MAKUNDI mbalimbali ya Wanawake wakiwemo walimu na mama lishe wanaendelea kupata elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijisia katika kuadhimisha siku 16 dhidi ya ukatili wa kijinsia sambamba na kupatiwa mafunzo ya matumizi ya nishati safi na kugawiwa majiko ya mitungi ya gesi.
Katika maadhimisho hayo yanayoendelea Barrick na washirika wake wanaendesha shughuli mbalimbali za kutoa elimu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia sambamba na kutoa mafunzo ya matumizi na nishati safi za kupikia na kugawa majiko ya gesi katika mikoa mbalimbali kwa ajili kuunga mkono ajenda ya Serikali ya kulinda mazingira na kuwapunguzia Wanawake ambao ni wahanga wakubwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Washirika wa Barrick katika maadhimisho ya mwaka huu ni Jeshi la Polisi kupitia madawati ya kijinsia, Halmashauri za wilaya,mashirika yasiyo ya kiserikali ya VSO, LCF, Jadra, Hope for the Girls and Women (HGWT) ,kampuni ya wanasheria ya Bowman na kampuni ya uzalishaji na usambazaji nishati ya gesi nchini ya Taifa Gas.
Akiongea katika hafla ya kukabidhi majiko hayo iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) jijini Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi ambaye alikuwa mgeni rasmi alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wanawake kufanya shughuli mbalimbali za mikono ili kujiingia kipato kwa kuwa mtu akiwa na kipato anaondokana na utegemezi unaopelekea kunyanyasika kwenye jamii.
Aliwashukuru wadau wanaoshirikiana na Barrick katika maadhimisho ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia mwaka huu kwa kutoa majiko ya nishati safi ili kutunza mazingira na kuwafanya mama lishe kufanya shughuli zao kwa urahisi na kufanikisha ajenda ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupiga vita mabadiliko ya tabia nchi na uchafufuzi wa mazingira.
Mmoja wa wanufaika wa msaada huo Happiness Kalebe ambaye ni mama lishe wa soko la Mkolani akiongea kwa niaba ya wenzake amesema jiko hilo linakwenda kumuongezea tija katika upishi wake wa chakula na kuhudumia wateja wake.
“Kwa kutumia jiko hili litanifanya nisinunue kuni kwa ajili ya kupikia ambapo nitajiongezea kipato, kipindi cha mvua kama hiki kuna wakati tunanunua kuni zikiwa zimenyeshewa wakati wa kusafirishwa na kutusumbua wakati wa kupika, nawashukuru Barrick na Taifa Gas kwa kututhamini sisi wanawake” amesema Kalebe.