Matukio ya utekaji bado tishio nchini

Dar/mikoani. Inasubiriwa atekwe nani ili hatua zichukuliwe? Ndilo swali wanalojiuliza wengi kuhusu giza lililogubika mwenendo wa uchunguzi wa matukio ya utekaji na kutoweka kwa raia yanayofanywa na watu wasojulikana.

Msingi wa swali hilo ni mashaka waliyonayo wananchi juu ya kukithiri kwa matukio hayo ambayo yanaendelea kuwa tushio, huku mamlaka zikiishia kuahidi kuchukua hatua, bila kutoa taarifa ya utekelezaji.

Majibu kama ‘uchunguzi unaendelea, tupo hatua za mwisho za uchunguzi na tuvipe nafasi vyombo husika vifanye kazi yake’ ndio  aghalabu hutolewa na mamlaka, bila kushuhudiwa matokeo.

Miongoni mwa matukio hayo ni linalomhusu aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya Chadema, Ali Kibao aliyechukuliwa jioni ya Septemba 6, 2024 eneo la Kibo Complex, Tegeta Dar es Salaam na watu wasiojulikana akiwa katika usafiri wa umma na siku moja baadaye mwili wake ukaokotwa eneo la Ununio nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ukiwa na majeraha.

Licha ya Rais Samia Suluhu Hassan kulaani tukio hilo la Kibao na kuagiza uchunguzi na hatua dhidi ya wahusika, hadi sasa ni zaidi ya siku 85 zimepita haijatolewa taarifa yoyote kuhusu mwenendo wa uchunguzi wala hatua za tukio hilo.

“Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili (la Kibao) baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi.

“Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,” aliandika katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Septemba 8, 2024.

Wakati tukio hilo na mengine ya kutekwa, kutoweka kwa watu wanaodaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana yakiwa hayajapata ufumbuzi, linaibuka jingine la

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT- Wazalendo, Abdul Nondo kuchukuliwa na watu wasojulikana.

Nondo alichukuliwa alfajili ya Jumapili, Desemba 1, 2024 katika Kituo cha mabasi cha Magufuli, Dar es Salaam akitokea Kigoma kwenye shughuli za kisiasa. Kelele za wadau mbalimbali zilipazwa. Jeshi la Polisi likasema linafuatilia kwani alichukuliwa na watu wasiojulikana wakiwa na gari aina ya Land Cruisers.

Jana Jumapili usiku, Nondo alipatikana akiwa na majeraha na kukimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya matibabu. Polisi  walisema Nondo alitelekezwa fukwe za coco na watu asiowafahamu.

Polisi wakasema Nondo alisimamisha bodaboda na kumwelekeza dereva  amfikishe ofisi za chama chake Magomeni Dar es Salaam. Polisi walisema wanaendelea kufuatilia suala hilo.

Tukio la Nondo nalo linaibua wasiwasi iwapo uchunguzi na hatua zitachukuliwa kwa wahusika.

Maswali yanakuwa mengi zaidi hasa, kutokana na mamlaka hizo hizo kuwa na ufanisi wa uchunguzi na kuchukua hatua za haraka katika baadhi ya matukio, likiwemo la ubakaji wa binti wa Yombo Dovya.

Katika tukio hilo, ni la Agosti 2024, ilichukua mwezi mmoja tangu liliporipotiwa, watuhumiwa walikamatwa na kufikishwa mahakamani, hatimaye hatua zikachukuliwa na wote waliofikishwa mahakamani wakahukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Tukio lingine ni lile linalomhusu kijana aliyechoma picha ya Rais, alikamatwa ndani ya muda mfupi na kuhukumiwa.

Kuchelewa kwa upelelezi ni moja ya changamoto zinazolikabili Jeshi la Polisi, hata ripoti ya Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Samia ililibainisha hilo.

Tume hiyo iliyoongozwa na Jaji mstaafu, Chande Othman iliangalia mifumo yote ya haki jinai na katika mapendekezo yake ilitaka Jeshi la Polisi lifanyiwe tathmini.

Katika mapendekezo yake ya Julai 2023, ilisema tathmini kwa jeshi hilo, iwezeshe kuwapo maboresho makubwa na kuundwa upya ili kuondoa kasoro za kiutendaji.

Leo Jumatatu, Mwananchi limemtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime  kuhusu matukio mbalimbali  ya utekaji na watu kutoweka ambapo amesema: “Tukio lolote lile la jinai linapotokea Jeshi la Polisi hulipa uzito mkubwa wa kukusanya ushahidi sambamba na kutafuta aliyetenda au waliotenda uhalifu wenyewe.”

