Bondia aliyefariki Zanzibar kwa kupigwa TKO, azikwa Dar

Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Abassi Mselem, ambaye Novemba 30, 2024 alipigwa ulingoni na kupoteza fahamu kisha kufariki Desemba 1, 2024, amezikwa leo jijini Dar es Salaam.

Mselemu amezikwa kwenye makaburi ya Saku yaliyopo Mbagala jijini Dar es salaam baada ya mwili wake kuwasili leo asubuhi ukitokea Zanzibar.

Mweka Hazina wa Chama cha Makocha wa Ngumi Taifa, Maneno Abdallah, amesema marehemu Mselemu alicheza pambano la utangulizi la raundi 6 dhidi ya bondia Bakari Bakari ambapo ilipofika raundi ya mwisho alianguka na mwamuzi kumaliza pambano.

Abdallah amesema baada ya bondia huyo kuanguka, aliwahishwa Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Unguja kutokana na afay yake kutokuwa sawa ambapo umauti ulimkuta akiwa anasubiri kufanyiwa upasuaji.

“Alipofikishwa hospitali alitakiwa kufanyiwa upasuaji lakini daktari akasema aachwe kwanza kutokana na hali yake kuwa mbaya zaidi, wakati akisubiriwa akae sawa ndipo akafariki,” amesema Abdallah.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Zanzibar, Novemba 30, 2024 bondia Mselemu alipanda ulingoni kwenye mapambano ya ‘Usiku Wa Left Hook Ya Baba Mwinyi’ yaliyoandaliwa na Machatu Boxing Promotion na kufanyika Ukumbi wa Zanzibar Golf Club.

Related Posts