Mila, desturi kandamizi chanzo cha ukatili

Dar es Salaam. Kila mwaka Novemba 25 hadi Desemba 10, dunia hujikita kwenye kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Ukatili huu unatajwa kuwaathiri wanawake na watoto ukilinganisha na idadi ya wanaume wanaokutana na ukatili huo.

Kihistoria, siku hii ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 1981 ikiwa mi njia ya kuwaenzi wanaharakati wa kisiasa Mirabal Sisters waliouawa mwaka 1960 huko Jamhuri ya Dominika kwa amri ya aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Rafael Trujillo.

Mwaka 1993 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na kuteua siku hizo, kuendesha kampeni za kupinga ukatili.

Sambamba na harakati hizo za kumkomboa mwanamke, kumekuwa na mila kandamizi kwa wanawake kwa baadhi ya makabila huku zikijificha kwenye kivuli cha mila, tamaduni na desturi za kabila husika.

Mila hizo hufanyika na baadhi ya makabila kama vile Wamasai, Wachaga, Wabarbaiq, Wakurya na makabila mengine mengi.

Baadhi ya mila hizo ni pamoja na kukeketwa, kuibwa na kwenda kuolewa pasipo na ridhaa ya wazazi wala binti, kuolewa katika umri mdogo, umaskini unaosababisha mtoto kuolewa kwa matakwa ya wazazi pekee, mwanamke kutoshirikishwa katika uamuzi na ubaguzi wa majukumu ya kifamilia.

Mwananchi limezungumza na baadhi ya wananchi kuhusu namna ubaguzi huo ulivyoathiri uthubutu wa kundi hilo katika jamii, na wamesema ukandamizwaji ndiyo chanzo cha wanawake kujiona wanyonge katika jamii.

Flackian John, mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro anasema baadhi ya mila hizo huabudiwa katika jamii, huku wakizihalalisha kupitia mila na desturi.

“Sidhani kama kuna tofauti ya mtoto wa kike na wa kiume hasa katika mgawanyo wa majukumu wanapo kuwa nyumbani. Aina hii ya mawazo inapaswa ikemewe ili kuondoa mnyonyoro wa mila kandamizi katika jamii,” anasema.

Anasema ubaguzi kwa wanawake mara nyingi huondoa kujiamini na huchochea dharau, hali ambayo si rafiki kwa ustawi wa mwanamke na jamii kwa ujumla.

“Wanasema ukimwelimisha mwanamke umeelimisha jamii nzima, msemo huu unamaanisha hivyo kama jamii tumuunge mkono mwanamke na si kumkandamiza kila iitwapo leo,” anasisitza John.

Naye, Allan David  anasema jamii zinazo mkandamiza mtoto wa kike au mwanamke kwa kiasi kikubwa ni za vijijini,  ambazo hazijapata elimu ya kutosha kuhusu usawa wa kijinsia kati ya mwanaume na mwanamke.

“Baadhi ya jamii zimekuwa zikimkandamiza mtoto wa kike kielimu na haki kadha wa kadha, baadhi yao huona elimu ameumbiwa mtoto wa kiume pekee, kitu ambacho si sahihi. Wapo wanaompeleka shule na kisha anapotokea muoaji saa yoyote ile humkatisha masomo na kumuozesha,” anasema.

David anasema kumekuwa na mila za kumuwahi mke bado akiwa tumboni hajazaliwa, hii mara nyingi hutokana na wazazi kuona mtoto wa kike ni mtaji.

“Kuna baadhi ya familia mtoto wa kike hufanya kazi za nyumbani peke yake, bila msaada wa mtoto wa  kiume, hata akiwepo mara nyingi hawatoi msaada, yote haya chanzo ni fikra potofu kuwa kazi za nyumbani ni za mtoto wa kike pekee,” anaeleza na kuongeza;

“Hali hii humuharibu mtoto wa kike kisaikolojia na kupunguza kujiamini katika lolote huku akijishusha thamani na kuona yeye si kitu katika familia,” anasema.

 Anasema ubaguzi wa aina hiyo humfanya mtoto ashindwe kutimiza ndoto zake kutokana na kutoona thamani yake, na hata akijaribu kutimiza ndoto hizo hazitathaminiwa  kuanzia ngazi ya familia na jamii.

