Simba, Pamba zatozwa faini mamilioni

Klabu ya soka ya Pamba Jiji ya Mwanza imetozwa faini ya Sh5 milioni kwa kosa la maofisa wake kuingilia mazoezi ya klabu ya Simba siku moja kabla ya tarehe ya mchezo tajwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Maofisa wa Pamba walionekana ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba katika muda ambao kikanuni ulikuwa ni wa klabu ya Simba kufanya mazoezi, jambo ambalo lilisababisha vurugu baada ya walinzi wa klabu ya Simba kulazimisha maofisa hao watoke nje. Tukio hilo liliathiri utekelezaji wa matakwa ya kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.

Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo ikizingatiwa kuwa hili ni kosa la kujirudia kwa klabu ya Pamba wakifanya hivyo pia katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons ya jijini Mbeya.

Wakati huo huo, klabu ya soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh5 milioni kwa kosa la walinzi wake kufanya vurugu na kuvunja mlango na kioo cha dirisha la ofisi ya Meneja Msaidizi wa Uwanja wa CCM Kirumba wakilazimisha maofisa wa Pamba na wa uwanja waliokuwa ndani ya ofisi hiyo kutoka nje wakati klabu ya Simba ikiendelea na mazoezi.

Klabu ya Simba italazimika kulipa gharama za uharibifu uliofanywa na walinzi hao kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Pamba ilicheza na Simba Novemba 22, 2024 ambapo mchezo huo ulimalizka kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 la penalti ya Leonel Ateba huku ukitawaliwa na matukio mengi nje ya uwanja.

Related Posts