“Wapo watuhumiwa ambao kulingana na ushahidi uliopatikana kutokà kwa watendewa, watu wengine na uchunguzi wa kisayansi, husaidia kumkamata au kuwakamata wahalifu kwa muda mfupi sana na mara nyingi na kwa kiasi kikubwa makamanda wa Polisi mikoa na vikosi mmekuwa mkiwasikia wakitangaza kukamatwa kwao.’’

Misime amesema yapo matukio machache ambayo wahalifu huchelewa kukamatwa kutokana na ushahidi uliopatikana wakati mwingine aliyetendewa hatoi ushahidi utakaowezesha kumkamata mhalifu kwa wakati mpaka utumie mbinu mbalimbali hadi kumfikia.

“Lakini pia ikumbukwe waliotenda uhalifu ni binadamu na wana akili na hutumia mbinu nyingi kujificha na hufikia wakati mwingine huvuka mipaka ya nchi,” amesema.

Kuhusu ukimya wao, Misime amesema si utaratibu wa kiuchunguzi kila siku lazima wazungumze wamefikia hatua gani, kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kumkimbiza mhalifu zaidi.

“Lakini pia hatua za kiupelekezi ni moja ya mambo yatakayowasilishwa mahakamani sasa huwezi kuweka ushahidi hadharani,” amesema.

“Hivyo wananchi waelewe kuna kazi kubwa inafanywa na Jeshi la Polisi na mhalifu anaweza kutenda uhalifu na kukamatwa muda mfupi tu kama inavyofanyika, wapo wengine huchukua muda kiasi ndipo hukamatwa.

Tunachoweza kuwaambia wananchi ni kwamba hakuna kesi ya jinai inayokufa na sasa hivi mifumo ya kielektroniki imewezesha kuhifadhi kumbukumbu za kesi kwa muda mrefu, hivyo aliyetenda uhalifu inaweza kuchukuwa muda mrefu kumkamata lakini ipo siku atakamatwa,” amesema.

Ameongeza; “Tushirikiane kwa kutoa taarifa za kweli na sahihi na siyo zile za uongo za kutaka kuchafua mtu au taasisi au za kishabiki na za uongo za mtandaoni.”

Mbali na hao, raia wengine zaidi ya 80 wanadaiwa kutoweka na baadhi yao kuuawa na wasiojulikana, kama ilivyoripotiwa Agosti 2024 na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Wito wa uchunguzi kuwabaini wahusika na kuundwa tume ya kijaji itakayochunguza matukio yote kwa jumla, umekuwa ukitolewa na wadau wa haki za binadamu, wanasiasa na wanaharakati nchini.

Hata hivyo, wadau wanatoa wito huo wakati tayari Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), ilishaanza uchunguzi wa matukio ya namna hiyo.

Miongoni mwayo ni la Juni 2024, kijana Edgar Mwakabela maarufu ‘Sativa’ naye alikumbwa na tukio hilo, akichukuliwa na wasiojulikana kisha kupigwa risasi ya kichwa na kutelekezwa kwenye hifadhi ya Katavi Juni mwaka huu.

Agosti 2024, Katibu wa Umoja wa Vijana Chadema (Bavicha), Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na wenzake wawili, Jacob Mlay na Frank Mbise, walitoweka tangu Agosti 2024.

Kiongozi wa Chadema, wilaya ya Sumbawanga, Rukwa, Dioniz Kipanya, naye inadaiwa alitekwa. Wote hao mpaka sasa hawajulikani walipo.

Novemba 12, 2024 kupitia video yenye sekunde 49 iliyosambaa katika mitandao ya kijamii alionekana kijana aliyetambuliwa kwa jina la Deogratius Tarimo akilazimishwa kuingia ndani ya gari aina ya Toyota Raum na vijana wawili.

Wakati tukio hilo likiendelea, Tarimo alikuwa akipiga mayowe ya kuomba msaada huku akisema: “Naenda kuuawa..nisaidienii” hata hivyo, miongoni mwa waliomkamata alisema “Sisi ni maaskari…twende Gogoni”

Sura za vijana hao waliokuwa na pingu zilionekana kupitia video hiyo ambayo hadi mwisho inaonyesha, Tarimo alifanikiwa kujichoropoa mikononi mwao.

Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, lilisema inaendelea na uchunguzi kubaini wahusika wa tukio hilo.

Ingawa inaonekana Serikali ina uwezo wa kudhibiti matukio hayo, kilichokosekana ni mkakati wa kufanikisha hilo, kama inavyoelezwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa kiroho, viongozi wa dini wanaona Serikali ina uwezo wa kudhibiti matukio ya utekaji, japo hakuna mkakati wa uhakika kutekeleza hilo.

