COASTAL UNION imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons na kuifanya timu hiyo kusogea hadi nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Mchezo huo ulipigwa leo Jumatatu saa 7 mchana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, baada ya kushindwa kufanyika juzi kutokana na mvua kubwa iliyonyesha.
Coastal ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 41 kupitia kwa Hernest Malonga aliyefunga kwa mkwaju wa penati baada ya kiungo Abdallah Hassan kufanyiwa faulo ndani ya boksi.
Bao hilo lilodumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika na kumfanya Malonga kufikisha mabao matatu kwenye ligi akiwa kinara wa ufungaji kwa Coastal.
Hata hivyo, kipindi cha pili Tanzania Prisons ikarudisha bao na kufanya ubao usome 1-1 kupitia Meshack Mwamita aliyeukwamisha mpira nyavuni kwa kichwa dakika ya 56 akimalizia krosi ya Kelvin Sengati kabla ya Maulid Juma wa Coastal kufunga bao la pili na kuipa timu yake pointi tatu.
Matokeo hayo yanaifanya Coastal Union kufikisha pointi 16 ikitoka nafasi ya 11 hadi ya tisa ukiwa ushindi wa nne msimu huu ndani ya ligi hiyo, ikiwa na sare nne huku ikipoteza michezo mitano.
Kwa upande wa Tanzania Prisons inayonolewa na Mbwana Makata, matokeo hayo yanaifanya iendelee kusalia nafasi ya 13 ikipoteza mchezo wa sita, sare nne na kushinda mbili.
Hii inakuwa mechi ya tano kwa Kocha Juma Mwambusi kuiongoza Coastal tangu atambulishwe kikosini hapo akianza na kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Yanga, Oktoba 26 mwaka huu.
Mechi zilizofuata Coastal ikapata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, 0-0 dhidi ya Singida Black Stars kisha 1-1 mbele ya KenGold na jana ulikuwa ushindi wake wa pili kikosini hapo.