MADIWANI KENYA WATEMBELEA TARI TENGERU KUJIFUNZA KILIMO

Madiwani kutoka kaunti ya Eligeyo-Marakwet nchini Kenya wametembelea Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha TARI Tengeru kilichopo Arusha kwa lengo la kujifunza shughuli zinazofanywa kituoni hapo ili kuweza kushauri Serikali nchini kwao kutokana na uzoefu wa kazi zinazofanyika nchini Tanzania.

Ugeni huo wa watu 12, ukihusisha madiwani 10, Katibu na dereva ikiwa ni ujumbe wa kamati ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Umwagiliaji katika kaunti ya Eligeyo-Marakwet, umetembelea TARI Tengeru leo Desemba 02, 2024 ambapo baada ya kupata maelezo ya kazi zinazofanywa na TARI wametembezwa maeneo mbalimbali ya utafiti ili kuona kazi mbalimbali za utafiti zinazofanyika.

Akizungumza kuhusu ujio wa wageni hao, Mkuu wa msafara ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mheshimiwa Jeremiah Kibiwott amesema wamechagua kuja kujifunza TARI ikiwa ni Taasisi inayofanya vizuri katika Utafiti wa Kilimo. Amesema ziara hii ni sehemu ya utaratibu wao kujifunza katika Taasisi zinazofanya vizuri za ndani na nje ya nchi ya Kenya TARI ikiwa ni Miongoni.

Mheshimiwa Kibiwott ameendelea kusema, ujio wao Tanzania hususani TARI ni kutokana na kuwa na kiu ya kufahamu tafiti zinazofanyika kwani mazingira na hali ya hewa ya Arusha na eneo wanalotoka inafanana sana hivyo wanaamini matokeo ya utafiti wa TARI Tengeru Tanzania yanaweza kufaa katika maeneo yao nchini Kenya.

Mheshimiwa Kibiwott ameeleza kufurahishwa namna TARI Tengeru inavyofanya Tafiti ambazo zinajibu changamoto za Kilimo na kusema ziara hiyo ni mwanzo wa kuwepo programu za Wataalamu wa pande mbili kubadilishana ujuzi na uzoefu ili kusaidia zaidi Wakulima.

Akitoa wasilisho kwa wageni hao Mkurugenzi Idara ya Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano TARI Dkt Sophia Kashenge amesema TARI kupitia mtandao wake wa vituo 17 nchini inafanya tafiti mbalimbali zinazolenga kuleta tija katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao mbalimbali

Dkt. Sophia amesema ikiwa suala la uzalishaji tija halitazingatiwa athari zake ni uwepo wa njaa hasa wakati huu bara la Afrika linapotajwa kuwa na ongezeko kibwa la Watu.

Kwa upande wake, Meneja wa Kituo cha TARI Tengeru Dkt. Happy Mollel amewapongeza madiwani hao kutembelea TARI Tengeru ambapo amesema wamepata kujifunza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika kituo hicho chenye dhamana ya Utafiti wa Mazao ya Bustani.

Aidha Dkt. Happy amewaeleza wageni hao dhamira ya TARI Tengeru kuendelea kufanya tafiti mbalimbali zinazolenga kuleta tija na kusema kuwa kwasasa kituo kipo hatua za mwisho kutoa aina 19 mpya za mbegu bora za Mazao ya Bustani
Mkurugenzi idara ya Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano TARI Dkt Sophia Kashenge akieleza kwa madiwani wa Kenya walipotembelea TARI Tengeru leo Desemba 02 2024 namna TARI kupitia vituo vyake inavyotekeleza shughuli mbalimbali za Utafiti wa Kilimo
Madiwani wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano wa TARI Dkt Sophia Kashenge wakipata maelezo kuhusu  uzalishaji wa Miche bora ya parachichi aina ya HASS unaendelea kituoni TARI Tengeru
Mwenyekiti wa kamati ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Umwagiliaji kutoka kaunti ya Eligeyo-Marakwet nchini Kenya Mheshimiwa Jeremiah Kibiwott akizungumza Leo Desemba 02 2024, walipotembelea TARI Tengeru kujifunza shughuli za Utafiti wa Kilimo zinazofanywa kituoni hapo

Related Posts