Yanga!… Haya ni maajabu | Mwanaspoti

JANA saa 12:30 jioni Yanga ilikuwa pale Ruangwa mkoani Lindi kucheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo. Timu hizo zilikutana zote zikiwa hazina matokeo ya kuridhisha.

Wenyeji Namungo kabla ya mchezo wa jana, ilikuwa imetoka kupoteza mechi sita mfululizo za ligi wakati Yanga ikipoteza mbili za mwisho.

Wakati zote zikiwa kwenye hali mbaya, mabingwa watetezi, Yanga msimu huu imeonyesha maajabu katika eneo la ulinzi licha ya kwamba haina matokeo mazuri sana kwa ujumla.

Maajabu hayo ni ya kuruhusu mabao machache zaidi kulinganisha na msimu uliopita katika mechi 10 za kwanza.

Wakati ikiruhusu mabao machache, pia timu hiyo imefunga mabao machache sana kulinganisha na msimu uliopita. Hiyo inatoa picha kwamba makali ya safu ya ushambuliaji yamepungua.

Takwimu za Yanga msimu huu katika mabao ya kufunga, timu hiyo inayo 14 katika mechi 10 za kwanza kabla ya jana, huku pia ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne.

Msimu uliopita katika mechi 10 za kwanza, timu hiyo ilifunga mabao 30 na kuruhusu matano.

Kwa ujumla ndani ya misimu mitano kuanzia 2020-21 hadi sasa, timu hiyo imekuwa na wastani mzuri wa kufunga mabao ambayo yamekuwa yakipanda kila msimu ukiondoa msimu huu, lakini hata kwenye kuzuia haipo vibaya sana.

Yanga ambayo imetawala ligi kwa kipindi cha misimu mitatu mfululizo 2021-22, 2022-23 na 2023-24 ambapo imebeba ubingwa, msimu huu takwimu za mabao ya kufunga zinawarudisha nyuma hadi 2020-21 ambapo Simba ilibeba ubingwa wa ligi hiyo kwa mara ya mwisho.

Ukiachana na takwimu za Yanga katika mechi kumi za ligi msimu huu na msimu uliopita, timu hiyo wakati inapambana kuuondosha utawala wa Simba msimu wa 2020-21, mechi kumi za kwanza angalau safu yake ya ulinzi ilianza vizuri kidogo kutokana na kuruhusu mabao matatu pekee lakini pia ikifunga mabao machache ambayo ni 12.

Katika mechi hizo kumi, ilishinda saba na sare tatu, haikupoteza huku ikikusanya pointi 24.

Msimu wa 2021-22 ambao ilibeba ubingwa baada ya kuukosa kwa misimu minne mfululizo, mechi kumi za kwanza ilifunga mabao 16 zaidi ya mawili ya msimu huu na kuruhusu manne sawa na ya msimu huu.

Lakini pia ilikusanya pointi 26 zilizotokana na kushinda mechi nane na sare mbili, haikupoteza.

Katika kuutetea ubingwa wao huo msimu wa 2022-23, Yanga mechi kumi za kwanza ilifunga mabao 19 na kuruhusu sita, ikishinda mechi nane na sare mbili, haikupoteza ikiwa imekusanya pointi 26. Utaona hapa mabao ya kufunga yameongezeka manne kutoka msimu wa nyuma, pia pointi zimeongezeka mbili, huku pia ikiruhusu mabao mawili zaidi.

Msimu uliopita 2023-24, ndiyo ulikuwa bora zaidi kwao kuanzia ishu ya kufunga mabao hadi kukusanya pointi kwani ilianza na mkwara mzito wa kupata ushindi wa 5-0 mechi mbili mfululizo.

Katika mechi kumi za kwanza, Yanga ilifunga mabao 30 ikiwa ni kiwango kikubwa cha mabao katika misimu mitano iliyopita huku yenyewe ikiruhusu mabao matano pekee.

Msimu huo ilishinda mechi tisa na kupoteza moja, haikuwa na sare ambapo ilikusanya pointi 27 ambazo ni nyingi pia kulinganisha na misimu ya nyuma yake.

Kinachoitesa Yanga hivi sasa kinatajwa kuwa ni uchovu wa wachezaji kwani asilimia kubwa ya wanaounda kikosi cha kwanza walifanya kazi kubwa msimu uliopita katika kutetea makombe yao ambao ni Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, pia kuifikisha timu hadi robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza kutokana na kufuzu makundi msimu huo baada ya kupita takribani miaka 25.

Related Posts