Eneo la kilimo cha Umwagiliaji laongezwa

Unguja. Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar imeongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 875 mwaka 2019 hadi kufikia hekta 2,300 mwaka 2024.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Shamata Shaame Khamis leo Jumatatu Desemba 2, 2024 wakati akijibu swali la mwakilishi wa Kwerekwe, Ameir Abdalla Ameir aliyetaka kujua asilimia ya wakulima wanaokosa huduma ya kilimo hicho.

Akijibu swali hilo, amesema maeneo hayo ya umwagiliaji yanatumiwa na wakulima 14,000 sawa na asilimia 28 ya wakulima wote ambao wangeweza kunufaika na kilimo hicho ikiwa miundombinu hiyo ingekuwepo katika maeneo yenye sifa.

“Hadi sasa maeneo ya kilimo cha umwagiliaji maji yana ukubwa wa hekta 2,300 sawa asilimia 23 ya eneo lote na yanatumiwa na wakulima 14,000 sawa na asilimia 28,” amesema Shamata.

Hata hivyo, amesema kwa kuzingatia umuhimu wa kilimo hicho wizara inaendelea kukarabati miundombinu iliyochakaa ili wakulima wanufaike na kilimo hicho na waondokane na mifumo ya kutegemea misimu ya mvua jambo linalorejesha nyuma uzalishaji.

Pia, amesema wizara inatekeleza miradi mbalimbali ukiwamo wa mfumo wa chakula unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB). 

Hivi karibuni, mratibu wa mradi wa Umwagiliaji Bonde la Mlemele Pemba, Mohamed Hassan Bakari alisema mradi huo upo kwa lengo la kuwakomboa wananchi waliokuwa wanategemea mvua.

Alisema awali, wakulima walikuwa wanavuna tani moja kwa kila ekari moja ila kupitia kilimo cha umwagiliaji utawanufaisha kwa ongezeko la mavuno kutoka tani moja hadi kufikia tani tano kwa kwa ekari.

“Wakulima walikuwa wanategemea mvua ila kwa sasa watalima kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji kitakachosaidia ongezeko la mavuno,” alisema Mohamed. 

Related Posts