Wasira: Tatizo la maadili bado kubwa nchini

Unguja. Mwanasiasa mkongwe nchini, Stephen Wasira amesema Taifa linakabiliwa na tatizo kubwa la mmomonyoko wa maadili.

Amesema tatizo hilo pia lipo kwa baadhi ya viongozi wa kitaifa na kisiasa, hivyo kuna haja ya somo la maadili kupewa kipaumbele katika taasisi za elimu ya juu.

Wasira ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar, ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 2, 2024 alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya tisa ya chuo hicho.

 “Taifa hili kwa sasa lina tatizo kubwa la maadili, mmomonyoko umekuwa mkubwa, kwa hiyo ndio maana sisi chuo tumeongeza somo la maadili na uongozi ili kukabiliana na tatizo hili,” amesema Wasira. 

Ametumia fursa hiyo kuwataka wahitimu katika chuo hicho kubeba taswira halisi ya jina la chuo kama alivyokuwa yeye akisema, maadili yake hayakuwa na shaka na uongozi uliotukuka.

“Nendeni mkawe mabalozi wazuri wa maadili mjitofauitishe na watu wengine ili kubeba taswira nzima ya Mwalimu Nyerere, tunajua alivyokuwa amebeba maadili na uongozi bora, tukifanya hivyo, tutakuwa tumemtendea haki na kubeba jina lake,” amesema Wasira.

Amesema kutokana na mwitikio wa wanafunzi katika chuo hicho ikilinganishwa na walivyoanza miaka 10 iliyopita, ipo haja ya kupanua wigo wa kuongeza programu zingine kwa kuwa, jamii imeamua kuwapeleka wanafunzi kusoma.

 Hata hivyo, Wasira ameonesha kukoshwa na idadi kubwa ya wahitimu wanawake akisema ni ishara ya kuwapo kwa mabadiliko kwenye jamii hususani ya Kizanzibari na kuona kuwa elimu ni kwa kila mmoja sio tu kwa wanaume pekee.

Mkuu wa chuo hicho, Profesa Harun Mapesa amesema kwa sasa chuo kimeingiza katika mitalaa yake somo la maadili na uongozi ili kukabiliana na changamoto hiyo inayoonekana kuwa tatizo kwenye jamii.

Amewataka wahitimu kutumia fursa hiyo kujiendeleza zaidi badala ya kubweteka na kiwango walichokipata huku wakionyesha maarifa yao katika kutatua changamoto za jamii zinazowakabili.

Licha ya kutaja mafanikio ya chuo hicho kilichoanza mwaka 2014 kikiwa na watumishi wanne na sasa wapo 74, amesema bado kinakabiliwa na upungufu wa watumishi.

Ameomba waendelee kuzingatiwa ili kuendana na matakwa ya kitaaluma na wingi wa wanafunzi. 

“Kuweni mabalozi, tatueni changamoto za kijamii ili kuonesha utofauti kati yenu na jamii kusaidia kumaliza shida zao,” amesema Profesa Mapesa. 

Amesema chuo kinaendelea na ujenzi wa bweni litakalokuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 1,534, kati ya hao wanawake ni 768 na wanaume 766. 

Baadhi ya wahitimu wamesema ni wakati wa kuonyesha mabadiliko kwenye jamii na kuhakikisha wanashughulikia changamoto zinazoikumba badala ya wao kuwa sehemu ya changamoto.

Mhitimu wa shahada ya elimu katika jiografia na historia, Scolastika Mbuya amesema wanapaswa kujitofautisha katika kutatua changamoto za jamii badala ya kuendelea kuwa sehemu ya changamoto. 

“Yapo mengi tumejifunza, ni wakati sasa wa kwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo, lazima kuangalia mambo yanayoweza kuleta mabadiliko sisi binafsi, jamii inayotuzunguka na hata Taifa letu,” amesema mhitimu katika stashahada ya maendeleo ya jamii, Said Abeid Haji.

Related Posts