MCHEZO wa raundi ya 11 wa Ligi ya Championship kati ya Mbeya City na Biashara United uliopangwa kuchezwa leo saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, umeahirishwa hadi Jumanne, huku sababu zikitajwa kuwa ni ukata.
Taarifa iliyotolewa na Mbeya City ilieleza mchezo huo utachezwa siku ya Jumanne badala ya leo kama ulivyopangwa awali.
Mwanaspoti lilimtafuta Ofisa Habari wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota ambaye alieleza wao walijipanga kwa ajili ya mchezo huo, japo walipokea mabadiliko hayo, huku akikataa kuweka wazi sababu za kuahirishwa kwa mechi hiyo ambayo wao ndio wenyeji.
Kaimu Mwenyekiti wa Biashara United, Augustine Mgendi alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia mabadiliko hayo alisema, hadi sasa hajapokea ujumbe wowote kwa njia ya baruapepe, hivyo asingependa kulizungumzia hilo.
Hata hivyo, wakati viongozi wa timu hizo wakishindwa kuweka wazi sababu chanzo cha ndani kimesema, viongozi wa timu mojawapo waliomba kuahirishiwa mchezo huo kutokana na ukosefu wa fedha.
“Waliomba mchezo huo upelekwe mbele ili wapate nafasi ya kujiandaa kwani walikuwa hawana fedha, sisi tuliona tufanye hivyo, kwa maslahi mapana ya mpira wetu kwa sababu ni changamoto ya timu nyingi,” kilisema chanzo hicho.
Katika michezo 10 ambayo Mbeya City imecheza imeshinda mitano, sare minne na kupoteza mmoja tu ikiwa nafasi ya sita na pointi 19, wakati Biashara imeshinda miwili, sare minne na kupoteza minne na inashika nafasi ya 11 kwa pointi zake 10.