Ukatili, unyanyasaji ulivyotikisa vikao vya Bunge

Dodoma.  Ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ni miongoni mwa hoja zilizozungumzwa zaidi na kutikisa vikao kadhaa vya Bunge mwaka 2024.

Pamoja na mambo mengi yanayoangukia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, hoja ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ilizungumzwa na wabunge wengi katika bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25.

Mbali na kwenye bajeti ya wizara hiyo, hoja hiyo iliibuka hata wakati wa mikutano yote minne ya Bunge kwa mwaka huo, wabunge wakilalamikia kukithiri kwa vitendo hivyo.

Kutokana na hoja hizo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima alisema wamekuja na mkakati wa kuhakikisha wote wanabeba ajenda hiyo kwa kuizungumzia kila mahali.

Katika mjadala wa bajeti hiyo, baadhi ya wabunge walitaka sheria kutungwa ama kufanyiwa maboresho ili kuweka adhabu kali ikiwamo kuwahasi wanaopatikana na hatia ya kulawiti au kubaka watoto.

Miongoni mwao ni mbunge wa viti maalumu (CCM), Mwantumu Dau Haji aliyetaka wahusika wahasiwe, hoja iliyoungwa mkono na mbunge wa viti maalumu, (CCM), Shally Raymond.

Mei 31, 2024, mbunge wa viti maalumu (CCM), Najma Giga alihoji kwa nini Serikali isiweke kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa kila mwaka kwa kipaumbele cha kudhibiti vitendo vya udhalilishaji wa watoto nchini.

Swali hilo lilijibiwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis aliyesema Serikali imejumusha masuala yote ya ukatili na udhalilishaji wa watoto katika Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (Mtakuwwa) na Sh30 bilioni zimetengwa kwa awamu ya kwanza.

Aprili 18, 2024, mbunge wa viti maalumu, Tunza Malapo alimuuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa maswali ya papo kwa hapo akitaka kujua lini Serikali itaongeza adhabu kwa wakosaji.

Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema inawezekana matukio hayo yanajirudia kutokana na baadhi ya maeneo ya sheria siyo makali.

Alisema Serikali itaendelea kufanya mapitio ya sheria na kanuni zinazohusiana na adhabu dhidi ya makosa ya unyanyasaji wa kijinsia na pale kutakapohitaji mabadiliko ya sheria na kanuni watapeleka bungeni kwa ajili ya kufanya marekebisho zaidi.

Juni 11,2024 suala hilo la ukatili liliibuka tena bungeni, mbunge wa viti maalumu (CCM), Tamima haji Abbas alihoji ni lini Serikali itatunga sheria mahususi kwa makosa ya ukatili wa kijinsia.

Akijibu swali hilo aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini alisema tathimini inafanyika kubaini iwapo kuna haja ya kuwa na sheria mahususi ya ukatili wa kijinsia au kuziboresha sheria zilizopo nchini.

Katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 inaonyesha katika kipindi cha miaka mitano matukio hayo yameongezeka kwa asilimia 80 huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiwa kinara.

Katika ripoti hiyo ya ufanisi katika usimamizi wa hatua za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini, inaonyesha kuwa mwaka 2022 Dar es Salaam yaliripotiwa matukio 1,656 kutoka matukio 326 ya mwaka 2018.

Mbali na CAG, ripoti ya uhalifu na usalama wa barabarani ya mwaka 2023 iliyotolewa na Jeshi la Polisi na kuchapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaonyesha kuongezeka kwa matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watu wazima na watoto nchini.

Kwa kipindi cha kati ya Januari hadi Desemba mwaka 2023, inaonyesha watu walioathirika na matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia walikuwa ni 22,147 huku wanawake wakiwa ni 13,322 na wanaume 825.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa ni kubwa zaidi ukilinganishwa na waathirika 18,403 walioripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la watu 3,744 sawa na asilimia 20.3.

Wadau wataja mbinu za kukomesha

Meneja wa shirika linalojishughulisha na maendeleo ya watoto na familia la  ICS Africa, Kudely Sokoine anasema matukio yote ya ukatili yanafanywa kwenye ngazi ya jamii.

Anasema kutokana na hali hiyo jamii inatakiwa kuamka na kusema hapana dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, hivyo hatua zitaanza kuchukuliwa kutoka katika ngazi ya jamii hadi kwenye mamlaka nyingine.

“Pia, vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuhakikisha mfumo uliowekwa unafanya kazi ili wale waliofanya vitendo hivyo waweze kuchukuliwa hatua. Jamii inaweza kufanya kazi yake lakini inapofikia kwenye ngazi ya kuchukua hatua kunakuwa na kulegalega sana,”anasema.

“Sasa hiyo mwisho wa siku jamii inaona kama hatua stahiki hazichukuliwi, wanakata tamaa ya kutoa ushirikiano kwenye matukio,” anasema Sokoine.

