MSIMU wa 17 wa Wiki ya Maonesho na tuzo za Mitindo za Swahili (Swahili Fashion Week and Award 2024 ) imezinduzliwa ambapo ambapo wabunifu wa Mitindo 40 kutoka nchini na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki kuonesha kazi zao.
Maonesho hayo yanatarajiwa kufanyika Desemba 6 hadi 8, 2024 katika ukumbi wa Parthenon Hall Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Swahili Fashion Week 2024 leo Desemba 2, 2024 Jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Jukwaa hilo, Mustafa Hassanali ambaye pia ni Mbunifu mkongwe amesema mwaka huu kauli mbiu ya Jukwaa hilo ni ‘Nishati Safi Ya Kupikia’ kwa lengo la kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi.”Huu ni msimu wa 17 tangu kuanzisha kwa jukwaa hili na mwaka huu litashirikisha wabunifu 40 kutoka Tanzania na nje ya mipaka kuonyesha kazi zao,” Amesema Hassanali.
Aidha amesema Swahili Fashion Week 2024 itatoa nafasi kwa wabunifu wa kimazingira kwenye mitindo ambapo wabunifu wataonesha makusanyo yanayojumisha malighafi rafiki wa mazingira, mbinu za uzalishaji wa kimaadili na miundo ya mzunguko, wakisisitiza dhana ya “Made in Afrika”.
Nae Mkurugenzi wa Ukuzaji na Maendeleo ya Sanaa, Edward Buganga amesema sekta ya mitindo hivi sasa imepiga hatua kutokana na wabunifu wengi kufanya vizuri na kukuza pato lao na la nchi kwa ujumla.
“Sekta ya mitindo ni kazi ambayo inashirikisha nchi za Afrika na kuweka lugha ya kiswahili mbele, pia inaongeza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi,” Amesema Buganga.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na waandaji wa jukwaa la Swahili Fashion Week kwa lengo la kukuza tasnia ya mitindo nchini na sekta hiyo izidi kupiga hatua.
“Tutaendelea kushirikiana nanyi katika hatua moja na nyingine katika kuhakikisha mitindo inaongeza pato la uchumi wa taifa na kutangaza nchi yetu,” Ameeleza Buganga.
Wabunifu ambao wataonyesha kazi zao ni Sliq Shedafa, Reen Fashion Flair, Kai Zuri by Sristri Bosco, Zawadi, Asili by Naliaka, Katty Collection, Fiderine’s, Mkwandule’Son, Blackcherry, Nyuzi CAD, Zuh Fashion, Jojo African Designs na Blackcherry.