Morogoro yaanza kupata mvua, Ma-DC waja na mikakati kukabili athari

Morogoro. Maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro yameanza kupata mvua, huku wakuu wa wilaya na viongozi wengine wa halmashauri wakiweka mikakati ya kuepuka athari zinazoweza kutokea kutokana na mvua hizo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu, Desemba 2, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Danstan Kyobya amesema mvua hizo zimeanza kunyesha tangu jana katika maeneo mengi ya wilaya hiyo.

Hata hivyo, amesema mpaka leo mchana hakuna athari yoyote iliyosababishwa na mvua hizo.

Mkuu huyo wa wilaya amesema ili kukabiliana na mvua hizo kubwa zilizotabiriwa na TMA, tayari wameweka mikakati ya kukabiliana na madhara yatakayojitokeza

Kyobya amesema Serikali ya wilaya imeanza kutoa elimu kwa njia ya matangazo ya wazi na kupitia redio ya halmashauri kwa wananchi, ikilenga kutoa tahadhari hasa kwa wale wanaoishi maeneo ya mabonde na kuwataka kuhama.

“Hatujui hizi mvua zitakuwa nyingi kiasi gani, hivyo tumeendelea kuwashauri wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni na wale wanaoishi jirani na mito, wachukue tahadhari mapema,” amesema Kyobya.

Amesema anaamini kukamilika kwa ujenzi wa tuta la mto Lumemo unaodaiwa kuwa chanzo kikubwa cha mafuriko katika maeneo mengi ya Mji wa Ifakara, utasaidia kuzuia mafuriko kama yatatokea.

“Tuta hili litapunguza kwa kiasi kikubwa madhara yatokanayo na mvua, maana litazuia maji yasitawanyike. Mafuriko yaliyotolea Mei 5, mwaka huu katika mji wa Ifakara, chanzo kikubwa kilikuwa huu mto ambao unakatiza jirani na mji wa Ifakara,” amesema Kyobya.

Mkakati mwingine ametaja kuwa ni kukaa na wavuvi na kuwapa tahadhari za kuchukua wakati wa mvua.

Akizungumzia miundombinu ya barabara na majengo, Kyobya amesema bado haijaathirika na shughuli za kiuchumi zinaendelea kama kawaida.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amesema mvua zilizoanza kunyesha wilayani humo tangu Desemba mosi, 2024 hazijaleta madhara.

Hata hivyo, amesema tahadhari ni muhimu, hivyo Serikali imewataka wananchi wanaoishi maeneo ya mteremko, mabondeni na shambani hususani ya mpunga kuhama kabla mvua hazijaongezeka.

“Wilaya ya Kilosa ina historia ya kukumbwa na mafuriko ya mara kwa mara, hivyo TMA inapotangaza uwepo wa mvua kubwa, mimi kama kiongozi na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, lazima nichukue hatua.

“Hatua ya kwanza ni kuyabaini maeneo ambayo yana historia ya kukumbwa na mafuriko na baada ya hapo ni kutoa tahadhari kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwaomba waondoke kwenye maeneo hayo,” amesema Shaka.

Maeneo mengine yaliyoanza kupata mvua ni pamoja na Wilaya ya Malinyi, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Khamis Katimba akizungumza na Mwananchi amesema uongozi wa halmashauri hiyo umekutana na watendaji wa kata na vijiji na kuwapa maagizo ya kipi cha kufanya katika kipindi hiki

Katimba ametaja hatua nyingine ni kuwaondoa wananchi wanaoishi kando ya hifadhi ya mito ambao ndio wamekuwa waathirika wakubwa wa mafuriko yanapotokea.

Kwa upande wa Manispaa ya Morogoro, maeneo yaliyokuwa kwenye hatari ya kukumbwa na mafuriko ni pamoja na Kata ya Lukobe, Mafisa, Kichangani, Mkundi na Mwembesongo.

Hata hivyo, licha ya mvua kubwa zilizotabiriwa na TMA na Serikali kutoa tahadhari, wananchi wameendelea kuishi kwenye maeneo hayo kwa madai hawana pa kwenda kuishi.

Ofisa mtendaji wa kata ya Lukobe, Manispaa ya Morogoro, Mariam Rajabu amesema wananchi wa kata hiyo wanaoishi maeneo hatarishi wameshapewa tahadhari, licha ya kutochukua hatua kama wanavyoelekezwa.

“Nimeshatoa tahadhari, hata wataalamu wengine kutoka taasisi na mashirika mbalimbali, ikiwemo ActionAid wameshakuja na kuwaambia wananchi wasogee, lakini ndio kwanza watu wanaendelea kujenga uzio wakiamini ndiyo kinga ya mafuriko badala ya kuhama.

 “Mafuriko yaliyotokea Januari 25 mwaka huu yalikuwa na madhara makubwa na watu wameona walivyopoteza samani za ndani, lakini sasa watu wakiambiwa wanakuwa wagumu kusikia, wachache ndio wamehama baada ya mafuriko ya Januari,” amesema.

Related Posts