Aliyeiba iPhone 16 Pro Max, apewa kifungo cha nje

Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, imemhukumu Justo William (31) kutumikia kifungo cha nje cha miezi minne baada ya kupatikana na hatia ya kuiba simu ya mkononi aina ya Iphone 16 Pro Max yenye thamani ya Sh7 milioni.

William ambaye ni dereva na mkazi wa Kitunda, jijini Dar es Salaam amehukumiwa kifungo hicho leo, Jumanne Desemba 3, 2024 na Hakimu Mkazi Scola Odela, baada ya kukiri shtaka lake.

Hakimu Odela amesema kwa kuwa mshtakiwa amekiri shtaka lake, Mahakama hiyo inamtia hatiani kama alivyoshtakiwa.

“Mshtakiwa umetiwa hatiani kama ulivyoshtakiwa na kwamba Mahakama inakuhukumu kifungo cha nje cha miezi minne,” amesema Hakimu Odela.

Mshtakiwa alivyopewa nafasi ya kujitetea ameomba apunguziwe adhabu kwa kuwa amekiri shtaka lake.

Hata hivyo, simu hiyo alirudishiwa mlalamikaji katika kesi hiyo, ambaye ni Katundu Rocky.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hili Januari 27, 2024 katika Barabara ya Morogoro na Indira Gandhi nje ya Hoteli ya Tiffan Diamond.

Siku hiyo, saa 12 asubuhi katika eneo hilo, mshtakiwa akiwa dereva wa gari aina Toyota Sienta aliiba simu ya mkononi aina ya Iphone 16 Pro Max yenye thamani ya Sh 7,020, 000 mali ya Katundu Rocky.

Mshtakiwa alidaiwa kuiba simu hiyo, huku akijua ni kosa kinyume cha sheria.

Related Posts