Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa mpito wa Yas Tanzania, Jérôme Albou amesema jina la Yas na Mixx by Yas, ni matokeo ya ubunifu uliofanywa kupata kitu cha tofauti na kuja kivingine katika biashara.
Albou amesema miongoni mwa matarajio yao ni kuwa na huduma bora zinazohusu bidhaa zao zote.
“Tumekuwa na miaka 14 ya Tigo na sasa tupo katika Yas, jina hili limetokana na ubunifu wa hali ya juu ambao unaakisi huduma nzuri na zenye ubora zaidi,”amesema
Albou amesema hayo leo Jumatatu, Desemba 2, 2024 katika mahojiano maalumu na Kaimu Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Mpoki Thompson makao makuu ya Kampuni ya Yas Tanzania.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas, Angelica Pesha akizungumza katika mahojiano hayo amesema mtandao huo unatumia jina hilo kwa sababu huduma zao za kifedha zinahusisha mambo mengi na si kutuma na kupokea fedha pekee.
“Kwa sasa unaweza kupata zaidi ya kutuma na kupokea fedha kupitia bidhaa yetu, ndio maana tuna mikopo, akiba na vitu vingine ni kama tumechanganya vitu vingi ndani ya bidhaa yetu ndio maana tumeenda na neno mix.
“Wateja wetu tunaendelea kuwaambia kilichobadilika ni jina tu, kutoka Tigo pesa kwa sasa ni Mixx by Yass, ila huduma ni zilezile na bidhaa ni ileile,” amesema na kuongeza.
Kuhusu changamoto wanazozipitia katika mabadiliko ya jina, Angelica amesema: “Changamoto kubwa ni watu kutaka neno pesa, money au hela katika jina ambalo tunalo, lakini ndio ubunifu na tunaichukulia hiyo kama fursa, na kama kusingekuwa na mrejesho wa wateja wetu isingeleta maana.”
Akizungumzia mchakato wa mabadiliko ya jina hilo, Albou amesema Serikali ya Tanzania imesaidia kwa kiwango kikubwa katika kuukamilisha.
“Katika mabadiliko ya jina tumefanya kazi kwa karibu na kampuni mbalimbali binafsi, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), UCSAF…Kiukweli Rais Samia Suluhu Hassan na sera za Serikali yake zinawatunza wawekezaji,”amesema Albou.