Ummy Mwalimu ataja siri ushindi wa Dk Ndugulile WHO

Dar es Salaam. Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu amezungumzia ushindi wa aliyekuwa mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika na mbunge wa Kigamboni, marehemu Dk Faustine Ndugulile kuwa ulikuwa mgumu hasa katika mchakato wa kuomba kura.

Ummy aliyewahi kuwa Waziri wa Afya amesema hayo leo Jumapili, Desemba mosi, 2024 alipofika Kigamboni, kuhani msiba nyumbani kwa Dk Ndugulile aliyefariki dunia Novemba 27, 2024 nchini India.

Amesema akiwa Waziri wa Afya, huku Dk Ndugulile akiwa naibu waziri wake, alimfuata na kumueleza kusudio lake la kugombea nafasi hiyo, baada ya hapo walifanya mazungumzo na Wizara ya Mambo ya Nje na kuandika barua rasmi kwenda kwa Rais Samia Suluhu Hassan kumueleza dhamira hiyo.

“Tulimuandikia barua aridhie Dk Ndugulile agombee nafasi hiyo, aliridhia na tulifanya kazi kubwa, lakini siri ya ushindi ule kwa asilimia kubwa ni Dk Ndugulile mwenyewe,” amesema.

Amesema Dk Ndugulile alipambana kusoma, kutokana na ugumu wake alianza kujifunza hadi lugha ya kifaransa na kuna wakati walikuwa wanakaa kuomba kura kwa mawaziri wanaozungumza kifaransa na ilikuwa inawapa shida namna ya kuwajibu.

“Tulikuwa tunatuma ujumbe, mawaziri wanatujibu kwa lugha ya kifaransa, nikimwambia Dk Ndugulile ananipa moyo subiri, ananirushia ujumbe nami nilikuwa nafowadi hivyo hivyo, alihangaika kiasi cha kutafuta nchi zenye watumishi wachache WHO,” amesema.

Amesema kutokana na ugumu wa kuomba kura ya nafasi hiyo, ilifikia hatua walikuwa wanaahidi kutoa nafasi za kazi kwa baadhi ya nchi.

“Tukiwa Nigeria na kwa sababu lilikuwa eneo gumu na kwa kutambua makao makuu ya WHO yako Brazaville, tuliahidi kuweka ofisi za makao madogo Nigeria, lakini tumepata kura na kushinda ilikuwa nafasi kubwa na ingeleta heshima.

“Dk Ndugulile mwenyewe aliniahidi kunipa kazi kama ingetokea nataka kuacha siasa, angenipa mwakilishi maalumu wa mkurugenzi wa kanda ya Afrika- Tanzania, lakini nimepoteza,” amesema Ummy.

Amesema Dk Ndugulile ameacha ujumbe kwa wataalamu wa kitanzania kuacha kuogopa kuwania nafasi za kimataifa, kwani ni jambo linalowezekana.

Agosti 27, 2024, Dk Ndugulile alishinda nafasi hiyo, katika kinyang’anyiro ambacho wagombea wengine walikuwa pamoja na Dk Boureima Hama Sambo (Niger) Dk N’da Konan Michel Yao (Cote d’Ivoire) Dk Ibrahima Soc’e Fall (Senegal) na Dk Richard Mihigo (Rwanda).

Dk Ndugulile alishinda baada ya nchi 19 kuipigia kura Tanzania katika mzunguko wa kwanza, 12 wakiipigia Senegal, saba (Niger) na nchi saba zikiipigia Rwanda.

Mzunguko wa pili wa kuondoa mgombea mmoja, mgombea kutoka Niger alipigiwa kura 22 za kuondolewa, Rwanda kura 20 na Absteein alipigiwa kura 3.

Katika matokeo ya jumla ya mzunguko wa pili, Dk Ndugulile alipata kura 25, Senegal 14 na Niger kura sita.

Ummy amesema kuwa Dk Ndugulile alikuwa kiongozi mwerevu na aliyependa kuona matokeo.

“Nimefahamiana na Dk Ndugulile mwaka 2010 akiwa mbunge wa Kigamboni, mimi nikiwa mbunge wa viti maalumu mkoa wa Tanga, tulikuwa tunawasiliana kwa karibu zaidi, lakini mwaka 2015 ukaribu uliongezeka baada ya kuteuliwa kwangu kuwa Waziri wa Afya, naye akiwa mshauri wangu mkubwa.

“Mungu kama alisikia dua zangu mwaka 2017 Dk Ndugulile aliteuliwa kuwa naibu waziri wangu, nilishukuru Mungu, kwani alikuwa mshauri wangu, tulifanya kazi wizarani kwa upendo na wema,” amesema na kuongeza;

“Watumishi wa serikali tunajuana hapa, lakini Dk Ndugulile alikuwa ananishauri mambo ya kuzingatia na nasimama bila uoga kusema kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 tulifanya vizuri na mafanikio makubwa yalionekana.”

Amesema licha ya kwamba katika mafanikio hayo walipitia misukosuko, ikiwemo tishio la ugonjwa wa Ebola lakini hawakulala na walipambana hadi wakavuka.

Ummy amesema hata baada ya kuondoka serikalini waliendelea kushirikiana, Dk Ndugulile alipoteuliwa kuwa Waziri wa Teknolojia na Mawasiliano aliwasaidia kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa mfumo wa tehama.

Naibu waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi na Mbunge wa Mikumi, Dennis Londo amesema Dk Ndugulile alikuwa kielelezo cha uongozi kwa kizazi cha sasa, hasa katika eneo la uadilifu, huku akigusia aliwahi kumueleza mapito ya kisiasa aliyopitia.

“Alinifundisha kuna wakati unatakiwa kusimama, ameondoka katika kipindi ambacho tulikuwa tunamuhitaji zaidi,” amesema.

Amesema moja ya jambo ambalo kwake hakutaka kuliacha ni kupenda kujifunza na kusoma mara kwa mara, huku akieleza alikuwa mahiri katika kujenga hoja.

“Hata katika kugombea nafasi hii mpya WHO, tulishirikiana naye kwa ukamilifu na alikuwa miongoni mwa wabunge waliolitumia Bunge kama njia ya kutafuta fursa nje ya nchi,” amesema.

Related Posts