Dar es Salaam. Jamii inakabiliwa na changamoto zinazohusu matukio ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kama kubaka, kulawiti, kutupa watoto, wizi wa watoto, ukeketaji na vipigo.
Matukio hayo yanazidi kuongezeka kila siku na asilimia kubwa yanatendeka katika jamii, hasa ndani ya familia.
Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uhalifu iliyotolewa na Jeshi la Polisi, katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2023, waathirika 37,448 walifanyiwa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, ikilinganishwa na waathirika 30,566 mwaka 2022.
Hilo ni ongezeko la waathirika 6,882, sawa na asilimia 22.5 na waathirika wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia wameripotiwa kutoka mikoa mbalimbali.
Temeke yameripotiwa matukio 4,751, Arusha 4,565, Tanga 3,252, Kinondoni 3,150 na Ilala 2,490, huku matukio yenye idadi kubwa ya waathirika ni kubakwa 8,691, shambulio 6,727, kudhuru mwili 5,497, kujeruhi 4,975 na lugha ya matusi 3,657.
Katika matukio yote hayo waathirika wakubwa ni watoto na kwa kipindi cha mwaka 2023, jumla ya waathirika 15,301 wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia waliripotiwa, ikilinganishwa na waathirika 12,163 katika kipindi cha mwaka 2022.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mikoa yenye idadi kubwa ya matukio ni Arusha 1,089, Morogoro 976, Tanga 884, Kinondoni 789 na Mjini Magharibi 788.
Kutokana na hali hii, Jeshi la Polisi katika maboresho yake limeunda kikosi kazi maalumu kupitia dawati la jinsia kufuatilia, kuratibu na kusimamia kwa karibu zaidi makosa dhidi ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji.
Kwa kutumia kitengo hicho cha dawati la jinsia, Jeshi la Polisi limeendelea kuinua kiwango cha uelewa wa jamii na kuimarisha huduma ya madawati ya jinsia katika vituo vya polisi, ili kuhamasisha wananchi kutoa taarifa kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Akizungumza na Mwananchi, mkuu wa dawati la jinsia na watoto Mkoa wa Morogoro, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Mwanaidi Lwena anasema katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia wameelekeza nguvu katika kutoa elimu zaidi na kwa kuanzia wameanza katika familia za kifugaji.
Anasema walianza kutoa elimu katika Kijiji cha Dakawa, wilayani Mvomero katika jamii za kifugaji, kwani ni miongoni mwa waathirika wa vitendo hivyo kwa uwepo wa ndoa za utotoni na kurithishana wake baada ya ndugu kufariki.
“Katika siku hizo 16 tuna jukumu la kutoa elimu sehemu tofauti si tu kwa wafugaji, pia katika shule za msingi na sekondari pamoja na kwenye mikusanyiko ya watu ambayo ni kwenye vituo vya magari na masoko,” anasema Mwanaidi.
Pia, anasema kutokana na ukubwa wa tatizo wanaelimisha wananchi namna ya kubaini na kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kabla ya kuleta madhara kwa kutokutoa taarifa.
“Kuna watu wanaona matukio ya kikatili, lakini wanashindwa kutoa taarifa kwa madai si mtoto wake au ndugu yake, hivyo haiwahusu, kwa kuona hilo tumeelekeza nguvu katika kutoa elimu na umuhimu wa kutoa taarifa,” anasema.
Hali hiyo inaweza kuwapa tathmini sahihi ya watu kuripoti matukio hadi mwishoni mwa mwezi Desemba na kuweza kutoa takwimu sahihi za matukio yaliyoripotiwa.
Mkazi wa Mwananyamala, Ummuh Tariq anasema tatizo kubwa wengi wanahofia kuripoti matukio haya kwa sababu ya unyanyapaa, hivyo zinahitajika kampeni za kitaifa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuripoti.
“Wanawake tunapaswa kuwa na mshikamano tupaze sauti, kwani ndio waathirika wa kwanza kwenye hili. Huu ni wakati wa kusaidiana, hatupaswi kukaa kimya,” anasema.
Mkazi wa Mbagala, Abdallah Hamisi anasema ili kukabiliana na ukatili wa kijinsia ni muhimu wa kufuata sheria zilizopo ambazo utekelezaji wake umekuwa ni kizungumkuti.
