Vietnam. Mahakama Kuu ya watu nchini Vietnam imethibitisha hukumu ya kifo ya mwanamke tajiri wa sekta ya mali isiyohamishika, Truong My Lan ambaye Aprili mwaka huu alihukumiwa kwa utapeli wa Dola 12 bilioni za Marekani (Sh31 trilioni).
Mahakama hiyo imeamua kuwa, hakuna sababu ya kupunguza adhabu ya kifo ya Truong My, japo imesema hukumu hiyo inaweza kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha ikiwa Lan atarejesha robo tatu ya fedha hizo.
Lan ambaye ni mwenyekiti wa Kampuni ya Van Thinh Phat Holdings Group Lan, alipatikana na hatia ya kutumia udanganyifu kuidhibiti Benki ya Kibiashara ya Saigon (SCB), moja ya benki kubwa za kibinafsi nchini humo.
Utapeli huo ulisababisha mgogoro mkubwa wa kifedha na kuathiri takribani watu 36,000, na kusababisha athari za kiuchumi zilizoelezwa kuwa hazikuwahi kutokea katika historia ya Vietnam.
Kwa mujibu wa tovuti ta Aljazeera leo Desemba 3, 2024, matokeo ya uhalifu wa Lan ni ya kipekee katika historia ya kesi za Mahakama, na kiasi cha fedha kilichoporwa ni kikubwa mno na hakiwezi kurejeshwa,”
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Serikali ya Vietnam, Lan alikiri makosa yake, kuonyesha majuto na kurejesha sehemu ya mali iliyoporwa, lakini upande wa mashtaka ulisisitiza kuwa, hatua hizo hazikutosha kupunguza hukumu kutokana na athari kubwa za kijamii, kiuchumi na kifedha zilizotokana na vitendo vyake.
Lan mwenye umri wa miaka 68 alikamatwa mwaka 2022 na alihukumiwa Aprili mwaka huu, kukamatwa kwake kulisababisha hofu kubwa miongoni mwa wateja wa SCB na hatimaye kusababisha watu wengi kutoa fedha zao katika benki hiyo.
Kesi hii imekuwa sehemu ya kampeni ya muda mrefu ya kupambana na ufisadi nchini Vietnam, inayojulikana kama “Blazing Furnace,” iliyoanza tangu mwaka 2022.
Kampeni hiyo imewalenga viongozi wakuu wa biashara, maofisa wa Serikali na wanachama wa vikosi vya usalama katika juhudi za kuimarisha uwajibikaji wa kifedha.
Vitendo vya Lan vilizua maandamano nchini Vietnam huku waathirika wengi wakipoteza akiba zao za maisha, utapeli huo unaokadiriwa kufikia asilimia 3 ya Pato la Taifa (GDP) la mwaka 2022 wa Vietnam umeathiri vibaya soko la kifedha na kuharibu imani ya umma katika taasisi za kifedha.
Serikali ya Vietnam imesisitiza kujitolea kwake kupambana na ufisadi kwa nguvu zote, ikionya kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria hukumu ya Truong My Lan inachukuliwa kama onyo kali kwa wengine katika sekta ya kifedha na biashara.
Kwa sasa Lan ana nafasi ya kuomba mapitio ya kesi yake kupitia taratibu za rufaa ya mwisho au kurudiwa kwa kesi lakini matarajio ya kupata afueni yanaonekana kuwa finyu.