Biden amewasili Luanda akilakiwa kwa vifijo na maelfu ya raia wa Angola na katika ziara hiyo atajikita katika mradi mkubwa wa reli unaoungwa mkono na Marekani ulio na lengo la kukabiliana na ushawishi wa China katika bara la Afrika lililo na zaidi ya watu bilioni 1.4.
Mradi huo wa reli wa Lobito Corridor utakaoshuhudia kuimarishwa kwa reli inayopitia Zambia, Kongo na Angola unalenga kuendeleza uwepo wa Marekani katika eneo hilo lililo na madini muhimu yanayotumika katika betri za magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki na nishati safi ya teknolojia.
Ziara ya Biden kusukumwa mbele mara kadha
Ziara hii ya Biden inakuja wiki chache kabla Donald Trump kuchukua mamlaka mnamo Januari 20 na kwa ziara hii anatimiza ahadi yake ya kuzuru nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.
Biden atasafiri katika mji wa bandari wa Lobito ambapo atautazama mradi huo wa reli. Kulingana na maafisa wa White House, atatangaza mambo mapya kuhusiana na afya, kilimo biashara na usalama.
Biden alitarajiwa kuizuru Afrika mwaka jana baada ya kuufufua mkutano wa kilele wa Marekani na Afrika mnamo Disemba 2022. Ziara hiyo iliahirishwa hadi mwaka 2024 na ikacheleweshwa zaidi kwasababu ya Kimbunga Milton, jambo lililotilia mkazo kauli ya baadhi ya Waafrika kwamba bara lao bado halipewi kipau mbele na Marekani.
Rais wa mwisho wa Marekani kufanya ziara katika mataifa ya kusini mwa Jangwa la Sahara alikuwa Barack Obama mwaka 2015. Mwaka 2022, Biden alihudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira nchini Misri, kaskazini mwa Afrika.
Madini ndilo eneo muhimu ambalo Marekani na China wanashindania na China tayari imeshikilia madini muhimu ya bara la Afrika.
Je, mradi wa Lobito utaendelea chini ya Trump?
Kwa miaka, Marekani imekuwa ikijenga mahusiano barani Afrika kupitia biashara, usalama na misaada ya kiutu. Ila sasa hiyo reli ya kilomita 1,300 ni mkakati mpya na kwa kiasi fulani inawiana na ule mkakati wa China wa barabara na miundo mbinu barani Afrika.
Lakini kuendelea kustawi kwa mradi huo wa Marekani wa Lobito unategemea rais anayeingia madarakani Donald Trump na mahusiano yake na bara la Afrika.
Maafisa wa serikali ya Marekani wanasema nchi hiyo imedhamiria kutoa dola bilioni 3 kwa mradi huo wa Lobito Corridor na miradi mingine inayohusiana. Ufadhili zaidi umetoka kwa Umoja wa Ulaya, mataifa saba yaliyostawi kiviwanda duniani G7, muungano wa makampuni ya kibinafsi unaoongozwa na mataifa ya Magharibi pamoja na benki za Afrika.
Wengi wanaamini kwamba mradi huo wa Lobito ambao Biden ataondoka afisini kabla kukamilika kwake, utaungw amkono pia na Donald Trump, kwani miongoni mwa mambo anayoyapa kipau mbele rais huyo mteule, ni kuupunguza ushawishi wa China.