Samia asema atatafutwa mrithi wa Dk Ndugulile WHO

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile itaelekezwa kwa Mtanzania mwingine mwenye sifa.

Rais Samia amesema hayo leo Jumatatu Desemba 2, 2024 katika hafla ya kuaga mwili wa Dk Ndugulile, aliyekuwa mbunge wa Kigamboni iliyofanyika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Dk Ndugulile alifariki dunia Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu. Mwili wake utazikwa kesho Jumanne, katika makaburi ya Mwongozo, Kigamboni.

Alifikwa na mauti ikiwa imesalia miezi michache kwenda kuanza kutumikia nafasi yake mpya WHO Februari, 2025. Alichaguliwa kwenye nafasi hiyo Agosti 2024, akiweka rekodi ya kuwa Mtanzania na mwana Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kwanza.

Katika salamu zake, Rais Samia amesema nchi ilimpata mwakilishi: “Wanadamu tunapanga yetu, lakini Mungu anatupangia, Dk Ndugulile ameiweka nchi pazuri lakini Mungu amechukua kilicho chake.

“Tutaingia tena kwenye mashindano tutatafuta Mtanzania mwenye sifa anayeweza kushindana na ulimwengu, tutaingia tena na tutaweka mtu mwenye sifa ileile kutuwakilisha,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema amepokea salamu nyingi za pole kutoka ndani na nje ya nchi, huku akiwashukuru viongozi waliofika kumuaga Dk Ndugulile hasa kutoka WHO.

“Mengi yamesemwa na tumeyasikia mengi katika mchango wake kwa nchi na duniani, uongozi wake, mchango wake katika taaluma ya tiba na siasa hasa kwa wananchi wa Kigamboni,” amesema.

Rais Samia amesema wajibu wa nchi ni kuimarisha uwakilishi wa Tanzania ndani ya nchi na Afrika hasa katika Shirika la Afya Duniani.

“Katika kuimarisha ushiriki wetu ni azma ya Serikali kuhakikisha sasa Watanzania wabobezi tunaweka kila aina ya nguvu watuwakilishe katika fani za kimataifa.

“Dk Ndugulile alikuwa mwanamajumuia kutokana na imani yake ndicho kilichomsukuma akagombee nafasi hiyo na Serikali ikamuunga mkono tukajaliwa kupata nafasi ile, mwanadamu hupati unachokipata unapata majaliwa,” amesema Samia.

Awali, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani WHO Kanda ya Afrika, Dk Matshidiso Moeti amesema Dk Ndugulile alikuwa na maono ya kufanya mageuzi makubwa katika shirika hilo.

Amesema tangu aliposhinda nafasi yake Agosti 2024, alishaanza kuandaa namna atakavyoliongoza Bara la Afrika katika nafasi yake mpya.

Amesema kupitia nafasi yake, tayari alianza kuandaa mambo kadhaa kwa kushirikiana na ofisi yake.

“Alitutembelea mwezi uliopita na alizungumza nasi mambo mengi kuhusu kile atakachokuja kukifanya na mageuzi anayoyataka. Tulijiandaa kufanya vizuri zaidi katika uongozi wake na wengi walijiandaa wakiwemo wafanyakazi na wengine ambao tumekuwa tukifanya nao kazi,” amesema Dk Moeti.

Kwa mujibu wa Dk Moeti, taarifa za kifo cha Dk Ndugulile ziliwashtua si tu ofisi ya WHO Afrika iliyopo Brazzaville DRC Congo, bali katika ofisi kuu za WHO Geneva, Uswisi.

“Leo nimeongozana na viongozi wengi, wakiwemo wakurugenzi wa WHO Afrika, mawaziri wa afya na washirika wengine.

“Baada ya taarifa za kifo, nilipokea meseji nyingi na simu kutoka nchi mbalimbali duniani. Machozi ni ya wengi kuondoka kwa Dk Ndugulile na wengi wameumia kuona kiongozi mwenye maono anaondoka bila kutumikia nafasi yake,” amesema Dk Moeti.

Amesema wakati huu wa majonzi ni kubaki kushangilia maisha yake, kwani ni mtu aliyekuwa na uwezo mkubwa katika afya ya umma na waliamini uwezo wake angeutumia zaidi katika sera za kiafya kuhakikisha analeta mabadiliko Afrika.

Dk Moeti amesema kifo cha Dk Ndugulile kimemtonesha kidonda cha Dk Mwele Malecela.

“Kwa niaba ya WHO natoka pole kwa Tanzania na Serikali ya Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Jamhuri ya Tanzania, watoto na mke wake,” amesema Dk Moeti.

Chama cha Madaktari Wanafunzi Tanzania na (Tamsa) na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) wamesema wataenzi mema aliyoyaacha Dk Ndugulile.

Akisoma salamu za Tamsa, Makamu wa rais wa chama hicho, Dua Almas amesema walizipokea taarifa za kifo cha cha mlezi wao Dk Ndugulile kwa masononekana na wanahisi wamepoteza kioo kuelekea kutimiza ndoto zao.

“Dk Ndugulile alikuwa mwanachama hai na alihudumu nafasi mbalimbali katika chama chetu, ikiwemo katibu mkuu na alipohitimu masomo aliendelea kuwa mwanachama na kutoa michango yake, alikuwa anatupa moyo siku moja tunaweza kufanikiwa zaidi yake,” amesema Almas.

Amesema Dk Ndugulile alikubali kuwa mlezi wa chama hicho tangu 2023 na alikuwa msaada mkubwa, hivo kifo chake ni pigo kwao.

Kwa upande wake, rais mteule wa MAT, Dk Alex Msyoka amesema Dk Ndugulile alikuwa daktari bingwa wa afya ya jamii pamoja na kwamba alikuwa mwanasiasa, hakuweka kando taaluma yake.

“Tutamkumbuka kwa mambo mengi, ikiwemo alipokuwa mstari wa mbele kukabiliana na ugonjwa wa Uviko 19, na alikuwa kinara kwenye kupambana ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi,” amesema Dk Msyoka.

Related Posts