Dk Ndugulile alivyohitimisha safari yake duniani ya siku 20,336

Dar es Salaam. Safari ya mwisho hapa duniani ya Dk Faustine Ndugulile ya siku 20,336 imehitimishwa kwa mwili wake kuzikwa katika makaburi ya Mwongozo, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Dk Ndugulile aliyezaliwa Machi 31, 1969 alifikwa na mauti Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa kwa matibabu. Amezikwa leo Jumanne, Desemba 3, 2024. Tangu kuzaliwa kwake hadi amezikwa ni sawa na siku 20,336 ama miaka 55 na miezi minane.

Safari hiyo ya mwisho ya aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni (CCM) na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika imehudhuliwa na waombolezaji mbalimbali wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Dk Ndugulile ameacha watoto wawili, Martha na Melvin. Martha ni daktari, Melvin ni mwanafunzi wa kidato cha sita akisoma masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia pamoja na mjane wa Dk Ndugulile, Magdalena Lyimo ambaye naye ni daktari.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi akitoa heshima za mwisho kwenye kaburi la aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile leo Jumanne Desemba 3, 2024 Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Mbali na Majaliwa, wengine waliokuwapo ni Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, mawaziri William Lukuvi (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama (Afya) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Dennis Londo na wakuu wa mikoa, Albert Chalamila wa Dar es Salaam na Paul Makonda wa Arusha.

Msafari wenye gari lililobeba mwili wa Dk Ndugulile uliwasili alasiri eneo la makaburi na kukuta taratibu zote zimekamilika pamoja na viongozi wote wamefika, wakati jeneza likiingizwa makaburi watoto wake walitanguliwa Martha aliyeshika msalaba na Melvin alibeba shada la maua.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akiweka shada la maua kwenye kaburi la aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile leo Jumanne Desemba 3, 2024 Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Kutoka gari lililokuwa limesimama hadi karibu na kaburi zilitandikwa nguo (vitenge na khanga) chini na waliokuwa wamebeba jeneza la Dk Ndugulile lililokuwa limefunikwa na bendera ya Bunge walipita juu yake.

Haikuwa rahisi pale sanduku lenye mwili wa ndugu, jamaa na rafiki wa Dk Ndugulile lilipoanza kushushwa katika makazi yake ya milele huku wanae, Martha, Melvin, mama yao, Dk Magdalena waliokuwa karibu na kaburi wakiwa hawamini kinachotokea.

Sanduku lilipoanza kushushwa kwenye kaburi hilo na watoto, ndugu na wapambe wa Bunge, waombolezaji waliojitokeza kwenye msafara huo wakiwa na nyuso za majonzi walikuwa wakilipungia mikono ishara ya kumuaga.

Wakati wote jeneza likishushwa, mjane wa Dk Ndugulile, watoto na ndugu waliweka mikono yao juu ya jeneza hadi liliposhuka huku mama mzazi wa mwanasiasa huyo akionekana akinyoosha mkono wa kuaga na mwanaye.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda akiweka shada la maua kwenye kaburi la aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile leo Jumanne Desemba 3, 2024 Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Kengera ilipigwa na mtumishi wa ibada hiyo ya mazishi iliyoongozwa na Padri Piere Kasongo. Wimbo wa mazishi uliimbwa na wana kwaya walioipamba safari hiyo ya mwisho ya Dk Ndugulile.

Sehemu ya wimbo huo uliimbwa hivyi: Nimekufa leo, kesho ni zamu yako (ona) ona vema nilivyowekwa humu, na nilivyoacha mali na jamaa nilitoka uchi tumboni mwa mamangu, narudia uchi, katika tumbo la nchi, sanda moja hilo ni vazi langu, wameninyang’anya hata senti moja.

Nifunike vema na hilo jembe lako, nalitangatanga, katika ulimwengu, basi leo kiburi kimekwisha, kumbe dunia hii ni mti mkavu. Nyumba yangu leo ni shimo udongoni, hakuna mlango, hakuna madirisha, kitanda changu na blanketi langu, ni udongo mzito wanielemea.”

Kaburi lake lilianza kupambwa mashada na Padri Kasongo akifuatiwa mke wa marehemu, Dk Magdalena kisha mama mzazi wa Dk Ndugulile (jina halikuweza kupatikana). Wakafuatia watoto Martha na Melvin na wakafuatia viongozi, mawaziri, wabunge na wengine.

Related Posts