Mnamo mwezi Oktoba, Biden aliahirisha mpango wa kuitembelea Angola wakati Kimbunga Milton kilipokaribia kulifikia jimbo la Florida. Alifanya hivyo ili kusimamia mipango ya kukabiliana na janga hilo.
Katika ziara ya sasa, mara tu atakapotua mjini Luanda, atashughulikia ajenda kadhaa. Anatarajiwa kutia saini mikataba ya kijeshi, kisiasa na kiuchumi ikiwa ni ishara ya kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na Angola. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Claudio Silva anasema ziara hiyo ni mafanikio makubwa kwa Angola.
Soma zaidi:Rais Biden aanza ziara ya siku mbili nchini Angola
Kufanyika kwa ziara ya Biden, muda mfupi baada ya uchaguzi wa Marekani siyo jambo linalotokea kwa bahati mbaya na kutambuliwa kwa miradi ya ushirikiano kunaonekana kupewa kipaumbele
Angola ina miradi muhimu ya sasa na ya baadaye inayoihusisha Marekani iliyotoa mkopo kwa ajili ya ujenzi na uendeshaji wa mtambo wa kusafisha mafuta wa Soyo kaskazini mwa Angola. Pia ina mradi wa reli wa Lobito ambao ndiyo mkubwa zaidi. Mradi huo wa reli unaiunganisha bandari ya Lobito katika Pwani ya Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia yenye utajiri wa Madini.
Ushirikiano wa kijeshi kati ya Marekani na Angola wazidi kukua
Wakati ziara hiyo ya Biden ikitarajiwa kuimarisha zaidi uhusiano wa kijeshi, mwanasosholojia Paulo Ingles aliyewahi kufanya utafiti katika chuo cha jeshi cha Munich na Bayreuth anasema kwa sasa ushirikiano katika sekta hiyo kati ya Marekani na Angola umekua. Ingles anasema kuwa Marekani inapanga kujenga kambi ya kijeshi Kaskazini mwa Angola kwani hatua hiyo itaendana na maslahi ya kimkakati ya kijiografia ya Marekani.
Soma zaidi: Biden akutana na kiongozi wa Angola huku Marekani ikilenga kukabiliana na China barani Afrika
Mtaalamu wa diplomasia ya Kimataifa wa Angola Kinkinamo Tussamba ameiambia DW kuwa, kwa hakika ziara ya Biden nchini Angola ni tukio la Kihistoria lakini kwa bahati mbaya haiwezi kubadilisha maisha ya Waangola kuwa bora zaidi.
Tussamba anabainisha kuwa huenda ni kundi dogo la watu wenye hadhi ya juu wa nchini humo ndiyo pekee watakaonufaika na uwekezaji wa Marekani, kama ilivyokuwa kwa miradi mikubwa ya Wachina iliyofanywa Angola na si vijana wanaokabiliwa na changamoto kubwa ya ajira.