Pemba. Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Shaaban Ali Othman amesema bonanza la michezo na utamaduni la Pemba linachochea utalii wa eneo hilo pamoja na kuimarisha uchumi.
Waziri Othman ameytasema hayo Novemba 30, 2024 akifunga bonanza hilo lililohusisha michezo mbalimbali kama triathlon na duathlon.
“Bonanza hili ni mfano wa dhati wa juhudi zetu za kuendeleza uchumi wa buluu kupitia utalii na michezo. Limeimarisha mshikamano wa kijamii na kuleta mwonekano mpya wa Pemba kwa dunia,” amesema.
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Arif Abbas, amesema mwaka huu bonanza hilo limepiga hatua, likishirikisha washiriki wa kimataifa kutoka Kenya katika michezo ya triathlon, duathlon, na kuogelea.
Abbas amesema kuwa Kamisheni ya Utalii inalenga kuifungua Pemba kupitia utalii wa michezo, utamaduni, na utalii wa halal.
“Lengo letu ni kuitangaza Pemba si tu kwa wageni wa ndani, bali pia katika soko la kimataifa. Michezo kama triathlon na gwaride la punda ni njia za kipekee za kuonyesha urithi wa Pemba,” alisema.
Kwa mwaka huu, tamasha hilo lilihudhuriwa na washiriki mbalimbali ambapo mchezo wa triathlon ulikuwa na washiriki 23, huku wa duathlon ukiwa na washiriki 29 na mashindano ya kuogelea yakihusisha washiriki 56 (wanawake 18, wanaume 38).