Mdondoko wa wanafunzi tishio mkoani Dodoma

Dodoma. Idadi ya wanafunzi wanaokatisha masomo katika shule za sekondari mkoani Dodoma, imeongezeka kutoka wanafunzi 4,744 mwaka 2021 hadi 6,870, huku katika shule za msingi mdondoko ukipungua.

Takwimu hizo zipo katika kitabu cha uchumi na shughuli za kijamii za Mkoa wa Dodoma mwaka 2022, kilichoandaliwa kwa ushirikiano wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Wizara ya Mipango na Uwezeshaji na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Katika kitabu hicho kilichozinduliwa na Naibu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, kinaonyesha kuwa mwaka 2018 waliosajiliwa shuleni walikuwa ni 18,133 katika shule za sekondari za Serikali, lakini waliomaliza mwaka 2021 walikuwa ni 4,744 sawa na asilimia 26.2.

Mwaka 2019, waliosajiliwa walikuwa ni 24,062 lakini waliomaliza kidato cha nne mwaka 2022 walikuwa ni 17,192 mdondoko ukiwa ni wanafunzi 6,870 sawa na asilimia 28.6.

Pia takwimu hizo zinaonyesha idadi kubwa ya walioshindwa kumaliza shule ni wasichana ambao ni wanafunzi 3,728 sawa na asilimia 54.3 huku wavulana wakiwa ni 3,142 sawa na asilimia 45.7.

“Mkoa wa Dodoma unapaswa kuhakikisha unakuwa na kiwango cha chini cha wanafunzi wanaoacha masomo, ili kuwezesha wanafunzi kumaliza masomo yao na kufikia maarifa yaliyokusudiwa kwa ajili ya kuboresha jamii,”ilisema sehemu ya kitabu hicho.

Kwa upande wa shule za msingi, takwimu zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2019 idadi ya watoto walioacha shule walikuwa ni 6,848 ikiwa ni sawa na asilimia 5.5 ya wanafunzi wote walioandikishwa.

Kwa mujibu wa kitabu hicho, sababu za utoro zinaongoza kusababisha mdondoko, ambapo mwaka 2021 wanafunzi 6,181 waliacha shule kutokana na utoro, ikifuatiwa na sababu nyingine (615), mimba (30) na vifo (22).

Kwa mwaka 2022 walioacha shule walikuwa ni wanafunzi 5,882 huku walioacha kwa sababu za utoro wakiwa 5,331, sababu nyingine (501), mimba (20) na vifo (30).

Wilaya ya Kongwa inaongoza kwa kuwa na wanafunzi 2795 walioacha shule ikifuatiwa na Mpwapwa (1820), Chamwino (493) Dodoma Mjini (467), Chemba (269) na Kondoa (230), Bahi (71) na Kondoa Mjini (36). Hizi ni takwimu za mwaka 2021.

Hali ni hiyo hiyo kwa mwaka 2022 ambapo Wilaya ya Kongwa iliongoza kwa kuwa na wanafunzi 1,842 walioacha shule, ikifuatiwa na Mpwapwa (1,659) na waliokuwa na idadi ndogo walikuwa ni Bahi (1) na Kondoa Mji (27).

Akizungumzia nini kifanyike ili kuondokana na changamoto hiyo, Mwalimu wa Shule ya Msingi Kongwa mkoani Dodoma, Pendo Nkhwangi alisema elimu kwa wazazi, kutengeneza mazingira ya kiuchumi na walimu kuangalia adhabu wanazotoa, vinaweza kusaidia watoto kubaki shuleni.

“Jambo la kwanza ni kutoa elimu kwa wazazi, wao kama hawajapata elimu wasitengeneze mazingira ya watoto wao kutopata elimu. Pia kutengeneza mazingira ya kiuchumi kwa watoto wanaotoka katika familia zinazoishi katika mazingira magumu,”alisema.

Alisema mazingira magumu wanaoishi baadhi ya wanafunzi, yanasababisha wengi kutoelewa wanapofundishwa darasani, na kusababisha kuacha shule na wengine wanakwepa adhabu kali zinazotolewa na baadhi ya walimu shuleni.

Mmoja wa wazazi jijini Dodoma, Stella Mwakyoma alisema ushirikiano kati walimu, wazazi pamoja na wanafunzi, ni jambo muhimu katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanamaliza masomo.

“Tofauti kati ya mwalimu na mzazi inafanya ufuatiliaji wa mtoto kuwa ni mgumu…’’ alisema mzazi huyo.

Mfano katika shule ambayo mwanangu anasoma ilijitokeza mwanafunzi aliyeacha shule siku moja kabla ya wenzake kufanya mtihani wa kuhitimu shule ya msingi mwaka huu,”alisema.

Related Posts