Dar es Salaam. Mwakilishi wa wabunge walio wachache bungeni, Halima Mdee amesema aliyekuwa mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile alikuwa wa moto, akimaanisha alisimamia kile alichokiamini bila kuyumba.
Mdee ambaye pia mbunge wa viti maalumu, amesema kitu pekee ambacho wengine wanapaswa kujifunza kutoka kwa Dk Ndugulile ni “Kuwa wa moto ili tusaidie nchi na kuinua Taifa.”
Mdee amesema hayo leo Jumatatu, Desemba 2, 2024 wakati akitoa salama za rambirambi kwenye hafla ya kuaga mwili wa Dk Ndugulile katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam. Waombolezaji mbalimbali wameshiriki, wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema Dk Ndugulile aliyefariki dunia 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu, alitumia muda wake mwingi kuwakilisha wananchi wake wa Kigamboni na kazi za kitaifa kwa kweli tupu bila kujali itamgharimu nini.
Mdee amesema Dk Ndugulile hakuwa mnafiki na kama ana jambo lake lazima atahakikisha litatekelezwa.
Katika salamu zake, Mdee amesema watu waliokuwa wakifuatilia kazi za Dk Ndugulile za kisiasa wanajua ajali kadhaa alizowahi kuzipata kwa sababu ya kuzungumza ukweli.
“Inawezekana hatukumuelewa kipindi kile, lakini tumekuja kumuelewa… Taifa lilimuamini na kumchagua kuwa mwakilishi wa Tanzania kupambania nafasi ya kanda ya Afrika WHO na akashinda na leo wenzetu wa tasnia ya afya wanamzungumza vyema,” amesema Mdee.
Pia amesema Dk Ndugulile alikuwa mtii ambaye hakuwa wa baridi au vuguvugu, bali wa moto.
“Mtoto wake amesema hapa hutakiwi kuwa baridi wala vuguvugu, bali uwe wa moto ili utimize malengo. Watu wengi sisi tupo katikati kwa sababu tunakuwa baridi au vuguvugu, ndiyo tunaita unafiki lakini Dk Ndugulile alikuwa wa moto na watoto wake wanajua,” amesema Mdee.
Amesema kitu ambacho wengine wanapaswa kujifunza ni kuwa wa moto ili wasaidie nchi na kuinua Taifa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema Dk Ndugulile alikuwa mnyenyekevu anayeheshimu watu, anayejali na kutafuta matatizo ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi.
Amewataka viongozi wa CCM na vyama vingine kuiga maisha ya Dk Ndugulile ambayo yanamjali Mtanzania wa kawaida na kumpa kipaumbele.
“Alijiepusha kabisa na ubinafsi na kuwatanguliza wananchi mbele, haya ndiyo maisha ambayo CCM ingependa kila kiongozi wake na kiongozi wa Taifa hili ayaishi,” amesema Dk Nchimbi.
Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema anatambua weledi wa ufanyaji kazi wa marehemu katika utumishi wake, ikiwemo kuishauri Serikali namna ya kuhudumia wananchi wake wa Kigamboni.