Wenye ualbino wataja changamoto tano zinazowakabili, Serikali yajipanga

Dar es Salaam. Wakati watu wenye ualbino wakitaja changamoto tano ‘sugu’ wanazodai kukwamisha utu na ustawi wao, Serikali imesema imekamilisha uandaaji wa mpango kazi wa haki na ustawi wao.

Mpango huo unatarajiwa kuzinduliwa Jumanne ya Desemba 3, 2024 kwenye maadhimisho ya Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani.

Jana Jumamosi, Novemba 30, 2024 yalifanyika matembezi ya hisani maalumu kwa ajili ya kuelimisha jamii kuhusu watu wenye ualbino na kuchangia fedha kusaidia mahitaji yao yaliyoongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu), Ridhiwani Kikwete aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Ualbino Tanzania (TAS), Godson Mollel amesema wana changamoto tano zinazokwamisha utu na ustawi wao hasa uelewa mdogo kwa jamii unaosababisha baadhi ya watu kuwa na imani potofu juu ya watu wenye ualbino hali inayosababisha kuwagharimu maisha au kupata ulemavu.

“Kuna jamii inaamini viungo vyetu vinaweza kuwapa utajiri, hii inatuumiza na kugharimu hadi maisha yetu, vilevile ngozi zetu ni adui wa jua, mionzi yake ikitupiga inatusababishia saratani ya ngozi.

“Mafuta yetu ambayo ndiyo kinga ya ngozi zetu ni gharama kubwa kwa kuwa yapo kwenye kundi la vipodozi na sio la dawa, hivyo wengi hushindwa kumudu gharama,” amesema Mollel katika matembezi hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Lions Club ya Dar es Salaam

Amesema changamoto nyingine ni uhaba wa kliniki za saratani ya ngozi nchini, hivyo kusababisha wengi wao kushindwa kufanya uchunguzi na wengi hufariki dunia kwa kukosa matibabu kwa wakati.

“Pia, kuna mitazamo hasi kwa waajiri wengi kwa kundi hili, wengi wanapoomba kazi uonekana kama mzigo, hata kama wana sifa hukosa na uhaba vifaa saidizi kwani watu wenye ualbino wana uoni hafifu, kwa wanafunzi ni changamoto,” amesema Mollel.

Kwa upande wake, Waziri Ridhiwani amesema ili kushughulikia changamoto za kundi hilo, Serikali imekamilisha uandaaji wa mpango kazi wa haki na ustawi kwa albino utakaozinduliwa Jumanne ya Desemba 3, 2024 kwenye maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu duniani.

“Serikali ipo pamoja na wenzetu hawa katika kila hatua, imezisikia changamoto zao na itazifanyia kazi,” amesema Ridhiwani akiwahamasisha pia kuzigeuza changamoto kuwa fursa huku akisisitiza.

“Serikali inafahamu uhitaji wa mafuta ni jambo muhimu kwani ni kinga ya ngozi za wenye ualbino, yakizuia madhara ya mionzi jua, hivyo bei na gharama za uingizwaji zinapaswa kushughulikiwa na hata mahitaji mengine ya kibinadamu,” amesema.

“Kuhusu hospitali za saratani ya ngozi, zipo ambazo zinafanya kazi, kwa Dar es Salaam, Kilimanjaro, Morogoro, Lindi, Mara na hospitali teule ya Muheza ambazo zinatoa huduma hiyo, hata hivyo wizara itashiriki kutoa elimu ili wananchi wote wawe na mtazamo chanya kuhusu wenzetu wenye ualbino,” amesema.

Gavana wa Lions Club Tanzania, Habil Khanbhai amesema hiyo ni mara ya kwanza kwa taasisi hiyo kusaidia watu wenye ualbino na wanatarajia kuendelea kushirikiana nao na kuwasapoti.

Katika matembezi hayo ya kilomita tano kuanzia Hospitali ya Ocean Road, Sh13 milioni zilikusanywa ili kusaidia mahitaji mbalimbali ya kibinadamu kwa kundi hilo.

Related Posts