CHUO KIKUU cha Lead Impact cha nchini Marekani, kinatarajia kutunukuu Shahada ya Udaktari wa Heshima kwa Watanzania wanne mwaka huu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Chuo hicho ambacho kimekuwa kikiwatunukia watu wa kada mbalimbali Udaktari wa Hashima, kinatarajia kutoa shahada hiyo Desemba saba mwaka huu.
Akizungumza na Gazeti hili jana, Mratibu Mkuu wa Chuo hicho nchini, Profesa Peter Rashid Abubakar, aliwataja watanzania waliokwisha kamilisha taratibu zote zinazotakiwa kuwa ni pamoja na CPA Yona Malundo.
CPA Malundo ni mmiliki wa kampuni ya Y H Malundo&Co, inayojishughulisha na Uhasibu, Ukaguzi wa Hesabu, Ushauri wa Kodi na Menejimenti ya fedha.
Kupitia kampuni yake, CPA Malundo amepata heshima hiyo kutokana na namna inavyoendesha shughuli zake kwa usahihi, kuzingatia maadili na ufanisi mkubwa.
Ufanisi wa kampuni hiyo, ndiyo umeiwezesha kufanyakazi na ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa muda wa miaka kumi.
Kwa mujibu wa Profesa Peter, mbali na CPA Malundo, wengine watakaopata shahada hiyo ya Udaktari wa Heshima ni Christine Mbelwa, Emmanuel Paul na Robert Mbelwa.
Akizungumza na Gazeti hili jana, Profesa Peter, alisema chuo hicho maarufu ulimwenguni, kinatunukua Udaktari wa Heshima kwa watu wa kada mbalimbali kulingana na sifa na mchango wa mtu anaoutoa katika jamii.
“Hiki chuo ni maarufu sana na kiko nchini Marekani, kinatunuku Udaktari wa Heshima kuendana na CV ya mtu na mchango wake kwa jamii na taifa kwa ujumla. Tayari tumeshatoa shahada za Udaktari wa Heshima kwa viongozi mbalimbali hapa nchini,” alisema.
Aliongeza kuwa chuo hicho kimekuwa kikitoa shahada hiyo kwa wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi wa dini na kina mpango wa kuanzisha tawi lake hapa nchini.
Hata hivyo alisema kuwa ofisi yake inaendelea kufanya mawasiliano na Makao Makuu ya Chuo hicho nchini Marekan ili kupata idadi kamili ya watakaotunukiwa pamoja na tarehe ya mwisho kama hakuna mabadiliko.