Novemba 23, 2024, Klabu ya Simba ilimtangaza rasmi, Zubeda Hassan Sakuru kuwa kaimu mtendaji mkuu (CEO), hatua ambayo imepokelewa kwa hisia mchanganyiko kutoka kwa wadau wa soka lakini pia na wanachama wa timu hiyo kutokana na matarajio yao.
Zubeda ameteuliwa kushika wadhifa huo akichukua nafasi ya Mnyarwanda, Francois Regis aliyedumu kwa miezi minne tu ndani ya kikosi hicho tangu alipoteuliwa Julai 26, 2024, akirithi mikoba ya mtangulizi wake, Imani Kajula aliyeondoka Agosti 1, 2024.
Wakati mashabiki wa klabu hiyo wakifurahia uteuzi huo, Mwanaspoti linakuletea makala kuhusu Kaimu CEO huyo na changamoto kadhaa zinazomsubiria kwa hamu kuzitatua, au kufanya zaidi ya kile ambacho kiliwahi kufanywa na watangulizi wake nyuma.
Zubeda ni mzoefu ndani ya timu hiyo kwani kabla ya hapo amefanya kazi kama meneja miradi wa kikosi hicho akimsaidia kwa ukaribu, Imani Kajula kuhusu mchakato wa kutengeneza sera na ushauri wa masuala ya kiutendaji jambo litakalomrahisishia kazi.
Kitendo cha kukaa na kufanya kazi kwa ukaribu na Kajula ambaye alikuwa mtendaji mkuu, ni dhahiri Zubeda kuna vitu vingi ambavyo amejifunza kutokana na uzoefu wa mtangulizi wake kitu ambacho kitamsaidia kutimiza vyema majukumu yake kikosini.
Jina la Zubeda sio geni machoni mwa watu wengi kwani licha ya kutambulika kama mwanachama wa muda mrefu wa timu hiyo ila mtakumbuka katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020, alishawahi kushika nafasi ya ubunge wa viti maalum kupitia Chadema.
Kitendo cha kushika nafasi ya ubunge ni dhahiri ana uwezo mkubwa na tayari ametengeneza wigo mpana na watu mbalimbali ambao watamsaidia katika kutimiza majukumu yake vizuri, ikiwemo kuitangaza kibiashara timu hiyo ndani na nje ya nchi.
Zubeda ni mmoja wa wanachama wa muda mrefu wa klabu hiyo na ameongoza idara mbalimbali ndani ya Simba, ikiwemo ya Meneja Miradi na usimamizi wa masuala ya uendeshaji na utawala, uwezo uliomfanya kusimamia masuala ya kifedha na mikakati ya timu.
Kwa kipindi chote ndani ya Simba, amekuwa akihusika moja kwa moja na mipango ya maendeleo ya klabu, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa miradi ya kiuchumi na mikakati ya kuongeza mapato, jambo linalompa fursa ya kuelewa changamoto na jinsi ya kuzitatua.
Zubeda anakuwa ni mtendaji mkuu wa pili wa Simba mwanamke tangu klabu hiyo ilipoanza kuingia rasmi katika mfumo mpya wa uendeshaji kutoka mikononi mwa wanachama hadi uuzaji wa hisa kuanzia Novemba 4, 2018, akitanguliwa na Barbara Gonzalez.
Tangu Novemba 4, 2018, klabu hiyo imepitia mikoni mwa watendaji wakuu mbalimbali akianza Crescentius Magori, akafuatia Senzo Mbatha aliyekaa kuanzia Septemba 7, 2019 hadi Agosti 9, 2020, kisha nafasi yake kuchukuliwa na Barbara Gonzalez.
Barbara alishika wadhifa huo Septemba 2, 2020 na kuandika rekodi ya mwanamke wa kwanza nchini kuwa mtendaji wa kwanza katika soka la Tanzania ambapo alifanya mambo makubwa ndani ya klabu hiyo hadi alipotangaza kujiuzulu Desemba 10, 2022.
Baada ya kuondoka kwake ndipo Imani Kajula akashika wadhifa huo kuanzia Januari 26, 2023 hadi Agosti Mosi, 2024 akiipa timu hiyo Ngao ya Jamii 2023 na Kombe la Muungano 2024, kisha nafasi yake kuchukuliwa na Regis aliyedumu miezi minne tu.
Licha ya uzoefu wake ndani ya timu hiyo, ila Zubeda anakabiliwa na changamoto nyingi za kuhakikisha anafuata nyayo au kuzivuka za Barbara Gonzalez na kuweka historia ambayo itabaki katika mioyo ya mashabiki wa kikosi hicho cha Msimbazi.
Katika utawala wa Barbara, Simba ilishinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ikacheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2020-2021, tena ikiongoza kundi ‘A’ lililokuwa na vigogo Al Ahly (Misri), AS Vita Club (DR Congo) na Al Merrikh ya Sudan.
Ukiachana na hilo, Simba ikashinda pia Kombe la FA kwa kuifunga Yanga bao 1-0, ingawa msimu wa 2021-2022 aliuanza vibaya kwa kupoteza taji la Ngao ya Jamii mbele ya watani zao Yanga japo hadi anaondoka mwaka 2022, amejiwekea historia kubwa.
Zubeda ana changamoto nyingi, hasa kwa kuzingatia matarajio ya mashabiki wa Simba ambao wana njaa ya mafanikio makubwa kuanzia kutetea taji la Ligi Kuu Bara lililokuwa mikononi mwa watani zao wa jadi Yanga kwa misimu hii mitatu mfululizo.
Pia, ana kazi ya kuhakikisha timu hiyo inafikia hatua ya nusu fainali ya michuano ya kimataifa ambapo kilio kikubwa ni kuifikisha huko kutokana na mara kadhaa kuishia robo fainali, jambo ambalo mashabiki wanaona kwa sasa linatosha kwao.
Katika utawala wa Barbara kitu kikubwa alichofanikiwa ni pamoja na kuinua hadhi na uchumi wa Simba kwa kusimamia kampeni mbalimbali za kuimarisha klabu kifedha na kuvutia wadhamini wengi ambao hadi leo wamekuwa chachu ya wao kufanya vizuri.
Zubeda anapaswa kutembelea upepo huo ambao utamsaidia katika majukumu yake huku akipambana pia kuhakikisha klabu hiyo inazidi kuimarika na kuwekeza katika miundombinu, ikiwemo Uwanja wa Mo Simba Arena ambao wanautumia kwenye mazoezi yao.
Pia ana jukumu la kuhakikisha anatengeneza mahusiano mazuri kati ya klabu na mashabiki ambao ndio itakuwa nguzo muhimu ya kikosi hicho kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ya ndani na nje hivyo, itamsaidia kuzidi kujijengea jina lake.