“Kwa uwezo mkubwa wa Serikali wa kudhibiti matukio haya tunashangaa yanaizidi nguvu, jambo linaloibua maswali kama ni kweli Serikali ina udhaifu wa kiasi hicho hadi matukio haya yaendelee,” amesema Padri Kitima.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Alhaj Nuhu Mruma, alisema matukio ya utekaji yanasikitisha na hayakubaliki katika jamii.

“Hatujui yanafanywa na kina nani na kwa dhamira gani, tunayalaani kwa nguvu zote na tunaomba vyombo vyote vya kisheria kuchunguza mambo haya kwa undani haki ipatikane bila kumuonea mtu,” alisisitiza Alhaji Mruma.

Kwa mtazamo wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, matukio hayo, hayajaishinda nguvu Serikali, isipokuwa tatizo ni kukosekana kwa nia ya dhati ya kuyashughulikia.

“Kama vyombo husika havishughulikii ndio kunasababisha watu wahisi wao wenyewe ndio wahusika, kama kitu kinafanyika na upo kwenye nafasi ya kufanyia kazi na hufanya watu wanahisi wewe ndio unakifanya,” amesema.

Henga amependekeza wanaohusika kuchunguza matukio hayo, waanze kuchunguzwa wao, kwa sababu ndipo tatizo linapoanzia.

Mwanazuoni wa Sheria, Profesa Gamaliel Fimbo alipendekeza Polisi kubadili utaratibu wake wa kutoa taarifa.

Badala ya taarifa za mwenendo wa uchunguzi wa matukio kama hayo kutolewa na msemaji wa jeshi hilo pekee, makamanda wa wilaya wapewe mamlaka hiyo pia.

“Nchi kubwa, mikoa mingi na wilaya nyingi. Kwanini walioko wilayani wasipewe mamlaka ya kutangaza ilimradi tu mkubwa wake awe anajua,” amehoji.

Sambamba na hilo, amesema mwenendo wa ukimya wa muda mrefu kuhusu matukio ya uchunguzi, unaibua mashaka kwa wananchi.

Kwa mtazamo wa mwanazuoni huyo, kuna mbinu nyingi na zinazojulikana na kumpata mhalifu, isipokuwa mwenye mamlaka na uchunguzi hatekelezi wajibu wake.

“Tunafikia kwenye hatua ambayo nchi inaitwa a failed state (taifa lililoshindwa). Kwenye nchi ya namna hiyo kila unachouliza huwezi hupata majibu. Kwanini tufike huko, wakati tumesoma,” amehoji.

Amehoji pia kwanini wengi kati ya wanaotekwa wanahusiana na vyama fulani pekee.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema matukio ya utekaji kuendelea kuripotiwa,  ni fedheha kwa Taifa.

“Mfano tukio la Tarimo ambaye alinusurika kutekwa na watu sura zao zilionekana mchana kabisa, hao watu wanataka kutuambia wanaweza kufanya lolote ni fedheha kubwa sana na ni dharau kwa Watanzania na ni jambo ambalo lazima hatua zichukuliwe,”alisema.

Kuhusu kutambua alipo mtu aliyetekwa kwa kutumia simu ya mkononi, mtaalamu wa usalama mitandaoni, Roshan Pyar alisema inawezekana kwa Jeshi la Polisi kushirikiana na kampuni ya laini ya simu anayotumia mtu aliyetekwa ama kutoweka.

“Polisi wanaweza kushirikiana na kampuni ya mtandao wa laini ya simu anayotumia mhusika na kubaini alipo na anapopelekwa, pia kama wana namba ya IMEI wanampata mhusika alipo,” alisema.

Mtaalamu wa Tehama jina limehifadhiwa anasema upo mfumo wa uongozaji satellite ambayo inaweza kutambua wapi mmiliki wa simu yupo mara ya mwisho hata baada ya simu kuzimwa.

“Pia zipo application za simu ambazo hulipiwa, unaweka namba ya simu inakuonyesha mhusika yupo wapi kwa muda fulani na anaelekea wapi,” alisema.

Aliongeza;  “Mfano pale stendi ya Magufuli kuna kamera, unaziangalie zile, kisha unaanza kuangalia kamera za maeneo barabara inakopita, unaangalia hilo gari kwa kusaidiana na mitandao ya simu unabaini wahusika kwa urahisi kabisa.”

“Au lile tukio la Kibao kule Tegeta, maeneo ya kuanzia Makonde kuna camera za watu binafsi hadi Bunju, unaweza kuwaomba ukaangalia ukaona magari yanayopita na yale yanayokwenda kumchukua. Kikubwa teknolojia inaweza kufanya lolote kama kuna utashi wa kukomesha matukio haya.”

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917

Related Posts