“Wanaharakati wa haki za wanawake wanapaswa wakishirikiane na serikali kufikisha elimu katika maeneo ambayo ubaguzi huu umekithiri kwa kutumia mabango, vipeperushi na vipindi mbalimbali vya runinga na redio na kuwepo na adhabu kali kwa yeyote atakaye thibitika kufanya ubaguzi kwa mtoto wa kike,” anasema David.

Naye  Mkurugenzi wa Dag project Tanzania, Lightness Mkolela anasema baadhi ya mila zimekuwa zikimkataza mtoto wa kike kuingia kwenye uongozi katika jamii.

“Kuna baadhi ya mila zinaendelea kumkandamiza mtoto wa kike hasa katika kuwanyima kauli kwenye jamii. Ukatili wa kingono kwa mtoto wa kike ni moja ya unyanyasaji uliokithiri,  huku hali hiyo ikitajwa kuwa ni chanzo cha sonona kwa kundi hilo,” anasema.

Mkolela anasema moja ya matokeo ya mila kandamizi ni kumchagulia mtoto wa kike mume, kitu ambacho huchochea visa na mikasa ya kuuana na kufanyiana vitendo vya kikatili katika maisha ya ndoa.

“Unapomchagulia binti mwanaume asiyemtaka, mara nyingi atabeba machungu na roho ya visasi ambapo mwishowe huyatoa kwa kufanya matukio ya kutisha kwenye jamii,” anasema Mkolela.

Anasema ubaguzi wa mtoto wa kike hasa katika kufanya uamuzi, mara nyingi unamrudisha nyuma kimaendeleo.

“Kuna mila pia zinamkataza mtoto wa kike kumiliki ardhi au nyumba, hali hii humuathiri mwanamke hasa anapofiwa na mume na mali zake na mumewe kutaifishwa na upande wa mwanaume huku wakidai mwanamke hana uwezo wa kumiliki mali hizo ambazo kimsingi ni mali za watoto,” anasema.

Mkurugenzi wa taasisi ya Binti Makini , Janeth John anasema kuna unafuu akilinganisha tulipotoka na tulipo katika suala zima la kupinga ukatili wa kijinsia.

“Kipindi cha nyuma, suala la uongozi kwa mwanamke ilikuwa ni kitu cha ajabu na kigumu sana kwa baadhi ya makabila tofauti na sasa,” anasema mkurugenzi huyo.

“Kipindi cha nyuma, ukatili wa kijinsia ulikuwa ukichukuliwa kama kitu cha kawaida, na kuwa mambo hayo yalifanyika hadharani tofauti na sasa,” anasema Janeth.

Anasema kupitia elimu zinazotolewa na Serikali, wanaharakati na vyombo vya habari imeweza kusaidia kupunguza ukatili kwa wanawake kwa asilimia kadhaa tofauti na kipindi cha nyuma.

“Kwa kiasi, elimu imesaidia kuokoa wanawake katika jamii, watu wameacha na wanaogopa kufanya ubaguzi au ukatili kutokana na sheria zilizopitishwa kuhusu mtu aliyethibitika kufanya ukatili huo,” anasema Janeth.

Anasema moja ya njia zlizosaidia kuwafikia watu katika jamii, ni matangazo kupitia vyombo vya habari katika ngazi zote na elimu zinazotolewa na wanaharakati wa haki za wanawake.

“Ndoa za utotoni bado ni tatizo kwa maeneo ya kanda ya ziwa ukilinganisha na mikoa mingine huku chanzo kikiwa ni mahari kubwa anayopokea mzazi, hali hii chanzo cha familia nyingi kuchukua uamuzi huo usio sahihi,” anasema.

Anasema moja ya njia bora ya kutokomeza unyanyasaji ni kuonesha kwa mifano namna  mwanamke anavyoweza kufanikiwa.

 Anasema mwanamke anapofanikiwa ni vyema asambaze habari njema katika jamii,  ili kuwapa chachu ya kuamini kuwa mwanamke anaweza.

“Hata kama hawaamini kwamba mwanamke anaweza, basi watakapoona mfano kwa mmoja aliyefanikiwa, watajenga imani na hata kuwekeza kwa mtoto wake wa kike,” anasema.

Mikoa iliyotajwa kuongoza ukatili wa kinjisia ni pamoja na Arusha katika jamiii ya Wamasai, Shinyanga,  Wasukuma, Mara,  Wakurya, Tabora na Singida.

Related Posts