WAMAMA Malkia 15 waliojitoa na kujitolea katika kufanya majukumu makubwa ya kuendeleza kazi za Asasi za Kiraia nchini,wamepewa tuzo maalum kwa ajili ya kuwapongeza kwa kazi wanazofanya.
Tuzo hizo zimetolewa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) wakati wa muendelezo wa kuadhimisha siku 16 za uanaharakati dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Miongoni mwa Wamama hao ni pamoja na Malkia Prof.Penina Mlama ambaye amepewa Tuzo ya Malkia Muasisi wa Usawa wa Kijinsia katika Taasisi za Elimu ya Juu,Malkia Jaji Mstaafu Joaquine De Mello ambaye amepewa Tuzo ya Upendo,Sheriabna Harakati za Kujenga Uwezo,Malkia Wakili Tumaini Silaa ambaye yeye amepewa Tuzo za Malkia wa Haki za Kisheria kwa Wanawake, Malkia Wakili Elizabeth Maro Minde ambaye amepewa Tuzo ya kuvunja minyororo na Kusonga Mbele,Malkia Rebeca Gyumi ambaye amepewa Tuzo ya Kuwawezesha Wasichana kuandika upya hatma yao.
Wengine waliopewa Tuzo ni pamoja na Malkia Wakili Utti Mwang’amba ambaye apewa Tuzo ya Aangaza Njia Kuielekea Haki,Malkia Noelah Msuya Shawa ambaye alipewa Malkia wa Utetezi wa Elimu Jumuishi kwa watoto wenye Ulemavu, Malkia Vicky Ntetema yeye amepewa Tuzo ya Malkia ya Mwenye Njozi hadi Mwandishi Mtetezi mwenye Mvuto,Malkia Asha Aboud Mzee ambaye amepewa Tuzo ya Amulika njia kuelekea uwezeshwaji Zanzibar pamoja na Malkia Rose Njilo ambaye amepewa tuzo ya kukaidi giza kumulika Mabadiliko.
Akizungumza katika utoaji wa Tuzo hizo kwa Wamama 15, Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WILDAF),Wakili Anna Kulaya amesema wametoa Tuzo hizo kutokana na juhudi za wamama hao za dhati zilizoacha alama isiyofutika kwenye uwanda wa Asasi za Kiraia.
Amesema miongoni mwa alama ambazo wamama hao walizoacha ni pamoja na msukumo wa usawa wa kijinsia kwenye taasisi za Elimu ya Juu nchini,kuchochea mabadiliko katika sekta ya Sheria,Ulinzi wa haki za watu wenye ulemavu, kuongeza ujuzi wa wanawake kwenye uchumi na kutikisa mipaka iliyokuwepo kwenye tasnia ya Habari.
“Safari ya wanawake hao inaonyesha matokeo ya aina mbalimbali waliyowezesha kwenye jamii na hasa kwenye duru la Asasi za Kiraia Tanzania na ulimwenguni kote,hivyo WiLDAF imetoa tuzo hizo kama shukrani kwa kazi kubwa na nzuri walizozifanya,”amesema.
Akipokea Tuzo yake mmoja wa wamama hao Prof.Penina Mlama amesema wanashukuru kwa shirika hilo kwa kuwapatia tuzo na kuwatambua wakinamama ambao wamefanya kazi za kuendeleza jamii kwa namna moja au nyingine.
Amesema katika jamii kuna watu ambao wanapambana sana ilikufanya hali za watu wale ambao wanaonewa kuwa nzuri zaidi.
“Tuzo hizi cha muhimu ni kutambua kazi walizozifanya inawatia moyo sio tu waliopokea tuzo na wale wengine ambao kwa namna moja au nyingine wanashughulika kwa kufanya mambo maisha ya watu yawe bora zaidi,”amesema na kuongeza
“Kwa wamama wanaochipukia waone tuzo hizi kama ni alama ya wao nao kuleta mabadiliko katika kuwapambania watu ambao wanahitaji msaada wao,”amesema.
Wamama wengine waliopewa Tuzo hizo ni Malkia Jane Magigita ambaye amepewa Tuzo ya kukuwawezesha wanawake wa Masokoni Tanzania, Malkia Fatma Aloo ambaye amepewa Tuzo ya Nyota Mpambania Mabadiliko,Malkia Shamshad Rehmatullah ambaye yeye amepewa tuzo ya Wakili Shupavu,Malkia Fortunata Manyeresa ambaye amepewa Tuzo ya Malkia wa Usawa wa Kijinsia na Uthibati wa Hali ya hewa pamoja na Malkia Maimuna Kanyamala ambaye amepewa Tuzo ya Nguvu isiyozuilika katika kujengea wanawake uwezo.
Mwisho