Moshi. Wakati mabalozi tisa wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani wakitarajia kuwaongoza Watanzania 300 kupanda Mlima Kilimanjaro, kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk Christopher Timbuka, amesema kama mazingira hayatatunzwa, kuna hatari ya barafu iliyoko kwenye mlima huo kuyeyuka.
Hivyo ametoa rai kwa wakazi wanaouzunguka mlima huo kutunza mazingira ili kuokoa barafu hiyo.
Wapanda mlima hao wanaopanda kupitia Kampeni ya Twenzetu kileleni, ambayo ni msimu wa nne, watatumia njia tatu za kupandia mlima huo, ambazo ni Lemosho walioanza safari leo Desemba 3, Machame wanaoanza safari Desemba 4 na njia ya Marangu wataanza safari Desemba 5, 2024.
Akizungumza leo Jumanne Desemba 3, 2024 wakati akiwaaga wapanda mlima 33 kupitia njia ya Lemosho, Dk Timbuka amesema mabadiliko ya tabianchi yameuathiri Mlima kilimanjaro na kufanya barafu yake kupungua mwaka hadi mwaka.
Amesema kutokana na hali hiyo, hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa ili kutunza uoto wa asili na kuzuia uharibifu wa mazingira.
“Sote tunatambua kuwa, maeneo mengi ya nchi yetu yameathirika na mabadiliko ya tabianchi, na uharibifu huu unafanywa na binadamu. Miongoni mwa maeneo yaliyoathirika sana na hali hiyo ni Mlima Kilimanjaro ambao tumeshuhudia barafu yake ikiendelea kupungua mwaka hadi mwaka,” amesema Dk Timbuka.
“Katika kupanda mlima huu tunaongozwa na kauli mbiu isemayo, “stawisha uoto wa asili Tanzania, okoa barafu ya Mlima Kilimanjaro,” nitoe rai kwa Watanzania kuacha vitendo vinavyochangia kuharibu mzingira lakini pia kurejesha uoto wa asili katika maeneo yetu ili kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabia nchi ili barafu hiyo iendelee kuwepo.”
Mkuu huyo wa wilaya amesema mlima Kilimanjaro umebeba historia kubwa ndani na nje ya Tanzania, hivyo unapaswa kuendelea kutunzwa vema.
Dk Timbuka amewaasa pia wapanda mlima huo kuwa hayo si mashindano bali waupande taratibu ili lengo la kufika kileleni litimie.
Awali, akizungumza kwenye hafla hiyo, Kamishina wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Betrita James amesema katika kampeni hiyo msimu wa nne 2024, zaidi ya Watanzania 300 wamejiandikisha kuupanda Mlima kilimanjaro kwa ajili ya kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika.
Amesema miongoni mwa wanaopanda mlima huo wapo mabalozi tisa, wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani.
“Lengo la kupanda Mlima Kilimanjaro kila mwaka ni kuadhimisha siku ya Uhuru wa Tanganyika, tunataka tuendelee kuwa wamoja na tuenzi yale ambayo tuliachiwa na waasisi wetu,” amesema James.
Amesema tangu waanzishe kampeni hiyo ya Twenzetu kileleni, wageni wanaojiandikisha kupanda mlima huo wanaongezeka mwaka hadi mwaka.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Africans Cenic, Nsimbo Natai amesema katika njia hiyo ya Lemosho, itawachukua siku saba kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro huku uwezekano wa kufika ukiwa ni mkubwa zaidi ukilinganisha na njia nyingine.
Amesema kampuni hiyo imeendelea kuwekeza katika kuitangaza njia hiyo ili watalii wengi waitumie kupanda mlima huo mrefu barani Afrika.
Ametumia pia nafasi hiyo, kuwaasa Watanzania kujenga utamaduni wa kupanda mlima huo kupitia njia hiyo ili kujionea mandhari tofauti tofauti za Mlima Kilimanjaro.