Anasema kama mfumo ukifanya kazi vizuri kwa wanaofanya matukio hayo kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria na kwa wakati itafanya hata wale wanaofikiria kufanya vitendo waache.

Aidha, Sokoine ambaye pia mratibu wa shirika hilo nchini anasema Serikali pamoja na wadau wanatakiwa kuhakikisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yanafanywa kuwa masuala mtambuka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Msichana Initiative, Rebeca Gyumi anasema yapo maeneo ya uwajibikaji yanayopaswa kuangaliwa ili kuleta matokeo makubwa zaidi katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Analitaja eneo hilo ni utekelezaji wa sheria kwa kuhakikisha sheria ambazo zina mwanya zinarekebishwa na kuhakikisha sheria zilizopo zinatekelezwa kwa usahihi na kwa haraka.

Anasema miongoni mwa changamoto inayoripotiwa zaidi kwenye jamii ni uwepo wa sheria lakini hazitekelezwi vizuri kwa hukumu za Mahakama kutopatikana kwa wakati au sheria kupindishwa.

Aidha, anasema ni wakati sasa wa kuangalia upya Sheria ya Ndoa itakavyoweza kuweka uwanja mpana wa kuwalinda watoto wa kike na wakiume dhidi ya ndoa za utotoni.

Pia, anasema ni vyema kukatunga sheria maalumu ya masuala ya ukatili wa kijinsia itakayolenga kushughulikia masuala hayo haraka.

Anasema katika mapambano hayo suala la utashi wa kisiasa ni muhimu kwa viongozi walioshika nafasi za juu.

Rebeca anasema eneo jingine la uwajibikaji linalopaswa kuangaliwa ni raslimali zinazotengwa kwa ajili ya kutatua changamoto zinazotokana na ukatili lakini na kusaidia afua ambazo zinalenga kuzuia ukatili.

 Mwazilishi wa Jukwaa la Tanzania Boys & Mens Ambassadors (TBMA), Dk Katanta Simwanza anasema bajeti inayotengwa kwa ajili ya kupambana na masuala ya ukatili wa kijinsia haitoshelezi.

Anasema Mpango Mkakati wa Kuzuia Ukatili wa Kijinsia wa awamu ya kwanza ulioisha, ulikuwa na vitu vingi ambavyo havikuweza kufanikiwa kwa sababu ya ukosefu wa raslimali za kutekeleza.

Anasema mpango huo ulishindwa kutekelezwa kwa sababu hakukuwa na chanzo mahususi cha fedha kwa ajili ya kuutekeleza.

“Tunategemea katika mpango awamu ya pili tuone wadau, wanajamii, taasisi za Serikali na zisizo za Serikali na sekta binafsi, wote kwa umoja wetu tunakaa chini na tutengeneze mfuko…Tunatarajia tuwe na mfumo ambao unazuia ushangiliaji,”anasema.

Kuhusu kukomesha ukatili wa kijinsia, Dk Simwanza anasema jambo la kwanza ni kuwekeza katika ngazi ya familia ili iweze kutambua na kuonea kinyaa ukatili wa kijinsia kuanzia ngazi hiyo.

“Kwa jinsi ninavyotazama ukatili wa kijinsia ni kama kinyesi, tena kinyesi kinachonuka, sasa bahati mbaya familia nyingi zimeamua kukikumbatia hicho kinyesi,” anasema.

“Ukiniambia nielezee ukatili wa kijinsia nini kwa maana nyingine, nitakueleza kuwa ni aina ya dhambi ambayo familia na jamii imehalalalisha ama imeamua kuinyamazia kimya,”anasema Dk Simwanza.

Pia, anasema ili kukomesha ukatili wa kijinsia ni kuwekeza katika kuhakikisha watendaji wa masuala ya ukatili wa kijinsia wanawajibishwa na kuwekeza katika mifumo itakayowapa mamlaka watu wanaoshudia kuwajibika.

“Shida ni kwamba kuna gap (mwanya), tunahangaika zaidi na watu wanaofanyiwa ukatili lakini wanaofanya na wanaoushuhudia hakuna tunalolifanya, utasikia tu ni maisha yao watajijua wenyewe,” anasema Dk Simwanza.

Anasema jambo jingine la kufanyika ni kuweka kipaumbele katika mifumo ya kutoa taarifa kwa kuhakikisha inakuwa rafiki, inausiri, inaonyesha heshima na inafanya mtoa taarifa kuwa salama pindi anapotoa taarifa.

Dk Simwanza anasema eneo jingine la kuwekeza ni kuwashirikisha wanaume kwa kuwaonyesha wanamchango katika kuzuia ukatili wa kijinsia badala ya wakati wote kuwanyoshea kidole kuwa ni wabaya.

Related Posts