Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inathamini mchango wa jukwaa la Wakurugenzi Watendaji (CEO Roundtable -CEOrt) katika kuchangia jitihada za kujenga uchumi endelevu na unaostawi hapa nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia katika sherehe za Chakula cha Jioni za mwaka 2024 ( CEOrt 2024 Dinner Gala) zilizofanyika katika Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro, Dar es Salaam, Jumamosi, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango alilipongeza jukwaa hilo na washirika wao kwa juhudi zao za kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi hapa nchi.
“Nawaletea salamu za heshima kutoka kwa H.E. Dr. Samia Suluhu Hassan, ambaye hakuwepo hapa leo kwa sababu ya majukumu mengine, lakini ameniagiza niwasilishe shukrani zake kwenu za dhati kwa mazuri mnayoyafanya,” alisema Dkt. Mpango.
“Rais anathamini michango yenu isiyokuwa na kikomo na kujitolea kwenu katika kujenga uchumi endelevu kwa kuwahusisha wadau mbalimbali wa sekta ya umma na sekta binafsi.”
Makamu wa Rais alielezea furaha yake katika juhudi za CEOrt zinazohusiana na masuala mbalimbali ikiwemo mazingira ya biashara na maendeleo ya rasilimali watu.
Alisema kauli mbiu ya usiku wa sherehe hii hizo za CEOrt mwaka huu inayosema “2050… Twende!” Kujenga Uchumi Uliostawi, Jumuishi, na Endelevu, na kusema kwamba inahusiana na Malengo ya Serikali ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, ambayo inalenga kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2050.
“Tunahitaji kuendelea kuzingatia masuala muhimu kama mabadiliko ya tabianchi na kutathmini athari zake kwenye mazingira ya biashara,” aliongeza. Akielezea ushiriki wake hivi karibuni kwenye mkutano wa COP 29, Dkt. Mpango alisisitiza ahadi ya Tanzania katika malengo ya kimataifa ya tabianchi na kusema ni muhimu kujenga uchumi imara licha ya changamoto za tabianchi.
“Kwenye hotuba yangu katika COP 29, nilisema kwamba mabadiliko ya tabianchi yanapunguza hadi asilimia 2-3 ya Pato la Taifa la Tanzania kila mwaka, na kuleta hasara ya mabilioni ya shilingi,” alisema Dkt. Mpango.
“Inafurahisha kuona kuwa CEOrt pia ina juhudi za kuhamasisha biashara kujiunga na ajenda ya tabianchi.”
Dkt. Mpango aliwahimiza wanachama wa CEOrt kuendeleza juhudi zao kwa kubuni suluhisho bunifu na kuanzisha ushirikiano ambao utasaidia biashara kuendana na malengo ya tabianchi ya Tanzania na kunufaika na fursa zitakazotokana na hilo.
Makamu wa Rais pia alisisitiza uwekezaji unaoendelea wa Serikali katika sekta muhimu za miundombinu kama vile barabara, reli, maji, usafiri wa angani, na nishati, ambazo zote ni muhimu kwa ukuaji na maendeleo ya uchumi.
“Tunahakikisha kuwa tunaboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kutekeleza sera zinazochochea sekta binafsi yenye ushindani,” alisisitiza. “Hii ni pamoja na kurahisisha michakato ya usajili wa biashara, kupunguza vikwazo vya kisheria, na kuanzisha vituo vya kutolea huduma katika dirisha moja ili kupunguza urasimu na kupambana na rushwa.”
Aliweka wazi kuwa Tanzania inajipanga kuwa mchezaji muhimu katika masoko ya kikanda na kimataifa, kuvutia uwekezaji na kuchochea ukuaji.
Kwa upande wa maendeleo ya kijamii, Dkt. Mpango alielezea mafanikio muhimu katika maeneo kama usalama wa chakula, elimu, huduma za afya, na usawa wa kijinsia.
Alisema kuwa kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi kimefikia asilimia 97% kufikia mwaka 2022, upatikanaji wa huduma za afya umeimarika, na kuleta kupungua kwa vifo vya kina mama na watoto wachanga, na uwakilishi wa wanawake katika elimu na nafasi za uongozi umeongezeka.
“Sekta binafsi imekuwa na mchango muhimu katika mafanikio haya, na ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuendelea na juhudi zetu, kuchukua jukumu la uwajibikaji, na kuonyesha uzalendo katika kutekeleza majukumu yetu,” alisema. “Pamoja, tunaweza kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.”
Dkt. Mpango alisisitiza ahadi ya Serikali kuimarisha ushirikiano wa umma na sekta binafsi, ambao ni muhimu kwa kukuza maendeleo ya taifa na uchumi.
Katika hotuba yake, Santina Benson, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, alisema jukwaa hilo linajivunia hatua mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuitisha majukwa za kujadili maendeleo ya kiuchumi, kupitia sekta za viwanda na biashara.
“Miaka hii imekuwa ya mabadiliko makubwa kwa CEO Roundtable, kwani tumepiga hatua kubwa katika maeneo yetu muhimu ya kipaumbele na kuendelea kutumia jukwaa la CEOrt kuanzisha mijadala juu ya masuala muhimu kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi ya nchi,” alisema Benson.
Aliongeza kuwa CEOrt imeendelea kufanya juhudi za kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali kama vile nishati, mipango ya urithi wa biashara za familia, maendeleo ya rasilimali watu, fursa za usafirishaji na umuhimu wa uchambuzi wa data katika kukuza maendeleo ya Tanzania.
Katika sherehe hiyo, watu kadhaa mashuhuri walitunukiwa tuzo kwa michango yao ya kipekee kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania, akiwemo aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru.
Watu mbalimbali, wakiwemo Mabalozi, maofisa waandamizi wa Serikali na wadhamini mbalimbali, wakiwemo CRDB, NMB, Yas, Vodacom, Stanbic Bank, Pepsi, Tiper, KCB Bank, Aris, TCC, TPA, Exim Bank, GSM, Serengeti Breweries, Strategis na Hyatt Kilimanjaro walikuwa ni sehemu ya usiku huo maalum.