Arusha. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wahasibu wakuu wa Serikali barani Afrika, kujikita katika matumizi ya teknolojia na bunifu ili kuboresha mifumo ya usimamizi wa fedha, uwazi na uwajibikaji kwa umma.
Amesema ili kujenga imani kwa umma, mifumo ya kifedha inapaswa kuwa ya kisasa inayokabiliana na changamoto mpya.
Wito huo umetolewa leo Jumatatu Desemba 2, 2024 na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, kwa niaba ya Waziri Mkuu alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa pili wa mwaka wa Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa Serikali Barani Afrika (AAAG).
Amesema lengo ni kuwa na Afrika inayoshuhudia maendeleo ya kiteknolojia na ongezeko la mahitaji ya huduma bora kwa umma.
Pia, amewataka wataalamu hao kujadili na kuandaa mapendekezo kuhusu umuhimu wa mifumo madhubuti ya usimamzi wa fedha za umma inayoweza kukabiliana na changamoto hizo ikiwamo mabadiliko ya tabianchi.
Majaliwa amesema ni muhimu wataalamu hao wakawa na mijadala inayoakisi maono ya ajenda ya Afrika ya mwaka 2063, inayolenga kukuza maendeleo endelevu na jumuishi kupitia ufanisi katika usimamizi wa fedha za umma na kujikita katika teknolojia na ubunifu.
Amesema pia, wana jukumu la kuongoza mageuzi katika mifumo ya kifedha itakayochochea ukuaji endelevu, kupunguza umaskini na kuhakikisha rasilimali zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.
“Ili kujenga imani kwa umma, mifumo yetu ya kifedha inapaswa kuwa ya kisasa na inayokabiliana na changamoto mpya,” amesema Majaliwa.
Amesema Afrika inashuhudia maendeleo ya kiteknolojia na ongezeko la mahitaji ya huduma bora za umma, hivyo ni muhimu kujikita katika teknolojia na ubunifu ili kuboresha mifumo ya usimamizi wa fedha.
Kuhusu uwekezaji katika miradi ya kijani na nishati jadidifu, amesema wanapaswa kuangalia eneo hilo ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Mapendekezo ya mbinu mpya za kuboresha usimamizi wa fedha za umma kupitia teknolojia ya kidijitali itasaidia kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika fedha za umma na itapunguza rushwa na kuongeza uaminifu wa umma katika mifumo ya kifedha,”amesema.
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema Rais Samia Suluhu Hassan amejizatiti kuliongoza Taifa na kuhakikisha ustawi wake kupitia falsafa ya 4R ambazo ni maridhiano, mabadiliko, ustahimilivu na kujenga upya.
Amesema falsafa hiyo inasaidia kuunganisha jamii, kuimarisha taasisi na kuweka msingi madhubuti kwa mustakabali wa Taifa na inasaidia kuleta mageuzi muhimu ndani ya taasisi kwa kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa fedha za umma.
“Kwa kusisitiza ustahimilivu, anahakikisha kuwa uchumi wa Tanzania unakuwa imara ili kukabiliana na changamoto za sasa na baadaye,” amesema Dk Nchemba. “Nawakaribisha kila mmoja wenu kutoa mchango wake muhimu katika kuimarisha usimamizi bora wa fedha barani Afrika sambamba na maono ya kimkakati yanayohitaji kukabiliana na changamoto ngumu za kifedha zinazotukabili.”
Mwenyekiti wa AAAG ambaye pia Mhasibu Mkuu wa Lesotho, Malehlonolo Mahase amesema mkutano huo wa siku tatu unaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Kujenga imani ya umma katika mifumo ya usimamizi wa fedha za umma kwa ukuaji endelevu.”
“Tunatamani kuwa na Afrika inayowajibika, iliyounganishwa,yenye ustawi na kutatua changamoto zinazotukabili.Masuala mengine ni rushwa kwani rushwa haifanyiki mahali pengine isipokuwa kwenye fedha,” amesema Mahase.
Mhasibu Mkuu wa Tanzania, Leonard Mkude amesema Tanzania imepiga hatua katika kuendeleza utoaji wa taarifa za fedha, matumizi ya mifumo ya kidijitali na kuimarisha nidhamu ya fedha.
“Hili ni jukwaa muhimu la kubadilishana maarifa na hatua ya pamoja ili kujenga taasisi thabiti juu ya usimamizi wa fedha za umma na kuendeleza uendelevu wa kifedha katika bara zima la Afrika,” amesema Mkude.
Ofisa Mkuu wa Biashara kutoka Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema kwa kuwa benki hiyo imekuwa ikishirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC), wameamua kudhamini mkutano huo ili kuvutia uwekezaji kutoka nchi zilizoshiriki mkutano huo.