WATANZANIA wawili wanaokipiga Ligi ya Walemavu nchini Uturuki wameanza vibaya ligi hiyo baada ya wote wawili kupoteza mbele ya vigogo wakimaliza dakika 90.
Nyota hao ni Ramadhan Chomelo anayekipiga Konya Amputee na Hebron Shedrack wa Sisli Yeditepe ambao wako nchini humo kwa msimu wa tatu mfululizo sasa.
Msimu mpya wa ligi hiyo ulianza Novemba 24, timu ya Shedrack ikipoteza mabao 3-1 mbele Sahinbey Belediye SK iliyomaliza nafasi ya pili msimu uliopita.
Kwa Chomelo walipoteza mbele ya bingwa mtetezi Alves Kablo kwa mabao 6-1 ambao hawajawahi kupata ushindi mbele yao tangu msimu uliopita.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Shedrack alisema licha ya kupoteza mchezo wa kwanza, bado wanaamini watafanya vizuri michezo ijayo.
“Tulikutana na timu ngumu ambayo msimu uliopita ilikuwa miongoni mwa timu bora iliyoleta ushindani, tumepoteza mchezo lakini tunaangalia inayokuja tutafanyaje,” alisema Shedrack.
Chomelo alisema walicheza na timu iliyokuwa imewazidi karibu kila eneo na kuanzia mabeki hadi washambuliaji wake walikuwa hatari langoni kwao.
“Wiki hii tunacheza na TSK baada ya kupoteza na bingwa mtetezi na kulikuwa na baridi kali na barafu zilizotanda kwenye uwanja na siku ile hatukucheza kwa hiyo sasa tutafanya maandalizi mazuri isitoshe tuko uwanja wa nyumbani,” alisema Chomelo.