“Sheria zipo lakini utekelezaji wake ni hafifu, tunahitaji adhabu kali kwa wahusika ili iwe fundisho kwa wengine,” anasema
Mwalimu Jane Michael kutoka Kinondoni.
Pia anasema ukosefu wa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia ni tatizo linalowakabili watu wengi kwenye jamii, ndiyo maana watu wengi huamua kuficha taarifa pindi jambo hilo likitokea.
Naye, mkazi wa Tandika, Saida Msuya, anasema ukatili wa kijinsia unaendelea kwa sababu watu hawana hofu ya Mungu, kwani hata viongozi wa dini wanaowategemea baadhi yao wamekuwa kwenye mkumbo wa ukatili. Mkazi wa Rufiji, Jackson Komba kwa upande wake anasema baadhi ya mila na desturi zinaendelea kuchochea ukatili wa kijinsia, hususan kwa watoto na wanawake, hivyo, kuwa kichocheo cha kuendeleza jambo hilo.
“Tunahitaji kubadilisha mitazamo na desturi hizi za kizamani ambazo zimeendelea kuchochea ukatili kizazi na kizazi na kufikia hatua ya kufichwa kwa yale yanayotokea kwa kuhofia kugombana na familia zao,” anasema Jackson.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), Paul Sangeze anasema katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia, upo umuhimu wa kupitishwa kwa mkataba wa 190 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), ili kusaidia wafanyakazi kujua haki zao.
“Kumekuwa na changamoto nyingi, hususan ukatili wa kijinsia mahala pa kazi na wafanyakazi hawajui haki zao na imekuwa kichocheo cha kuendelea kufanyiwa ukatili na kuwaathiri kisaikolojia,” anasema Sangaze.
Naye Ofisa Programu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kitengo cha jinsia, wanawake, wasichana, watoto na watu wenye ulemavu, Nancy Masenha anasema kwa sasa wamejikita kutoa elimu na uhamasishaji kuhusu ukatili wa kijinsia.
“Kila siku tunatoa rai kwa jamii kupinga ukatili kwa kuwa jambo hili si la mtu mmoja au shirika fulani, bali ni la watu wote na kila mmoja wetu ana wajibu wa kufanya hivyo,” anasema Nancy.
Pia, anasema wanatoa msaada kwa waathirika bila kuchoka, hususan wa kisheria na kisaikolojia, kwani wapo wanaofikiria kutoa msaada wa kimwili unatosha.
Mbali na hilo, anasema wanafikiria katika uboreshwaji wa sheria, sera na uelimishaji wa jamii kuhusu ukatili wa kijinsia, hususan kwa makundi yanayolenga ya watoto, wanawake na watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake, Mshauri Mwandamizi Afya ya Uzazi, Jinsia na Familia, Dk Katanta Simwanza anasema ukatili wa kijinsia umekithiri kwa sababu ya kundi moja kuwa na mamlaka tofauti na mengine.
Hivyo katika masuala ya malezi na makuzi katika jamii watoto na wanawake, jamii haijawapatia fursa ya kuwa na mamlaka, hali inayowafanya kuwa hatarini kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Katika kushughulikia mambo hayo ni vizuri kutengeneza mipango madhubuti itakayosaidia kuondoa masuala ya ukatili na sehemu ya kuanzia katika ngazi ya familia,” anasema Dk Katanta.
Anasema asilimia kubwa ya watu wakiulizwa kuhusu kuona, kufanyiwa au kushuhudia ukatili wa kijinsia wansema ni katika familia walizotoka au walizoishi nazo.
Dk Kantanta anasema familia ndio kitalu cha kutengeneza watu wazuri au wabaya wanaofanya matendo ya kikatili hivyo jamii na taasisi zinapaswa kuwekeza kwenye familia.
Mtaalamu wa Saikolojia, Halima Ramadhan anasema ukatili wa kijinsia unaharibu afya ya akili ya waathirika, hasa watoto na wanawake.
“Ni muhimu kuweka mifumo madhubuti ya msaada wa kisaikolojia pamoja na kuhamasisha familia kutoa usaidizi wa karibu kwa waathirika.
“Waathirika wanapaswa kusaidiwa zaidi, hasa kwa kuwapatia msaada wa kisheria na matibabu ya kisaikolojia. Hawa watu wanahitaji nguvu za kuanza maisha upya,” anasema Halima.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.