Ukimleta ndugu yako mjini mwambie haya

Mwaka unaisha, kwa sisi waswahili hiki ndio kipindi cha kuchukua ndugu zetu, watoto wa dada zetu, wa shangazi na wa wajomba zetu kutoka vijijini kuwaleta mjini kuwafundisha maisha ili wajijenge kama sisi ambavyo tuliletwa mjini tukajijenga.

Kushikana mikono ni utamaduni mzuri sana, lakini kama kawaida ya mtu anapokwenda kwenye mazingira mapya, lazima apate maelekezo ya jinsi ya kuishi. Haya ni maelekezo machache ya kumpa ndugu yako pindi tu anapofika mjini.

Akipewa cha bure, ajue yeye ndiye anayeliwa

Mwambie mjini hakuna cha bure, akiona anakwenda sehemu anapewa vitu vizuri bure au kwa gharama rahisi asijione anafaidi, ila akae akijua kuwa yeye ndiye wanayemfaidi.

Mwambie akipita Kariakoo, akaona watu wanauza simu ya milioni tatu kwa laki moja na nusu asithubutu kusimama. Tena ikiwezekana asiitikie hata salamu zao, apite mbali na asigeuke hata wakimuita kwa spika na matarumbeta na ving’ora.

Mwambie kuna msemo wazungu wanasema; “If you’re not paying for the product, you are the product.” Yaani, kama unapewa huduma au bidhaa bila malipo, basi kaa ukijua wewe ndiyo hiyo huduma au bidhaa.

Mwambie amekuja mjini kutafuta maisha, sio kufuatilia mambo ya watu. Mwambie hapa mjini atakuta familia ya baba, mama na watoto watatu wanalala chumba kimoja. Itamshangaza, lakini mwambie aachane nayo, sio kilichomleta mjini, hakimhusu.

Mwambie sio hayo tu, hapa mjini ataona vioja vingi, matukio mengi, mikasa ya kila aina. Atasikia stori za wababa wanaolea watoto wa wenzao wakidhani wao, atasikia habari za kila aina. Yatamshangaza, lakini mwambie aachane nayo, hayo sio yaliyomleta mjini, hayamuhusu. Akijikuta anapenda sana kufuatilia maisha ya watu hapa mjini, atapoteza umakini kwenye mambo yake na mwisho wa siku anaweza akajikuta yeye ndiye anakuwa kituko kingine cha wageni wengine kushangaa.

Mjini hakuna mwanamke single

Mwambie akija mjini atakutana na wanawake wazuri sana, lakini mueleze kwamba hao wote wana wenyewe. Mjini hakuna mwanamke asiyekuwa na mtu, na hata anayeonekana hana mtu, anaye ila haeleweki.

Kwa hiyo kama anaingia kwenye mapenzi mwambie akae akijua anaingia kwenye ligi, kwenye vita, kwenye mashindano. Tena mashindano ambayo ili kushinda atalazimika kutumia muda, nguvu, na pesa.

Ikiwezekana mwambie akija mjini asikimbilie kupendapenda mabinti wa watu. Mwambie atafute maisha kwanza, mwambie afanye kilichomleta, ajijenge, kwa sababu kama tulivyosema mwanzo, mjini hakuna cha bure, hata salamu inalipiwa. Kwa hiyo hata kupenda mabinti za watu pia panalipiwa.

Upendo ni biashara kubwa sana hapa mjini.

Mwisho kabisa, mwambie afahamu kuwa maisha ya mjini hayana muda wa huruma. Yeye ndiye anayehusika na maisha yake.

Akikosea kuchagua marafiki, akaangukia kwenye vishawishi vya haraka haraka, au akaamua kufuata mambo ya watu badala ya maisha yake, atajikuta anarudi kijijini mikono mitupu.

Mjini ni mahali pa fursa, lakini pia ni mahali pa changamoto. Kuishi kwa tahadhari ndiyo siri ya kufanikiwa.

Related Posts