Moshi. Isaack Mallya (72), mkazi wa Kijiji cha Umbwe Onana, Kata ya Kibosho Magharibi, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro amekutwa ameuawa nyumbani kwake na watu wasiojulikana, huku mwili wake ukiwa ukitelekezwa nje ya nyumba hiyo.
Mwili wa Mallaya umekutwa asubuhi ya leo Jumatatu, Desemba 2, 2024 ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa akizungumza na Mwananchi amesema tukio hilo limetokea leo asubuhi na wanafuatilia kujua waliohusika.
“Ni kweli kumetokea tukio hilo la mauaji na huyu mzee amepigwa na kitu kizito kichwani, tunafuatilia kuwabaini waliohusika na mauaji haya,” amesema Maigwa huku akiongeza kuwa kesho Jumanne, Desemba 3, 2024 atatoa taarifa rasmi.
Kaka wa marehemu, Patrick Boisafi ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro ameeleza kusikitishwa na ukatili aliofanyiwa kaka yake akisema wameliachia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi kuwabaini waliohusika, ili sheria ichukue mkondo wake.
Mbali na tukio la kuuawa kwa kaka yake, Boisafi amekumbushia tukio la kuuliwa kwa ng’ombe wa marehemu, akieleza huenda wakati huo walipanga kutekeleza mauaji hayo na kukosea katika kujipanga.
“Huyu ni kaka yangu, mtoto wa baba yangu mkubwa, tumeishi wote mji mmoja na mahali alipouawa ndipo nimekulia hapo. Ni jambo la kikatili limefanyika katika jamii, naamini Jeshi la Polisi litafanya bidii kuchunguza matatizo yaliyotokea na kuwatafuta waliohusika ili hatua za kisheria zichukuliwe,” amesema Boisafi.
Amesema tukio lililofanyika halikubaliki katika jamii na linatia hofu hasa kipindi hiki kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka na kueleza kama walikuwa wanamdai wangesema walipwe kwa kuwa hakuna kitu chenye thamani ya uhai wa mtu.
Kwa upande wake, mfanyabiashara maarufu katika Manispaa ya Moshi, Baraka Mallya ambaye ni ndugu wa marehemu, amesema: “Marehemu Isaack zamani alikuwa mfanyabiashara, lakini baadaye alirudi kijijini hapo alikouawa akiishi kuendelea na shughuli zake nyingine.”
Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Vick Massawe amesema:“Huyu baba alikuwa ni mchangamfu na kila mtu hapa Kijijini na alikuwa hana shida na mtu, sasa leo asubuhi tunaambiwa mwili wake umekutwa nyumbani kwake nje ukiwa na majeraha na damu zikivuja sana, huyu mzee kauawa kwa mateso sana.”