BAADA ya ushindi wake wa pili tangu amejiunga na Pamba FC, kocha Fredy Felix ‘Minziro’ amesema bado anajitafuta kuhakikisha anaifanya timu hiyo kuwa bora.
Pamba FC chini ya Minziro imeshinda mechi dhidi ya Fountaine Gate ugenini mabao 3-1 na juzi imeshinda mbele ya Ken Gold bao 1-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Minziro alisema mdogo mdogo wanasogea kwenye mafanikio japo ni mapema sana kujihakikishia hilo kutokan ana timu yake kukosa mwendelezo wa matokeo mazuri.
“Tulichokuwa tunakitarajia kimefanikiwa dhidi ya Ken Gold japo kwa ushindi mwembamba nimefurahishwa na upambanaji wa wachezaji wangu nitaendelea kuwajenga ili tuweze kubaki msimu ujao,” alisema.
“Tumesogea nafasi ambayo sio hatari kwetu kutoka 15 hadi 12 sio haba kilichopo ni namna ya kutengeneza muendelezo wa ushindani ili kujihakikishia nafasi ya kubaki msimu ujao makosa madopdo madogo bado yapo naamini nitaendela kuyafanyia kazi.”
Minziro alisema kuwa Ligi Kuu Bara msimu huu ni ngumu mipango imara ndio inaweza kuamua matokeo ndani ya sakika 90 za mchezo huku akisisitiza kuwa kwa upande wa Pamba FC bado anakazi kubwa ya kufanya ili iweze kuwa timu shindani.
“Licha ya kupata ushindi mara mbili nikiwa na timu hii nina kazi kubwa ya kufanya ili kuikwamua kwenye janga la kushuka daraja siwezi kuiweka kwenye daraja la kutwaa taji licha ya mechi nyingi kusalia napambana icheze msimu ujao.”