Watu 11 wameripotiwa kuuawa kufuatia mashambulizi hayo ya Israel nchini Lebanon. Jeshi la Israel limedai kuwa Hezbollah imekiuka makubaliano ya wiki iliyopita kwa kuvurumisha roketi katika mlima wa Dov unaofahamika pia kama mashamba ya Shebaa, eneo la mpakani linalozozaniwa na Lebanon, Syria na Israel.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu tayari alionya kuwa jeshi lake lingefanya mashambulizi makubwa ikiwa Hezbollah ingelikiuka makubaliano hayo ya usitishwaji mapigano kwa muda wa miezi miwili.
Soma pia: Israel na Hezbollah zatupiana lawama kukiuka mpango wa usitishwaji mapigano
Kwa upande wake, Spika wa bunge la Lebanon, Nabih Berri, ameishutumu Israel kwa kukiuka makubaliano hayo kwa zaidi ya mara 50 katika siku za hivi karibuni kwa kufanya mashambulizi ya anga, kubomoa nyumba za wakazi wa maeneo ya mpakani na kukiuka anga ya Lebanon. Mpango huo ulilenga kumaliza vita vya zaidi ya mwaka mmoja kati ya Hezbollah na Israel ambavyo vilisababishwa na vita vya Gaza.
Vita vyaendelea Ukanda wa Gaza
Israel imetoa amri mpya wa kuwataka wakazi kuondoka katika eneo la kusini, huku watu 12 wakiripotiwa kuuawa hivi leo katika mji wa kaskazini mwa Gaza wa Beit Lahiya.
Soma pia: UN: Hali ya Gaza ni ya kutisha na ni janga kubwa
Mjini Cairo, viongozi wa mataifa mbalimbali walikutana kuijadili hali ya Gaza na namna ya kuwezesha usafirishaji wa misaada ya kibinaadamu. Amina Mohammed, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alifafanua.
” Tuwe wawazi, jinamizi linaloikumba Gaza sio tatizo la vifaa, ni mzozo utokanao na utashi wa kisiasa na kuziheshimu kanuni za msingi za sheria za kimataifa za kibinadamu.”
Trump aionya Hamas kuwaachia mateka
Rais mteule wa Marekani Donald Trump ameandika kwenye mitandao ya kijamii na kutoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza, akisema kuwa ikiwa hawatoachiliwa kabla hajaingia madarakani Januari 20 mwakani, basi kundi hilo litakumbwa na zilzala ambalo hawajawahi kulishuhudia.
Haikuwa wazi ikiwa Trump anadhamiria kulihusisha jeshi la Marekani kwenye mzozo huo ambao tayari umesababisha vifo vya watu zaidi ya 44,460 na kuhatarisha vita vipana zaidi vya kikanda.
Wakati juhudi za kusitisha mapigano Gaza zikiendelea, makundi ya Hamas na Fatah yanakaribia kufikia makubaliano ya kuteua kamati huru ya wataalam wa kisiasa watakaoiongoza Gaza baada ya vita. Hii ikimaanisha utawala wa Hamas utakuwa umefikia kikomo, jambo ambalo linaweza kusaidia kupiga jeki mazungumzo ya kusitisha mapigano na Israel.
(Vyanzo: DPAE, AP, Reuters, AFP)