Dar es Salaam. Watoto wa alikuwa mbunge wa Kigamboni (CCM), marehemu Dk Faustine Ndugulile (55) wamemzungumzia baba yao namna walivyoishi pamoja, huku wakikumbuka jinsi alivyokuwa karibu na familia hata katikati ya ratiba zake ngumu.
Ukaribu huo ulimfanya Dk Ndugulile aliyekuwa Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika kutokuwa tayari kukosa sherehe yoyote ya familia, ikiwemo siku za kuzaliwa na mahafali.
Watoto hao Martha na Melvin wamesema hayo leo Jumatatu, Desemba 2, 2024 katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam kwenye shughuli ya kuaga mwili wa baba yao aliyefariki dunia Novemba 27, 2024 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.
Walipopata nafasi ya kuzungumza mbele ya waombolezaji mbalimbali kutoka nje na ndani ya nchi, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, watoto hao wawili pekee wa Dk Ndugulile wamemwelezea jinsi walivyoishi na baba yao na kukumbuka yale aliyekuwa akipenda, ikiwemo muziki.
Aliyeanza kuzungumza ni mtoto wake wa kwanza, Martha aliyesema amepoteza mwanga wake, nguzo yake, shujaa wake na kielelezo cha mtu aliyekuwa akimtazama katika vitu anavyofanya.
“Ninapomzungumzia baba yangu, namzungumzia kama mtu aliyekuwa akitenga muda kwa ajili ya familia yake, hata akiwa na ratiba ngumu. Hakuwahi kukosa sherehe za kuzaliwa, matukio ya kifamilia au mahafali. Alikuwa mtu anayependa familia na aliyeweka familia kwanza kila wakati,” amesema Martha.
Amesema baba yake pia ndiye aliyemfanya kupenda muziki mzuri na anakumbuka namna alivyokuwa akipenda wimbo wa ‘Hapo vipi’ ulioimbwa na Joseph Haule maarufu Profesa Jay na mara zote walikuwa wakiimba na kucheza pamoja.
“Hizi ni kumbukumbu ambazo zitakuwa zikiishi kwangu. Pia alinitaka kuweka juhudi zote katika kila ninachokifanya kama yeye alivyojitoa kikamilifu katika kila jambo, hakuwahi kuridhika na chochote kilicho chini ya kile alichostahili. Kwa somo hili, natamani siku moja kufikia hatua kubwa kama alivyofanya,” amesema Martha.
Amesema urithi wa baba yake haupo tu katika masomo, bali pia kwa watu wengi aliowainua njiani kama kiongozi, mwanajamii na mtu aliyewahamasisha wengine.
Amesema baba yake alikuwa mtu wa watu, daima alitabasamu na kutoa msaada kwa wale waliomtegemea au waliokuwa na mahitaji.
Amesema baba yake pia ndiye aliyetengeneza historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kugombea nafasi ya Mkurugenzi mwa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika na kufanikiwa, huku akisema hilo limemfundisha kutoogopa kuota ndoto kubwa na kujenga.
“Kwa bahati mbaya ametuacha kabla hajaanza rasmi kuitumikia nafasi hiyo. Kama mwanadiplomasia katika nafasi yake mpya, nilikuwa nikimfanyia utani mara kwa mara kuhusu kuboresha Kifaransa chake, naye alikuwa akicheka. Utani huu hata ukanifanya nianze darasa la Kifaransa,” amesema.
Amesema ingawa anahisi mzigo mzito juu ya msiba huo, lakini anajipa faraja akijua roho ya baba yake itaendelea kuwa nao daima na ataendelea kuwaongoza kama alivyofanya akiwa hai.
Baadaye alipopewa nafasi ya kuzungumza, Melvin ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita amesema baba yake alikuwa jasiri, mpenda watu, mkarimu, mwenye akili huku kwake atabaki kuwa baba bora zaidi.
“Namshukuru Mungu kwa kunipa baba na nitakuwa naye moyoni hata katika kutokuwepo kwake, ingawa hayupo nasi kimwili, nitampenda zaidi. Kwa hakika, nikianza kutaja kila kitu alichonifanyia na familia yetu katika miaka yangu 18 ya maisha, sidhani kama nitaweza kumaliza.
“Najua kwa hakika baba yangu alikuwa kielelezo cha mafanikio mengi nchini Tanzania, Afrika na duniani. Aliweka rekodi ambazo hazijavunjwa. Alijijengea urithi wake mwenyewe,” amesema.