Dar es Salaam. Kupunguza unyanyapaa, kutokubalika kwenye uongozi, kutengwa na jamii na kuuawa kwa imani potofu, ni miongoni mwa changamoto chache kati ya nyingi ambazo zinatajwa na watu wenye ulemavu kudidimiza utu na ustawi wao.
Mfano wa matukio ya ukatili ni lile la mtoto Asimwe Novart aliyeuawa kwa kile kinachodaiwa ni kwa sababu ya imani za kishirikina.
Pia, matukio ya unyanyapaa katika jamii, kukosa ajira kutokana na ulemavu wao licha ya kuwa wana uwezo wa kufanya kazi, ni vitu ambavyo kundi hilo linatamani vikomeshwe ili nao wapate fursa kama ilivyo kwa wengine.
Ili kukabiliana na changamoto hizo na nyinginezo, watu wenye ulemavu wamekuja na mipango miwili ambayo ni pamoja na mkakati wa taifa wa teknolojia saidizi na mwingine ni mpango kazi wa haki na ustawi kwa wenye ualbino.
Inaelezwa kuwa mpango mkakati hiyo miwili huenda ikawa kichocheo cha kundi hilo kuthaminiwa kama ilivyo kwa wengine.
Katibu wa Shirikisho la Watu wenye ulemavu Tanzania (Shivyawata), Jonas Lubago amesema kundi hilo linahitaji kutambuliwa mchango wao katika jamii na kukuza uongozi wa watu wenye ulemavu sambamba na kuondoa unyanyapaa dhidi yao ikiwamo wa kutengwa katika jamii.
Amesema knachofanywa na watu wenye ulemavu, kinapaswa kuonekana sambamba na uwezo wao utambulike na jamii nzima.
“Hata mwenye mtoto ambaye ana ulemavu anamficha, anapaswa kuondoa ile dhana kwamba huo ni msalaba wake, kuwa mlemavu sio msalaba,” amesema mwenyekiti huyo.
Anasema mikakati waliyokuja nayo hivi sasa ni mpango wa teknolojia saidizi kwa watu wenye ulemavu, wakilenga kuongeza fursa na kuwapunguzua adha watu hao kwa kupatia vifaa saidizi.
“Teknolojia inamsaidia mlemavu kupunguza changamoto za ulemavu, iwe kwa kupata viti mwendo na vifaa saidizi vingine. Mfano mwenye uoni hafifu, teknolojia itamsaidia kupata fimbo ya kutembelea, wenye uziwi watapata mashine za kuwasaidia kusikia na vifaa saidizi vingine kwa wenye ulemavu tofauti,” amesema.
Lubago amesema awali upatikanaji wa vitu hivyo ulifanyika kiholela na ilichangia kuongeza changamoto huku akitolea mfano mtu mwenye ulemavu, alipatiwa kiti mwendo ambacho hakikuwa saizi yake.
“Sasa katika hali kama hii ni wazi kuwa mtu huyu hakusaidiwa, bali aliongezewa tatizo, lakini mkakati huu wa teknolojia unakwenda kutuondoa huko,” anasema Lubago.
Akizungumzia gharama za vifaa saidizi, amesema licha ya kuwa na gharama kubwa, lakini kupitia mpango huo, utachochea uzalishaji wa vifaa hivyo nchini ambavyo vitatengenezwa kulingana na mazingira yaliyopo na kwa bei rafiki kwa wahitaji kuimudu.
Lubago pia amewazungumzia watu wenye ulemavu wa ualbino kuwa mpango huo utasaidia kujenga uelewa na ulinzi wa maisha yao ili jamii hiyo iishi kwa amani kama watu wengine.
Kundi hilo limekuwa likipitia changamoto ikiwamo ya kuishi kwa mashaka na kuhofia kuuawa kwa fikra za imani potofu kwa baadhi ya jamii.
Changamoto ya ukosefu wa ajira kwa watu wenye ulemavu, huenda ikapungua baada ya kuanzishwa kwa jukwaa la ajira la kidigitali litakalokuwa na orodha ya watu wenye ulemavu katika fani mbalimbali ili kuwarahishia waajiri.
Jukwaa hilo lijulikanalo kama YoWDO Connect Portal limeanzishwa kwa ushirikiano wa mashirika ya watu wenye ulemavu na linasimamiwa na kuendeshwa na Shirika la Vijana Wenye Ulemavu (YoWDO).
