi mwingine.
Amesema walioshindwa katika uchaguzi huo, ni kwa sababu hawakujiandaa na alitupa kijembe kwa Chadema akisema itakuwa vigumu kushinda katika mazingira ambayo chama kina migogoro kati ya mwenyekiti (Freeman Mbowe) na makamu wake (Tundu Lissu).
Alipoulizwa iwapo kuna kasoro aliyoiona katika uchaguzi huo, Profesa Kitila amesema ni katika baadhi ya maeneo idadi ya waliojitokeza kupiga kura hailingani na waliojiandikisha.
Kinachohalalisha jambo hilo kuwa kasoro, amesema ni kwa sababu tamanio la msimamizi wa uchaguzi lilikuwa kila aliyejiandikisha apige kura.
Kasoro nyingine, amesema ni wananchi kupata shida kuona majina yao ya kuthibitisha uhalali wao wa kupiga kura.
Hata hivyo, amesisitiza ni muhimu wakati ujao mamlaka ijipange kuweka orodha hiyo kiteknolojia kurahisishia wananchi.
Kuhusu wapinzani walioenguliwa, amesema CCM kupitia katibu mkuu wake (Dk Emmanuel Nchimbi) ilikwenda hadharani ikisema matatizo madogo madogo yasizingatiwe.
“Sisi kama wachezaji tulisikia malalamiko ya wenzetu, tukatoka hadharani kusema jamani hata haya matatizo madogo waachiwe tukashindane uwanjani, yapo maeneo ushauri wetu umesikilizwa wamerudishwa na bado tumewapiga,” amesema.
Hata hivyo, hoja hiyo iliibua ubishaji kutoka kwa washiriki wa mjadala wakihoji CCM ina mamlaka gani ya kuagiza makosa madogo yapuuzwe.
Profesa Mkumbo ameijibu hoja hiyo akisema uamuzi wa chama hicho tawala kutoa maoni kuhusu mapungufu madogo madogo yasizingatiwe, haimaanishi chama hicho kimeagiza.
Hata hivyo, amesema ili kuthibitisha hilo si agizo, katika maeneo mengi kilichoshauriwa na Dk Nchimbi hakikufuatwa, wasimamizi walisimamia sheria.
Hoja ya utumishi wa umma wa Profesa Mkumbo, alifafanuliwa pia na Madeleka aliyesema ibara mbalimbali za Katiba ya CCM zinazompa mbunge nafasi za kisiasa ndani ya chama hicho na hivyo si mtumishi wa umma.
Hata hivyo, amesema malalamiko juu ya uchaguzi huo usisimamiwe na Tamisemi yanatokana na ukweli kwamba wizara hiyo ipo chini ya Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM.
Katika mazingira hayo, amesema haiwezekani mchezaji awe mwamuzi na atoe nafasi ya ushindi kwa mpinzani ilhali naye ni mshindani.
Kwa sababu ya yote hayo, amesema ipo nafasi ya kurudiwa upya kwa uchaguzi huo iwapo utapingwa kwa mujibu wa sheria.
Amesema kisheria ni uchaguzi unaosimamiwa na INEC pekee ndiyo usiotakiwa kupingwa, lakini wa serikali za mitaa unaweza kuhojiwa mahakamani.
“Uchaguzi ni mali ya wananchi na ndiyo wanaolipa kodi na ikifika mahala wakaona umeendeshwa kinyume na matarajio yao si jambo la ajabu kurudia uchaguzi,” amesema.
Amesisitiza hakuna sheria inayosimamia uchaguzi wa serikali za mitaa, inayozuia uchaguzi huo kurudiwa.
Kwa upande wa Mchinjita, amedai CCM inashindikana kuondolewa madarakani kwa sababu ya matumizi ya dola na kuwageuza watumishi wa umma kuwa machawa wake.
Kutumika kwa vyombo hivyo kuiweka CCM madarakani, amesema kunaondoa nguvu ya vyombo husika, lakini muda mchache ujao hilo litakoma.
Amesema yaliyotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, yatafanana na yatakayofanywa katika uchaguzi mkuu wa mwakani.
Amesema haoni dalili ya kuwepo kwa uchaguzi huru na haki katika mazingira ya sasa, akisisitiza kunahitajika mabadiliko ya mifumo ya kisheria ikiwemo Katiba.
Kwa sababu ya uhalisia huo, amesema wamefanya juhudi mbalimbali ikiwemo maridhiano, mahakamani na sasa wanataka kukutana kama wapinzani na wadau wengine kupata suluhu.
“Tunapaswa kuwa na suluhisho litakalowezesha kuondoa changamoto zinazojitokeza,” amesema.