Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Ernest Lwila (30) kulipa faini ya Sh5 milioni au kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani, baada ya kupatikana na hatia kwa kosa la kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine.
Pia, mahakama hiyo imemuachia huru mshtakiwa huyo katika shtaka la kuchapisha taarifa za uongo na kuzisambaza mtandaoni bila leseni baada ya kutomkuta na hatia.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo ambaye ni mkazi wa Mlowo, wilayani Mbozi, ameshindwa kulipa faini hiyo, hivyo amepelekwa gerezani.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu, Desemba 2, 2024 na Hakimu Rahim Mushi, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 10 na vielelezo saba.
Akisoma hukumu hiyo, amesema amezingatia hoja za pande zote mbili kwamba mshtakiwa anategemewa na familia yake na anasomesha watoto wawili yatima na kuomba apunguziwe adhabu.
Pia amesema amezingatia hoja za upande wa mashtaka kwamba makosa ya kutumia laini iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, yamekuwa yakijirudia na wakati mwingine watu hutapeliwa na kuomba apewe adhabu kali, ili iwe funzo kwa wengine.
Hakimu Mushi amesema katika ushahidi wake, mshtakiwa amedai laini hiyo aliyokamatwa nayo inatumiwa na mtu aliyemtaja kwa jina la Diana Mwakitalimo ambaye hata hivyo hakumpeleka mahakamani kuthibitisha kwamba ni ya mtu huyo.
Amesema kukosekana kumpeleka shahidi huyo kunafanya mshtakiwa aonekane ametenda kosa hilo, hivyo kutiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.
“Mahakama inakutia hatiani kwa mujibu wa sheria inakuadhibu kulipa faini ya Sh 5milioni au ukishindwa kulipa faini hiyo utatumikia kifungo cha miezi sita gerezani,” amesema hakimu.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru ameiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa kwa kuwa makosa kama hayo yamekuwa yakijirudia na watu wamekuwa hawafuati sheria.
“Mheshimiwa hakimu, makosa ya kutumia laini za simu zilizosajiliwa kwa jina la mtu mwingine yamekuwa yakitumika katika utapeli, hivyo naomba mahakama itoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine” amesema.
Katika hatua nyingine, mahakama imeamuru mshtakiwa kurudishiwa kompyuta mpakato na simu mbili alizokamatwa nazo kwa sababu hazihusiani na kosa alilotiwa hatiani.
Katika kesi hiyo mshtakiwa alidaiwa kutenda kosa hilo Novemba 26, 2022, ndani ya Jamhuri ya Muungano Tanzania.