Mkurugenzi wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali linalojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu (DOLASED), Wakili Gideon Mandesi anasema wanaamini kupitia jukwaa hilo, waajiri wataweza kuwapata watu wenye ulemavu ambao wanavigezo, sifa na ujuzi.
Mandesi amesema kuna madai ya waajiri kutowafahamu watu wenye ulemavu ambao wana vigezo, sifa na ujuzi wa kuajiliwa wanapatikanaje.
“Tunayaomba mashirika ya umma na binafsi kujisajili katika jukwaa la ajira la kidigitali kwa ajili ya kuwapata watu wenye ulemavu wenye vigezo na sifa za kuajiriwa,”amesema na kuongeza:
“Sheria ya wenye ulemavu ya mwaka 2010 kifungu cha 31(2) kinasema sehemu yenye ajira kuanzia wafanyakazi 20 na kuendelea, basi asilimia tatu ya wafanyakazi hao wanapaswa waajiriwe watu wenye, ulemavu lakini sheria hii haitekelezwi na hata serikali yenyewe haijaitimiza,” amesema Mandesi.
Pia amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan atoe vibali vya ajira kwa watu wenye ulemavu waliohitimu vyuo vya kati na vya juu ambao wako mitaani.
Wakizungumzia maadhimisho yao ya Siku ya Walemavu yenye kauli mbiu: ‘Kukuza uongozi wa watu wenye ulemavu kwa ajili ya mustakabali jumuishi na endelevu,’ baadhi ya viongozi wa vyama mbalimbali wameeleza matamanio yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa YoWDO, Rajabu Mpilimpili amesema kwa kuzingatia kauli mbili ya mwaka huu ‘kuongeza uongozi wa watu wenye ulemavu kwa mustakabali jumuishi na endelevu’ hivyo ameiomba Serikali kuweka jitihada za dhati kwa kutoa fursa za uongozi kwa watu hao Ili waweze kushiriki na kuongoza kikamilifu ikiwemo shughuli za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Mpilimpili amesema changamoto zingine zinazowakabili watu wenye ulemavu ni vikwazo kwa ushiriki wao katika fursa za kiongozi pamoja na mazingira yasiyo sikivu, ubaguzi na unyanyapa na mitazamo hasi kuhusu uongozi.
Kwa upande wa mjumbe wa Chama cha Wenye Ualbino Tanzania(Tas),Abdallah Bocheka amesema ukatili dhidi ya watu wenye ualbino bado unatishia usalama na utu wao, hivyo wameyaomba mashirika yanayotetea haki zao kuhakikisha wanaimarisha sheria.
Mwenyekiti wa chama cha wenye ualbino Tanzania (TAS), Godson Mollel amesema wanatamani changamoto zinazokwamisha utu na ustawi wao, zikomeshwe ikiwamo kuuawa na kukatwa viungo vyao kwa imani potofu.
Akitolea mfano kesi ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novart aliyeuawa na kunyofolewa viungo, Mollel amesema ni moja ya matukio ambayo yamekuwa yakiwatoa machozi.
“Tunatamani hatua kali ziwekwe dhidi ya watu wanaofanya haya kwa imani kwamba viungo vyetu vitawapa utajiri,” amesema.
Pia, amesema upatikanaji wa mafuta yao ambayo ni kinga dhidi ya mionzi ya jua inayowasababishia saratani ya ngozi, bado ni gharama kubwa na hayachukuliwi kama dawa bali yanaonekana ni vipodozi hivyo gharama yake hushindwa kumudu na wengi.
Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania (Chawata), Hamadi Komboza amesema mazingira rafiki ya ajira kwa kundi hilo ni jambo ambalo wanalitamani.
“Baadhi ya waajiri wana mitazamo hasi kutoa ajira, hili ni miongoni mwa mambo tunayoyatamani yaboreshwe tunapokwenda kuadhimisha siku hii,” amesema Komboza.
Hayo na mengine mengi ni sehemu ya mambo yatakayojadiliwa na kupatiwa ufumbuzi katika maadhimisho ya siku ya wenye ulemavu duniani ambayo kitaifa yanafanyika jijini Dar es Salaam kesho Jumanne Desemba 3, 2024.