Mwenyekiti UVCCM Makongorosi auawa | Mwananchi

Mbeya. Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Tawi la Machinjioni, Kata ya Makongorosi Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya, Michael Kalinga amekutwa ameuawa na mwili wake kutelekezwa.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumanne, Desemba 3, 2024 na  mwili wake kukutwa Kata ya Mkola.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Wilbert Siwa amesema wamepata taarifa za mauaji ya Kalinga na wanaendelea kuzifanyia kazi.

Katibu wa CCM Wilaya Chunga, Charles Jockel akizungumza na Mwananchi amesema amepokea taarifa hizo leo Jumanne asubuhi kutoka kwa uongozi wa CCM Kata ya Makongorosi.

“Haijulikani alikuwa anakwenda au kurudi Makongorosi maana mwili wake umekutwa eneo la kuelekea  Kata ya Mkola,” amesema Jockel.

Amesema haijafahamika chanzo cha mauaji ya Kalinga aliyekuwa kijana tegemezi kwenye chama kwa kujituma katika shughuli mbalimbali.

“Kimsingi tumempoteza kijana ambaye alikuwa akijituma ndani ya chama hivyo tumepata mshtuko mkubwa kama chama baada ya kupotea taarifa za kuuawa kwake,” amesema Jockel.

Amesema kwa sasa wanaviachia vyombo vya dola kufanya uchunguzi kuhusu tukio hilo la kikatili.

Mbunge wa Lupa (CCM), Masache Kasaka amedai katika Mamlaka ya Mji wa Makongorosi matukio ya watu kuuawa yamekuwa yakijirudia mara kwa mara licha ya kuwepo kwa kituo kikubwa cha polisi.

“Mimi nimepata taarifa za kuuawa kwa kiongozi huyo,  leo saa 1:15 asubuhi na kwamba licha ya kufanya mauaji, maharamia hao waliondoka na usafiri wa bodaboda aliokuwa akitumia marehemu,” amesema Kasaka.

Amesema Mji wa Makongorosi kwa Wilaya ya Chunya umekuwa na matukio ya mara kwa mara watu kuuawa jambo ambalo limejenga hofu kwa wananchi kufanya shughuli za kiuchumi na kupunguza nguvu kazi kwa Taifa.

Diwani wa viti maalumu, Kata Makongorosi, Sophia Mwanautwa amesema marehemu licha ya kuwa kiongozi wa chama alikuwa akiongoza kwaya ya Agano iliyokuwa na mchango mkubwa kwa shughuli za kiserikali.

“Kwa kweli mpaka sasa tuna maswali nini kimetokea, ameuawa kifo cha kikatili kwani alikuwa hana makundi wala hatumii pombe,” amesema Sophia.

Sophia amesema kwa taarifa za awali mazishi yatafanyika kesho Jumatano, Desemba 4, 2024.

Tukio hilo ni mwendelezo wa matukio wa wanasiasa, wafanyabiashara na wanaharakati kutekwa au kuuawa na watu wasiojulikana maeneo mbalimbali nchini.

Usiku wa kuamkia jana Jumatatu, Desemba 2, 2024, Isaack Mallya (72), mkazi wa Kijiji cha Umbwe Onana, Kata ya Kibosho Magharibi, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro amekutwa ameuawa nyumbani kwake na watu wasiojulikana, huku mwili wake ukiwa ukitelekezwa nje ya nyumba hiyo.

Tukio jingie ni lile la kupigwa risasi hadi kufariki dunia kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Christina Kibiki Novemba 13, 2024.

Taarifa zilieleza kuwa, tukio hilo lilitokea Kijiji cha Njiapanda ya Tosa, Wilaya ya Iringa alipokuwa akiishi. Baada ya kushambuliwa, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Tosamaganga, alikofariki dunia.

Novemba 10, 2024 la Katibu wa CCM, Kata ya Itumba wilayani Ileje, Mkoa wa Songwe, Huruma Ally alidaiwa kuvamiwa na watu wasiojulikana na kuvunjwa miguu.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM wilayani Ileje, Maoni Mbuba alisema uvamizi huo ulitokea usiku wa kumakia Novemba 9, 2024 na chanzo hakikufahamika.

Pia, tukio la kutekwa kwa Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo, Abdul Nondo akiwa stendi ya mabasi ya Magufuli, Dar es Salaam.

Nondo alikutana na kadhia hiyo juzi Jumapili, Desemba 1, 2024 kwa kutekwa na watu wasiojulikana na usiku alitelekezwa maeneo ya fukwe za Coco, Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu asiowafahamu.

Kwa sasa anaendelea na matibabu Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

Related Posts