BoT yazungumzia uimara wa sekta ya benki

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema sekta ya fedha iko imara na inakua, licha ya changamoto za kiuchumi za kimataifa ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha, vita vya Ukraine na Mashariki ya Kati pamoja na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti ya hivi karibuni ya mwaka ya usimamizi wa mabenki ya mwaka 2023 iliyotolewa na BoT, inaonyesha mali za sekta hiyo ziliongezeka kwa asilimia 17.8, kufikia Sh54.4 trilioni kutoka Sh46.2 trilioni mwaka uliopita.

Akizungumzia ukuaji huo, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema ukuaji huo umechangiwa na ongezeko la amana, mikopo na mapato, jambo alilosema limechochewa na kuimarika kwa uaminifu wa watumiaji wa huduma za kibenki kutokana na mazingira mazuri ya kiuchumi.

Ripoti hiyo unaonyesha kuwa amana katika benki ziliongezeka kwa asilimia 16.9, kufikia Sh38.1 trilioni, mikopo ilikua kwa asilimia 22.7 hadi kufikia Sh32 trilioni.

“Mfumo wa benki uko imara kwa kiwango cha faida, mtaji, ukwasi na ubora wa mali. Benki kuu itaendelea kukuza uthabiti wa kifedha kupitia udhibiti madhubuti na usimamizi ili kuhakikisha sekta ya kifedha inabaki salama na imara,” amesema Tutuba.

Hali hiyo imechochea kuimarika kwa ubora wa mali na kiwango cha mikopo chechefu (NPLs) kilipungua hadi asilimia 4.4 kutoka asilimia 5.8 mwaka 2022. Hii ilitokana na maboresho katika usimamizi wa hatari za mikopo pamoja na hatua madhubuti zilizochukuliwa na BoT. Vilevile.

Uwiano wa mali za kioevu (Liquid assets) na madeni ya muda mfupi uliongezeka hadi asilimia 28.8, juu ya kiwango cha chini cha kisheria ambacho kinautaja ukomo kuwa ni asilimia 20.

Ripoti hiyo inaonyesha ongezeko la faida na faida kutokana na mali ilipanda hadi asilimia 4.4 kutoka asilimia 3.5, na faida kutokana na mtaji ikiongezeka hadi asilimia 20.5 kutoka asilimia 14.2 mwaka uliopita.

“Ukuaji huu umechangiwa na ongezeko la mapato ya riba, mapato yasiyotokana na riba na uboreshaji wa ufanisi wa uendeshaji, haya ni matokeo mazuri ya kiuchumi na sera ya fedha ya Benki Kuu inayohamasisha ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi,” amesema Gavana Tutuba.

Mbali na hayo, upanuzi wa sekta ya kibenki pia umeongeza upatikanaji wa huduma zake kupitia mtandao wa matawi, mawakala wa benki na njia za kidijitali.

 Ripoti hii pia inaonyesha idadi ya matawi ya benki iliongezeka hadi kufikia 1,011 mwaka 2023 kutoka 987 mwaka 2022, huku idadi ya mawakala wa benki ikiongezeka kwa asilimia 41.1 kufikia 106,176.

Hali hii imefanya sekta hiyo kuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya uchumi wa Tanzania, ikichangia zaidi ya asilimia 70 ya mali zote za kifedha nchini.

Related Posts