Geita. Mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kasota, Kata ya Bugulula Wilaya ya Geita (9) amejeruhiwa kwa kuchomwa moto kwa kutumia petroli na mama yake mzazi (jina linahifadhiwa).
Tukio hilo limetokea jana Desemba 2, 2024 wakati mtoto huyo akiwa nyumbani kwao Kasota baada ya mama yake kumtuhumu kuiba Sh6,000 alizokuwa amezitunza kwenye kibubu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema tayari Jeshi la Polisi linamshikilia mama huyo na mtoto amelazwa katika Hospitali ya Nzera kwa matibabu zaidi.
Kamanda Jongo akielezea tukio hilo amesema jana saa 11:30 jioni mtoto huyo alipotoka shule wakati akivua nguo dada yake alimuona akiwa na kiasi cha pesa na alipomhoji alidai amechukua za mama yake.
“Dada yake alimuona na pesa akamuuliza alikozipata akadai ameiba za mama yake wakati anamwambia dada yake mama hakuwepo, hivyo mama aliporudi dada yake alimueleza mama akaingia ndani kwenye kibubu akakuta pesa zake zimetolewa na imebaki 600 pekee,” amesema Kamanda Jongo.
Pia, amesema baada ya kuona pesa zake hazipo alikwenda kununua petroli na kibiriti kisha kurudi nyumbani na kummwagia kisha kumchoma moto.
Amesema wasamaria wema walipoona tukio hilo walimsaidia kwa kumuokoa na kumkimbiza Hospitali ya Kasota na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao walifanikiwa kumkamata mama aliyefanya kitendo hicho.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kasota Wilaya ya Geita, Asha Omary amesema mama huyo mwenye watoto saba anawalea watoto wake mwenyewe baada ya mume kumtelekeza.
Amesema mama huyo baada ya kukamatwa amedai alifanya kitendo hicho kutokana na hasira kutokana na tabia ya mtoto ya udokozi na hakupenda kuona mwanaye akiwa mwizi.
Omary amesema kwenye kijiji hicho hilo ni tukio la kwanza la mama kumchoma mwanaye lakini kumekuwa na matukio ya wazazi kuwashambulia watoto wao kwa vipigo kupita kiasi kutokana na tabia ya udokozi.
Akizungumzia watoto sita waliobaki, Omary amedai kwa sasa wanalelewa na dada yao mkubwa baada ya mama yao kuchukuliwa na Jeshi la Polisi.
Mwenyekiti wa Asasi za Kiraia Mkoa wa Geita, Paulina Alex amelaani tukio hilo na kuliomba Jeshi la Polisi kumchukulia hatua mtuhumiwa huyo.
“Tunaomba dawati la jinsia litende haki kwa kumchukulia hatua kali ili iwe fundisho kwa wazazi wengine kwa kuwa tunaamini mzazi ndiye mlinzi wa mtoto lakini kwa hili imekuwa kinyume badala ya kuwa mzazi wa kumuongoza mtoto amemfanyia ukatili mbaya,” amesema Paulina.
Amesema baadhi ya wazazi wanaingia kwenye ukatili kutokana na umaskini, mama kutelekezwa na mzazi mwenzake hivyo kuingia kwenye msongo wa mawazo na kupata shida ya afya ya akili.
Amesema pamoja na changamoto anazopitia mzazi kwenye malezi, haitoi uhalali wa kufanya ukatili huo.